Thursday, 6 October 2016

Kila sehemu ina namna yake, Je, unaufahamu vizuri Utamaduni wa Wamadagaka?


Nchini Madagascar, jamii ya Malagasy ina mila na desturi ya kushangaza ambapo maiti hufukuliwa na kufanyiwa sherehe.



Familia yote huhusika katika sherehe hiyo ijulikanayo kama Famadihana lakini sasa changamoto ni kwa familia nyingi zinashindwa kuchangisha fedha za kugharamia mila hii.

Washambuliaji Wavamia Kituo huko Mandare, Kenya.


Watu kadha wanahofiwa kufariki baada ya watu wenye silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Taarifa zinasema washambuliaji hao walivamia ploti moja usiku wa manane.


Gavana wa jimbo la Mandera Ali Roba ameandika kwenye Twitter kwamba watu 6 wameuawa na mmoja kujeruhiwa.
Amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye ploti hiyo wameokolewa na maafisa wa usalama.



Bado haijabainika nani walitekeleza mashambulio hao.
Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa al-Shabaab kutoka Somalia.


Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.


Kundi la al-Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulio nchini Kenya ikiwemo mauaji ya watu 67 katika maduka ya Westgate mjini Nairobi mwaka wa 2013.


Mwezi Juni mwaka huu, wanamgambo wa kundi hilo walishambulia gari ya polisi aina ya Land Cruiser kilomita chache kutoka mji wa Mandera, na kuua maafisa watano wa polisi.


Mwaka uliopita al-Shabab walitekeleza mashambulizi katika chuo kikuu cha Garissa na kusababisha vifo vya wanafunzi 148

Monday, 18 July 2016

Marekani sasa ni mwendo wa risasi tu


Rais Barrack Obama wa Marekani amewasihi wamerakani wajizuie dhidi ya hisia kali baada ya Mmarekani Mweusi kuwapiga risasi na kuwaua maafisa watatu wa polisi katika shambulizi la pili la kulipiza kisasi dhidi ya polisi wazungu wanaowaua wamarekani weusi.

Obama ameomba uvumilivu utawale mioyo ya wakaazi wa mji wa Baton Rouge Louisiana nchini Marekani ambao sasa wanahofu ya kuzuka mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Gavin Long ambaye ni mwanajeshi wa zamani aliwapiga risasi polisi kulipiza kisasi mauaji ya Alton Sterling.

Obama aliyasema hayo katika hotuba ya moja kwa moja kupitia kwa runinga kutoka ikulu ya WhiteHouse muda mchache tu baada ya mtu mmoja mweusi kuua maafisa watatu wa polisi hukohuko Baton Rouge alikouawa mtu mweusi
Alton Sterling pasi na hatia yeyote majuma mawili yaliyopita.

Alton Sterling aliyeuawa na polisi mzungu pasi na kosa lolote
Hasira imekuwa ikitokota miongoni mwa watu weusi baada ya mtindo wa kuuawa kwa wanaume weusi na polisi wazungu kuendelea kwa muda mrefu ilihali hakuna hatua inayochukuliwa dhidi yao.

Gavin Long ambaye ni mwanajeshi wa zamani alikuwa amerekodi ujumbe katika mji wa Dallas siku chache baada ya polisi watano kuuawa mjini humo katika shambulizi lililotekelezwa kulipiza kisasi cha mauaji ya Sterling.

Hasira imekuwa ikitokota miongoni mwa watu weusi baada ya mtindo wa kuuawa kwa wanaume weusi na polisi wazungu kuendelea kwa muda mrefu
Sasa imebainika kuwa Long alikuwa ameweka video kwenye mtandao akilalamika jinsi polisi wanavyowatendea waamerika weusi ambapo alitoa wito kwa wanaume weusi kujitolea kuokoa jamii yao.

Long mwenye umri wa miaka 29 aliwahi kuhudumu kama mwanajeshi wa Marekani .
Rais Obama ameshauri watu weusi dhidi ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Polisi akisema mauaji ya kulipiza kisasi sio suluhisho la tatizo sugu la ubaguzi wa rangi bali utachochea uhasama zaidi dhidi yao na polisoi wazungu.

Sunday, 17 July 2016

Tanzania na tishio la Ugaidi


Tanzania imefaulu kuepuka mashambulizi ya kigaidi kama yaliyoshuhudia katika mataifa jirani kanda ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo Shambulizi la hivi punde dhidi ya msikiti mmoja nchini Tanzania limeibua tishio la kuibuka kwa ugaidi nchini humo.

Aliyepokonywa ubunge Longido aipinga hukumu


Aliyekuwa Mbunge wa Longido (Chadema), Onesmo Ole Nangole amekata rufaa kupinga hukumu ya kuvuliwa ubunge.

Wiki chache zilizopita, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sivangilwa Mwangesi alitoa hukumu hiyo baada ya kujiridhisha na malalamiko ya Dk Stephen Keruswa

Wa CCM kwamba mazingira katika chumba cha majumuisho ya kura hayakuwa rafiki kuakisi matakwa ya wapiga kura.

Ole Nangole amesema hayo alipokutana na baadhi ya wakazi wa jimbo hilo nyumbani kwake mjini Longido na kuwaelezea msimamo wake wa kukata rufaa.

“Hukumu haikuwa ya haki hata kidogo, hakuna fujo yoyote tuliyofanya sisi tulikuwa tukidai haki ya kutangaziwa matokeo na hiyo ni haki yetu,” amesema.

Amewaambia kwamba ameshawasilisha maombi ya kukata rufaa ambayo tayari yamepokewa.

Hatimaye Mrema aukwaa, aula wa Rais Magufuli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempa shavu mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema kwa kumteua kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 16.

Mrema akiwa na Rais Magufuli wakati wa kampenzi za uchaguzi uliyopita

Mrema ambaye amewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani wakati awamu ya pili, amekuwa akimwomba Rais Magufuli ampe kazi aliyomwahidi alipojitokeza kwenye kampeni zake na kumpigia debe.

Mbali na Mrema anayechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Eusebia Munuo ambaye muda wake umemalizika, Dk Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi na watendaji wa taasisi nyingine mbalimbali na pia amewapandisha vyeo maafisa wa Jeshi la Polisi Tanzania.

Wengine walioteuliwa ni Profesa William R. Mahalu ana kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Wizi wa nyanya wamsababishia mauti


Watu wawili, wakazi wa Wilaya ya Musoma Vijijini na Tarime mkoani Mara, wameuawa kwa tuhuma za wizi na ujambazi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Erinest Kimola amewataja waliouawa kuwa ni Nyagoma Mase (34), wa Kijiji cha Mayani, Musoma Vijijini na Sererya  Moses (20) wa Kijiji cha Masanga Tarime.

Kimola amesema Moses aliuawa Alhamisi saa mbili asubuhi katika Kijiji cha Kukikukwe baada ya kukutwa na debe la nyanya zilizodaiwa kuwa ni wizi mali ya Ibaba Tunga.

Amesema Tunga alipomkuta mtuhumiwa huyo akiwa na debe la nyanya hizo zilizoibwa shambani kwake, alipiga yowe kuita watu.

Amesema watu  walikusanyika na  kumshambulia  kwa kutumia silaha za jadi kisha kuchoma moto mwili wake na kuteketeza nyumba yake ya  nyasi na kwamba, tayari watu watatu wamedakwa kutokana na mauaji hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa awataka viongozi wazembe wajiondoe


Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi amewaonya watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea watafute sehemu nyingine ya kwenda.

Akizungumza katika ufunguzi wa duka la kampuni ya Simu ya Tigo katika mji wa Kibaigwa wilayani Kongwa,  Ndejembe amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ haitawavumilia watendaji wa aina hiyo.

“Nawapa namba ya simu hii mnipigie kwa kero yoyote, nawaahidi nitayafanyia kazi maoni yenu lakini isiwe mambo ya umbeya kwa sababu sitayafanyia kazi hayo,” amesema.

Pia, amewataka wakazi hao kufanya kazi kwa bidii ili kukuza kipato na kuacha kulalamika, kwa sababu maendeleo yanapatikana kwa kufanya kazi siyo  vinginevyo.

Saturday, 16 July 2016

Siku 3 za maombolezo zatangazwa Ufaransa kufuatia mauaji ya kigaidi

Serikali ya Ufaransa imetangaza maombolezo ya kitaiafa kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu ya wiki ijayo, baada ya lori lililoingizwa kwa kasi Alhamisi Julai 14 usiku katika umati wa watu waliokua wakitazama urushwaji wa fataki katika sherehe ya maadhimisho ya Siku kuu ya kitaifa ya Julai 14.

Shambulio hilo lililotokea katika eneo la Promenade des Anglais mjini Nice liliwaua watu 84, wengine kadhaa kujeruhiwa, na watu wengine 18 wakiwa katika "hali mbaya" kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya ndani Bernard Cazeneuve. Rais Hollande amezungumzia "mashambulizi hayo kuwa ni ya kigaidi bila shaka”.

Mwendesha mashitaka wa mjini Paris, François Molins, katika taarifa yake Ijumaa hii Julai 15 saa 11 jioni, ametoa ripoti ya hivi karibuni kuhusu shambulizi la mjini Nice. “Watu 84 wamepoteza maisha, wakiwemo watoto na vijana 10, majeruhi 202, ikiwa ni pamoja na watu 52 walio katika hali mbaya na 25 katika chumba cha wagonjwa mahututi, “ amesema François Molins.

Baada ya shambulizi hilo la mjini Nice, Rais François Hollande amelihutubia taifa Ijumaa hii katika Ikulu kimkoa ya mji wa Nice kusini mwa Ufaransa. Rais Hollande aliyekuja kushikamana na kuungana na Serikali, ameeleza kwamba Ufaransa bado inakabiliwa na vitendo vya kigaidi. "Bado tunakabiliwa na tishio," amesisitiza François Hollande.

"Wakati huu ambapo ninazungumza, watu 80 wameuawa, watu 84 hasa, na watu zaidi ya hamsini bado wako katika hali mbayakabisa, ninamaanisha, kati ya maisha na kifo ...", amesema Rais Hollande

Nchini Marekani, viongozi mbalimbali serikalini wameelezea mshikamano wao na Paris katika tukio hilo. Barack Obama amelaani vikali, "kile kinachoonekana kuwa shambulio la kutisha nchini Ufaransa."

Mgombea urais katika chama cha Republican, Donald Trump, amefuta mara moja mkutano wake na waandishi wa habari uliokua umepangwa kufanyika Ijumaa hii.

Waziri Mkuu wa Canada alionyesha kwa upande wake toka Alhamisi hii jioni mshikamano wake na Ufaransa. "Canada inahuzunishwa na shambulizi (Alhamisi) hii jioni njini Nice," alisema Justin Trudeau kwenye akaunti yake Twitter.

Nchini Brazil Kaimu Rais, Michel Temer, amelaani kitendo hiki kilichoendeshwa dhidi ya raia wasiokuwa na hatia waliokua wakiadhimisha maadili ya juu kwa wote, uhuru wa watu, usawa kati ya wananchi na udugu.

"Ujerumani iko bega kwa bega na Ufaransa katika mapambano dhidi ya ugaidi," amesema Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Ijumaa hii Julai 15 asubuhi. "Kauli yangu inatosha tu kusema tunaungana na marafiki zetu wa Ufaransa," ameongeza Angela Merkel.

"Urusi inashikamana na raia wa Ufaransa katika siku hii ngumu," amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin. "Urusi uko tayari kwa ajili ya ushirikiano wa karibu na Ufaransa katika mapambano dhidi ya ugaidi."

Waziri Mkuu wa Uturuki Binal Yildirim ameandika kwa Kifaransa kwenye ukurasa wake wa Twitter: "Uturuki, daima inashirikiana na mataifa duniani katika mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi, na inaungana naUfaransa katika siku hii ngumu."

Marais mbalimbali kutoka nchi za Afrika vile vile wameonyesha hisia zao baada yatukio hilo la kuhuzunisha lililotokea nchini Ufaransa.

Ombeni Sefue azungumza tangu alivyotenguliwa

Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue amesema baada ya miaka mingi ya utumishi wa umma sasa ni wakati wake wa kupumzika na hafikirii kujitosa katika siasa.


Balozi Sefue ambaye alikuwa kivutio kwenye televisheni kutokana na kutoa taarifa za kutenguliwa uteuzi kwa watumishi waandamizi wa umma kabla ya kibao kumgeukia, amesisitiza kuwa siasa haipo katika damu na kwamba kazi anayopenda ni kuzisaidia taasisi za ujenzi kwa kuwa ni taaluma anayoipenda.


Mbali na kuonyesha kutokuwa na mpango huo, Balozi Sefue aliupongeza utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa maelezo kuwa una kasi nzuri na kwamba kurejea kwa uadilifu ni jambo linalomfurahisha zaidi akiwataka vijana kufanya kazi kwa bidii baada ya kuaminiwa na kupewa nafasi mbalimbali.


Balozi Sefue ambaye awali hakuonekana kuwa mmoja wa watu ambao wangeng’olewa kwa sababu yoyote ile, alilazimika kuondoka Ikulu ndani ya siku 123 tangu Rais Magufuli aapishwe kuwa Rais na siku 67 tangu balozi huyo atangazwe kuendelea na wadhifa wake. Uteuzi wake ulitenguliwa Machi 6 na nafasi yake kuchukuliwa na Balozi John Kijazi.


Baada ya kimya cha muda mrefu, Mei mwaka huu, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi wa Utawala Bora), Dk Laurean Ndumbaro alikaririwa akisema kuwa baadhi makatibu wakuu walioachwa katika uteuzi na Rais, wapo waliostaafu kwa mujibu wa sheria, akiwamo Balozi Sefue.

Ndessamburo ataka CHADEMA ijengwe


Aliyekuwa mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amesema inahitajika nguvu kukijenga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na Serikali kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara nchini.

Ndesamburo ambaye ni mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro amesema  wakati akifungua mkutano wa faragha wa  makatibu na wenyeviti wa chama hicho wa wilaya.

“Kujenga chama siyo mchezo, tunakoeleka siyo kuzuri tukaze buti na tutekeleze tunachokisimamia kwa vitendo kwa sababu wenzetu wanatumia mbinu nyingi kuhakikisha wanatukwamisha,” alisema.

Amefafanua kuwa kutokana na chama hicho kuzuiliwa kufanya mikutano ya hadhara, viongozi wa kata hadi Taifa wanatakiwa kuongeza nguvu ya ziada na kutumia mbinu mbadala kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao.

Mratibu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema wameamua ‘kutafuna mbuyu’ chini kwa chini kutokana kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara ili kuhakikisha chama hicho hakiyumbi.

Mapinduzi ya Kijeshi yafanyika Uturuki


Kundi moja la kijeshi nchini Uturuki linasema limechukua udhibiti wa nchi, huku madaraja jijini Istanbul yakifungwa na ndege za kijeshi zikionekana kupaa katika anga ya Ankara.

Mapema waziri mkuu Binalo Yildirim alitangaza kuwepo kwa “hatua zisizo halali” zilizochukuliwa na “kundi” la kijeshi, na kusisitiza kuwa hakuna mapinduzi ya kijeshi. Alisema serikali bado inadhibiti nchi.

Magari yamezuiwa kuvuka katika madaraja yanayovuka mto Bosphorus jijini Istanbul.

Kumekuwa na taarifa za milio ya risasi katika mji mkuu Ankara, na pia milio ya risasi karibu na ikulu ya rais.

Kumeripotiwa pia mlipuko karibu na makao makuu ya mkuu wa jeshi.
Kituo cha CNN Idhaa ya Uturuki kimeripoti kuwa Rais Recep Tayyip Erdogan yuko "salama” lakini hakikufafanua zaidi.

Erdogan amezungumza na CNN Turk kupitia Facetime
Baadaye, Bw Erdogan ameambia kituo cha habari cha CNN Turk, kwenye mahojiano ya webcam, kwamba kitendo cha leo kimechochewa na kuwepo kwa "mfumo sambamba".

Amesema jaribio la mapinduzi litakabiliwa kwa "hatua ifaayo" na kuwataka raia wa Uturuki wajitokeze barabarani.
Mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter na YouTube ilizimwa muda mfupi baada ya taarifa za mapinduzi ya serikali kutokea.

Ney wa Mitego ahojiwa na Polisi


Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama  Ney wa Mitego amehojiwa kituo cha Polisi Kati na kupewa dhamana kufuatia tuhuma zinazomkabili.

Kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema msanii huyo alihojiwa juzi kituoni hapo na yupo nje kwa dhamana, huku jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na  tuhuma zinazomkabili.

“Ni kweli juzi mchana  tulimhoji Ney wa Mitego na yupo nje kwa dhamana kuhusu kukamatwa kwake nitatoa taarifa  kwa nini tulimkamata,”amesema Kamanda Sirro.

Friday, 15 July 2016

Wasusia mazishi ya ndugu yao baada ya Mahakama kutupilia mbali shauri lao


Ndugu wamesusa kushiriki maziko ya marehemu Andrew Daffa  kutokana na Mahakama kumpa haki hiyo mjane wake badala ya baba mzazi aliyetaka yafanyike mkoani Tanga.

Kususa kwa ndugu hao kunatokana na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kutupilia mbali maombi yaliyofunguliwa na baba wa marehemu huyo akitaka mwili wa mtoto wake kuzikwa kijijini kwao mkoani humo.

Mwili huo umezika  katika makaburi ya Yombo Vituka, Dar es Salaam chini ya ulinzi wa polisi.

Awali, mwili wa Daffa ulizuiwa kuzikwa kutokana na maombi namba 240 ya mwaka 2016 yaliyofunguliwa na baba wa marehemu,  Charles Joseph aliyetaka apewe kibali cha kumzika mwanaye katika Kijiji cha Vigiri mkoani humo kwa madai kuwa alizaliwa huko.

Mvutano huo ulikuja kufuatia mjane wa Daffa, Glory Charles kutaka kupewa haki ya kuzika mwili wa mumewe katika makaburi yaliyopo Yombo Vituka kwa kile alichoieleza eneo hilo ndilo walilozika watoto wao watano.

Kutokana na mvutano huo, Jumanne wiki hii, Mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya mwili huo kuzikwa Tanga.

Daffa alifariki dunia Jumatano ya wiki iliyopita katika Hospitali ya Amana.

Hakimu Adolf Sachore amesema chanzo cha familia ni baba, mama na watoto, hivyo mahakama imetoa kibali mwili  huo uzikwe walipozikwa watoto wake.

Makumi wauawa katika Shambulizi la kigaidi Mjini Nice, Ufaransa


Zaidi ya watu 70 wameripotiwa kuuawa katika shambulio lililotokea katika mji wa Nice kaskazini mwa Ufaransa.

Lori lililokuwa likienda mwendo kasi lilijiingiza katika mkusanyiko wa watu waliokuwa wakiangalia maonesho ya fataki kuadhimisha siku ya kitaifa ya Bastille, ambayo huja na shamra shamra kila mwaka.

Mwendesha mashtaka katika mji wa Nice, Jean- Michel Pretre amesema lori hilo liliendelea kutembea kilo mita mbili kabla ya polisi kumpiga risasi dereva.

Bunduki na makombora yameripotiwa kukutwa ndani ya lori hilo.

Wakazi wa mji huo wa Nice wameshauriwa kutulia majumbani.

Rais Francois Hollande amerudi mjini Paris kwa ajili ya kufanya kikao cha dharura.

Hali ya tahadhari iliyowekwa toka kutokea kwa shambulio lililofanywa na Islamic State mjini Paris, bado iko palepale nchini Ufaransa.

Mkoa wa Mbeya wakataa tuzo ya usafi


Si jambo la kawaida kukataa tuzo hususan kwa Waafrika lakini Mkuu wa Mkoa  wa Mbeya Amos Makalla ameikataa tuzo hiyo  kwa madai kuwa jiji lake halijastaili kwani bado ni chafu.

 Makalla ameungana na wananchi wa jiji hilo kupinga kutajwa kushinda nafasi ya kwanza kwa usafi nchini, na kudai bado  limejaa takataka.

Makalla amesema hajatambua  vigezo vilivyotumika kwani jiji halina hata bustani za kupumzika wananchi, limejaa takataka karibu na bustani za maua hususan eneo la Kabwe na mitaa mbalimbali.

Awali  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alilitaja Jiji la Mbeya kwamba limeongoza kwa makundi ya majiji kwa usafi, wakati Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ikiongoza nchini na Kinondoni ikiongoza kwa kundi la manispaa za majiji.

Mkazi wa Uwanja wa Ndege, Daudi Mahenge amesema ipo haja kwa  Serikali kutoa taarifa sahihi kwani Mbeya haijawahi kuwa safi.

BAVICHA wakubali yaishe Mkutano Mkuu wa CCM


Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Mkoa wa Rukwa  limetangaza kuwa hawatakwenda  kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bavicha mkoani humo, Aida Khenan amesema wametii agizo la Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe la kuwazuia kwenda Dodoma.

“Tumeheshimu agizo la Mbowe ambalo limejaa busara na hekima kubwa  japokuwa  tulikuwa tayari kwenda Dodoma,” amesema Khenan ambaye pia  ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema).

Katibu wa Bavicha Mkoa wa Rukwa, Deogratis Kashatila  ameishauri Serikali  ya CCM isivizuie  vyama  vya  siasa kufanya mikutano kwa kuwa nchi ilisharidhia mfumo wa vyama vingi kwani ni kinyume na katiba.

Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi alinukuliwa akisema baraza hilo limeamua kuzuia mkutano huo wa CCM kutokana na tamko la Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yote ya kisiasa. “Hakuna mkutano wowote wa siasa unaotakiwa kufanyika, iweje CCM waandae mkutano huo, sisi vijana wa Chadema tutakuwapo Dodoma kuzuia,” amesema

Ombaomba wapato 60 wakamatwa jijini Dar

Katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ombaomba 60 wamekamatwa katika msako unaoendelea.

 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe amesema wamewakamata 60 na operesheni inaendelea.

“Ukamataji wa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam unaendelea, 60 wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka,”  amesema Dk Magembe.

Amesema miongoni mwa ombaomba hao, wapo watoto wenye umri wa chini ya miaka 18   ambao wamepelekwa katika vituo vya watoto yatima, kikiwamo Kituo cha Kurasini.

Dk Magembe amesema  bado ombaomba wamekuwa wakionekana jijini  Dar es Salaam kutokana na kuwapo kwa watu wanaotoka mikoani na kuingia katika makundi ya ombaomba kila siku.

Amesema  uongozi wa mkoa unashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoa elimu mikoani kuhusu operesheni ya kuwaondoa ombaomba.

Amesema ombaomba wengi wanakuja kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Awali  Makonda alitangaza operesheni kubwa ya kuondoa ombaomba katika Jiji la Dar es Salaam.

Aliwataka polisi kwa kushirikiana na ustawi wa jamii kuwaondoa ombaomba wote waliopo mitaani.

Pia, Makonda amepiga marufuku wananchi wanaowapa fedha ombaomba  kuacha mara moja ili wajitafutie riziki wenyewe kwa kufanya biashara au kurudi mikoani kujishughulisha na kilimo.

Mahakama yatupilia mbali pingamizi Tundu Lissu


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na washtakiwa wa kesi ya uchochezi, akiwamo mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu dhidi yake ikisema ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi mwisho.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, mwandishi, Idrissa Jabir Yunus na mchapishaji wa gazeti hilo, Ismail Mehboob.

Hakimu Thomas Simba amesema kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo tofauti na inavyodhaniwa na washtakiwa hao.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi hiyo  kwa kuandika na kuchapisha makala katika gazeti la Mawio la Januari 14-20, mwaka huu yenye kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar.”

Awali, Wakili wa washtakiwa hao,  Peter Kibatala aliweka pingamizi akidai Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo kwa  madai kuwa Kifungu cha Sheria ya Magazeti kilichotumiwa kuwashtaki  kinatumika Tanzania Bara tu na si Zanzibar.

Amedai Tanzania ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano inayojitegemea na kwamba mashtaka hayo yanazungumziwa kuwa yanasababisha chuki dhidi ya  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikikiliza.

 Hata hivyo, katika uamuzi wake jana, Hakimu Simba alifafanua kuwa  kifungu cha Sheria ya Magazeti kilichotumika kuwashtaki kinatumika hata Zanzibar.

Pia, Mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja nyingine ya pingamizi la upande wa utetezi la uhalali wa shtaka la tatu, ikisema liko mahakamani kiusahihi.

 Wakili Kibatala katika pingamizi lake kuhusiana na shtaka hilo alidai maelezo hayakidhi vigezo vya kisheria kulifanya liwe la uchochezi na hayako wazi ili washtakiwa wajitetee, hivyo aliiomba mahakama  kulifuta.

 Hakimu Simba alikubaliana na hoja za upande wa mashtaka kuwa shtaka hilo ni sahihi na linajitosheleza.

Thursday, 14 July 2016

Donald Trump asubiriwa kumtangaza msaidizi wake

Mgombea mtarajiwa wa chama cha Republikan Donald Trump anaendelea kupunguza watu anaotarajiwa kuchagua mgombea mwenza wa urais na anapanga kutoa tangazo lake Ijumaa.

Trump amesema katika mtandao wake wa Tweeter kwamba atatangaza saa 5 asubuhi Ijumaa katika jimbo la New York.

Kati ya wanaotarajiwa kupewa nafasi ni pamoja na Gavana wa Indiana Mike Pence ambaye alikuwa nae katika hafa ya uchangishaji fedha jumanne , spika wa zamani wa bunge la Marekani Newt Gingrich , na Gavana wa new Jersey Chris Christie .

Christie aliwahi kuwa mgombea wa chama cha republican na mpinzani wa Donald Trump katika uchaguzi wa awali ila aliamua kumuunga mkono mapema Trump baada ya kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Uhaba wa nishati ya umeme kuikumba Ghana


Ukosefu wa nguvu za umeme umetokea kwenye taifa la pili kwa ukubwa katika eneo la Afrika magharibi la Ghana.
Ukosefu wa nguvu za umeme umetokea kwenye taifa la pili kwa ukubwa katika eneo la Afrika magharibi la Ghana huku Rais John Dramani Mahama akilaumu wazalishaji wa mafuta katika Niger Delta nchini Nigeria.

Uchumi wa Ghana uliwahi kukua kwa haraka katika eneo hilo, lakini ukosefu wa umeme wa mara kwa mara, Serikali kutumia fedha zaidi pamoja na kuanguka kwa bei za bidhaa zinazotoka nchini humo zimepelekea Shirika la Fedha Duniani, IMF kutoa msaada wa dola bilioni moja kama njia ya kuokoa uchumi.

Rais Mahama amezungumzia tatizo lililoanza mapema mwaka huu baada ya kundi la wanamgambo kwa jina la Niger Delta Avengers, kuanza kuharibu mabomba yakusafirisha mafuta pamoja na vifaa muhimu katika eneo la Niger Delta ambapo Ghana inaagiza mafuta yake.

Wanajeshi wa Uganda waingia nchini Sudan Kusini

Hali ya usalama bado ni ya wasiwasi nchini Sudan Kusini licha ya hali ya utulivu kurejea, baada ya mapigano ya mwishoni mwa wiki iliyopita. Hakuna mapigano Alhamisi hii Julai 14 kwa siku ya tatu mfululizo.

Lakini nchi nyingi za kigeni zimeendelea kuwarejesha nyumbani raia wao. Na Alhamisi hii asubuhi, msafara wa majeshi ya Uganda umeingia katika ardhi ya Sudan Kusini, ukiwa na sababu rasmi, kuwarejesha nyumbani raia wa Uganda.

Askari zaidi ya mia moja na malori hamsini kutoka Uganda wameingia katika ardhi ya Sudan Kusini Alhamisi hii Julai 14. Hatua hiyo ilitangazwa siku moja kabla, na msafara ulichelewa kutokana na uamuzi wa Serikali ya Sudan Kusini kufunga mipaka yake.

"Vikosi vyetu vya vya jeshi viko njiani vikieleea katika mji wa Nisitu, kilomita 30 ana mji wa Juba. Hatuna nia ya kwenda mbali zaidi ya mji wa Nisitu, wala nia ya kwenda hadi katika mji wa Juba. Tayari kuna raia 2,000 wa Uganda ambo wanasubiri kurejeshwa nyumbani. Tunaamini kwamba operesheni hii itadumu siku 10, hadi 20, "amesema msemaji wa serikali ya Uganda.

Kuhusu muda wa operesheni, kumekuwa na hisia tofauti. Afisa wa Idara ya Ujasusi ya Uganda amelielezea shirika la habari la AFP kwamba vikosi vya jeshi la Uganda vnaweza kukaa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa mjini Juba, na kuongeza, "tumefanya hivyo katika siku za nyuma, kwa nini tusifanye hivyo kwa sasa? "

Marekani kwa upande wake, tayari imetangaza kwamba imewatuma askari 47 katika mji wa Juba, "kulinda raia na mali ya Marekani." Serikali ya Marekani imeongeza: "kwa sasa mjini Djibouti, askari wa ziada wako tayari kutumwa nchini Sudan Kusini kama itahitajika. "

Rwanda yapuuzia kumkamata Rais wa Sudan Kaskazini


Serikali ya Rwanda imepuzuia mbali ombi la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai yenye makao yake makuu huko Hague Uholanzi ICC ya kumkamata rais wa Sudan Omar el-Bashir.

Rais Bashir atahudhuria kongamano la viongozi wa Afrika linaloandalia mjini Kigali wikiendi hii.

Rais Bashir atahudhuria kongamano la viongozi wa Afrika linaloandalia mjini Kigali wikiendi hii.

Waziri wa maswala ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo amesema kuwa ombi la ICC kupitia kwa barua rasmi walioiandika siku mbili zilizopita haina uzito wowote.

Mapema juma hili mahakama ya ICC iliyashtaki mataifa ya Djibouti na Uganda kwa baraza kuu la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kukosa kumkamata rasi Bashir alipozuru mataifa hayo.
Hii sio mara ya kwanza ziara ya rais Bashir imezua utata.

Mwaka uliopita mahakama ya Afrika Kusini ilimpata na hatia rais Jacob Zuma kwa kukiuka amri ya mahakama ya kumtia mbarano rais Omar el Bashir alipohudhuria mkutano wa umoja wa Afrika mjini Johannesburg nchini humo.

Waziri wa maswala ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo
Moja ya mada kuu katika kikao kijacho cha Kigali, itakuwa uhusiano baina ya bara la Afrika na mahakama hiyo ya ICC.

Viongozi wa Afrika wamekuwa wakishikilia kukutu dhana kuwa dhamira kuu ya mahakama hiyo ni kuwahukumu viongozi wa Afrika ,huku viongozi wa mataifa ya magharibi wakiruhusiwa kuponyoka mkono wa sheria licha ya kuwepo kwa madai dhidi yao.

ICC iliyashtaki mataifa ya Djibouti na Uganda kwa baraza kuu la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kukosa kumkamata rasi Bashir alipozuru mataifa hayo.

Mahakama hiyo kwa upande wake inasema kuwa imekuwa ikijaribu kutoa haki kwa maelfu ya waafrika ambao wamedhulumiwa.

ICC inamtaka bwana Bashir akamatwe kwa makosa ya mauji ya halaiki katika jimbo la Darfur Sudan.
Rais Bashir amekanusha madai yote dhidi yake.

Wednesday, 13 July 2016

Dr. Kizza Besigye aachiliwa kwa dhamana


Mahakama kuu nchini Uganda, imemuachia kwa dhamana kiongozi mkuu wa upinzani na aliyekuwa mgombea Urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Dr. Kizza Besigye.

Mwanasiasa huyo wa chama cha The Forum for Democratic Change, FDC, alikuwa anazuiliwa kwenye gereza la Luzira akituhumiwa kwa kosa la uhaini.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Wilson Masalu Musene, amesema kuwa dhamana anayopewa Besigye ni ishara ya haki ya kisheria ya mtuhumiwa, ya kwamba hana hatia hadi pale atakapopatikana na hatia au mtu kukiri kosa.

Jaji Masalu ameongeza kuwa, "kipekee Besigye kama watuhumiwa wengine, alikuwa anahudhuria vikao vya kesi yake kwa uaminifu".

Besigye, mgombea wa nafasi ya Urais kwa zaidi ya mara nne na kushika nafasi ya pili kwenye chaguzi zote, mwezi February mwaka huu baada tu ya kumalizika kwa uchaguzi wa rais, alijiapisha ambapo baadae alishtakiwa kwa kosa la uhaini.

Kwa mujibu wa sheria za Uganda, kifungu namba 23 cha Penal Code, kinasema kuwa, mtu akipatikana na hatia ya kosa la uhaini, hukumu yake ni adhabu ya kifo.

Makosa mengine yanayomkabili Besigye ni pamoja na kujitangaza mshindi kinyume cha sheria, kukaidi amri halali ya polisi na kuitisha maandamano kinyume cha sheria pamoja na kula kiapo kinyume na sheria za nchi.

Viongozi wa BAVICHA kizimbani


Viongozi wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, BAVICHA, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini, wakikabiliwa na mashtaka ya kukutwa na maandishi ya uchochezi.

Mahakama imewaonya washtakiwa hao, kutofanya kosa lolote la jinai wakiwa nje kwa dhamana, vinginevyo dhamana yao itafutwa.

Washitakiwa hao wametajwa kuwa ni Patrobas Katambi (33), mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Julius Mwita (30) Katibu wa Bavicha Taifa mkazi wa Dar es Salaam na George Tito (28) Mwenyekiti wa baraza hilo mkoani Mbeya.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa serikali, Beatrice Nsana na Lina Magoma huku upande wa washtakiwa wakitetewa na mawakili watatu wa kujitegemea, Fred Kalinga, John Gigongo na Isack Mwaipopo.

Akiwasomea shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi James Karanyemaha, Wakili wa Serikali Lina Magoma alisema washtakiwa wanadaiwa kukutwa na maandishi yenye lugha ya uchochezi kinyume na Kifungu cha 32(2) cha Sheria ya Magazeti Namba 229 iliyofanyiwa marejeo 2002.

Alidai Julai 9, mwaka huu katika baa ya Cape Town Manispaa ya Dodoma, washtakiwa walikutwa na fulana zenye maandishi ya “Mwalimu Nyerere Demokrasia Inanyongwa na Tuungane tuukatae Udikteta Uchwara.”

Washtakiwa walikana shtaka hilo huku upande wa mashtaka ukisema unaendelea na upelelezi na kuomba tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo. Alisema hauna pingamizi la washtakiwa hao kuachiwa kwa dhamana.

Hakimu Karayemaha alisema dhamana iko wazi kwa washtakiwa kwa kila moja kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika wenye barua kutoka kwa mtendaji kata na wawe na mali isiyohamishika, yenye thamani isiyopungua Sh milioni moja.

Pia aliwataka wadhamini kuhakikisha washtakiwa wanahudhuria mahakamani kila tarehe ya kesi na kama kuna sababu ya msingi mdhamini afike mahakamani kutoa taarifa. Alisema mshtakiwa ambaye atafanya kosa lolote la jinai akiwa nje kwa dhamana, dhamana yake itafutwa.

Washtakiwa walitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo imepangwa kutahjwa tena Julai 26, mwaka huu. Katika kesi nyingine, Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema Taifa, Joseph Kasambala (32) alipandishwa kizimbani kujibu shtaka la kutumia maandishi ya uchochezi.

Ilidaiwa na Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana kuwa Julai 9, mwaka huu katika Kituo cha Kikuu cha Polisi, mshtakiwa alikutwa akiwa na fulana yenye maandishi ya Mwalimu Nyerere Demokrasia imenyongwa. Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Julai 26, mwaka huu.

Watumishi hewa kizuizi cha ajira zaidi ya 70 elfu


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema serikali imelazimika kusitisha ajira mpya za watumishi 71,496 serikalini, mwaka huu hadi pale tatizo la watumishi hewa litakapopatiwa ufumbuzi.

Akifungua mafunzo kuhusu maadili ya viongozi wa umma kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji Ikulu Dar es Salaam jana, Kairuki alisema tangu oparesheni ya kutafuta watumishi hewa ianze hadi sasa watumishi 12,246 wameshaondolewa.

Kairuki alisema tatizo la watumishi hewa nchini bado ni kubwa kwani uzoefu unaonesha kuwa nchi nyingi zilizokumbwa na tatizo hilo, ni asilimia ndogo tu ya watendaji ndio iliyokuwa inawajibika.

Alisema kwa sasa serikali imelazimika kusimamisha masuala mengi ya utumishi wa umma ili ipate taarifa kamili ya aina ya watumishi waliopo, na kwamba ma-DED hao kuhakikisha wanasimamia vyema oparesheni hiyo kwani hadi sasa watumishi hewa waliobainika, takribani asilimia 90 wanatokea katika Serikali za Mitaa.

Aidha, Kairuki alisema pamoja na kugundulika kuwa tatizo la watumishi hewa ni kubwa nchini, pia serikali imebaini kuwepo kwa watumishi watoro wasiotimiza wajibu wao.

“Nawataka mkahakikishe mnawabana hawa maofisa utumishi, haiwezekani kuwepo na tatizo la watumishi hewa kubwa kiasi hiki huku pia kukiwa na tatizo la watumishi watoro, hawa maofisa kwani walikuwa na majukumu gani?” Alihoji Kairuki.

Alisema endapo serikali itabaini kuwa maofisa utumishi hao wamehusika katika matatizo hayo ya watumishi hewa na utoro, wataondolewa mara moja. “Serikali haina mchezo kila ofisa katika eneo lake, awe ofisa elimu, afya na kilimo wafanye kazi zao,” alisema.

Mtoto anusurika kuliwa na ndege tai Australia


Tai mmoja mkubwa nusura afanye kitendo cha kustaajabisha ,,, tai huyo alijaribu kumtwaa mvulana mmoja na kupaa naye nchini Australia.

Umati wa watu uliokuwa katika hifadhi ya Alice Springs Desert Park ulipigwa na butwaa tai huyo alipojaribu kumbeba mtoto wakati wa kurekodi kwa onyesho moja la wanyama pori.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa ''ilikuwa ni kama tai huyo aliona mnyama mdogo ambaye alitaka kumfanya mlo wake''

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa ''ilikuwa ni kama tai huyo aliona mnyama mdogo ambaye alitaka kumfanya mlo wake''.

Mvulana huyo anayekisiwa kuwa kati ya miaka 6-8 aliepuka kwa kupiga kamsa na mwishowe ndege huyo mkubwa akapaa na kutoweka.

Mvulana huyo alitibiwa baada ya makucha ya ndege huyo kumgwara usoni.

Hata hivyo wahudumu wa hifadhi hiyo waliingilia kati na kumfukuza tai huyo.

Bi Christine O'Connell kutoka Horsham katika jimbo la Victoria aliyenasa tukio hilo kwa kamera anasema tai huyo alimvamia mtoto huyo akijaribu kumuinua.

Hata hivyo wahudumu wa hifadhi hiyo waliingilia kati na kumfukuza tai huyo.

Wasimamizi wa hifadhi hiyo wamemuondoa tai huyo kwenye onyesho hilo.

Waandalizi wa onyesho hilo walifungasha virago vyao kwa haraka baada ya tukio hilo maarufu.

Wasimamizi wa hifadhi hiyo wamemuondoa tai huyo kwenye onyesho hilo.

Monday, 11 July 2016

Mwanamke apinga unyanyasaji unaotekelezwa na Polisi nchini Marekani


Maandamano nchini Marekani kupinga mauaji ya wanaume weusi na polisi wazungu yameendelea katika mji wa Baton Rouge, Louisiana.

Makumi ya waandamanaji walikamatwa huku polisi wakiendeleza sera yao ya kuwakamata kamata weusi wanaopinga mauaji hayo ya polisi.

Viongozi wa vuguvugu la Black Lives matter walikamatwa
Matukio ya makabiliano hayo yameibua hofu ya kuenea kwa uhasama na ubaguzi wa rangi. Hata hivyo picha moja imeibua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii kote duniani.

Polisi wameendeleza kauli ya kuwa na msimamo mkali dhidi ya weusi
Picha hiyo inaonesha maafisa wawili wa polisi waliojihami hadi kwenye kisigino wakijiandaa kumkabili kipusa mmoja mweusi ambaye hakuwa amejihami kwa namna yeyote ila kwa ujasiri wa kupinga mauaji hayo ya wanaume weusi jumanne iliyopita.

Picha hiyo ya mwanamke huyo imefananishwa na ile ya ''Tank Man'' ya China
Picha hiyo ilipigwa na mpiga picha wa shirika la habari la Reuters Jonathan Bachman, ambaye ni mkaazi wa mji wa New Orleans.

Waamerika wengi waliosambaza picha hiyo wameifananisha na ile picha ya mwanaume aliyekuwa akipigania haki za wenyeji nchini China wakati walipokabiliwa na wanajeshi wakiwa wamejihami na vifaru vya kijeshi.

Wapiganiaji haki za kibinadamu na haswa haki za wamarekani weusi wamekuwa wakijadili sadfa ya kuwa taifa linalodai kuwa kitovu cha demokrasia kinatumia mbinu za kidhalimu zilizotumika mataifa ya kikomunisti karne iliyopita.

Wanaume weusi wamejipata pabaya mikononi mwa polisi wazungu
Mpiganiaji haki za weusi Shaun King ambaye pia ni mwandishi wa jarida la New York Daily anasema kuwa ni jambo la kufedhehesha mno mno kuwa picha hiyo ya kihistoria inatokea Marekani mwaka huu wa 2016, weusi wakipigana dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Alton Sterling ambaye mauaji yake yaliibua maandamano Marekani
Kipusa huyo anadaiwa kukamatwa na polisi lakini hakuna anayemfahamu wala anayejua kilichomkuta mikononi mwa polisi.

Sudan Kusini hali si shwari, ndege za kivita zatumika katika mapigano


Uganda imetangaza kwamba itatuma wanajeshi wake katika mpaka wake na Sudan Kusini baada ya mapigano kuzuka upya nchini humo.

Msemaji wa jeshi la Uganda Paddy Ankunda amesema wanajeshi hao watatumwa kuzuia mapigano kuenea hadi maeneo ya Uganda.

Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa mataifa, linawaomba viongozi wakuu wa serikali ya Sudan Kusini, kuyadhibiti majeshi yao.

UN inasema kuwa mashambulio dhidi ya raia na makao makuu pamoja na kambi ya Jeshi ya Umoja wa mataifa, ni uhalifu wa kivita.

Walinda amani wawili wa umoja wa mataifa kutoka Uchina, wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Umoja wa mataifa unasema kwamba, mataifa jirani na Uchina yanafaa kujiandaa kutuma majeshi zaidi nchini humo, ikiwa hali ya usalama itaendelea kudorora .

Wanajeshi wakishika doria mabarabarani katika mji mkuu wa Juba
Hata hivyo baraza hilo litahitaji kuidhinisha vikosi zaidi.

Kwa sasa wanajeshi wa umoja wa mataifa walioko Juba ni elfu 13 pekee.
Mapigano yazuka tena Juba, Sudan Kusini.

Umoja wa mataifa unasema kuwa, walinda amani wanafaa kutumia kila mbinu kuwalinda raia.

Waandishi wa habari wameiambia BBC kuwa ndege za helikopta zimetumika kurusha risasi pande zote huku zikishambulia majengo ya maskani ya bwana Machar.

Wanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir na wale watiifu kwa Riek Machar wamekuwa wakipigana tangu Alhamisi.

Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika makao makuu ya kambi ya kijeshi ya umoja wa mataifa.

Vifaru vya kivita vinaonekana katika barabara za mji mkuu Juba, huku wakaazi wakijifungia ndani ya majumba yao. Mamia ya watu wameuwawa tangu ghasia hizo zianze upya siku tano zilizopita.

Mapigano yaliyoripotiwa kutokea katika uwanja wa ndege mjini Juba, yamesitishwa, huku mashirika mbalimbali ya usafiri wa ndege kuingia na kutoka mjini Juba, likiwemo shirika la ndege nchini Kenya -KQ yamesitisha usafiri.

Marekani yawaonya wakuu wa Sudan Kusini na kuwataka wakomeshe mapigano


Serikali ya Marekani, imetaka kusitishwa mara moja kwa vurugu nchini Sudan Kusini, baada ya kutokea mapigano mapya, jijini Juba, mapigano yanayotishia kuvunjika kwa mkataba wa amani kwenye taifa hilo jipya kabisa duniani.

Mapigano haya ni ya kwanza kati ya jeshi la Serikali na wanajeshi waasi mjini Juba, toka kurejea nyumbani kwa kiongozi wao, Riek Machar mwezi April mwaka huu, na kuchukua nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais, kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu nchini humo kwa miaka 3.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani, imeagiza kuondoka nchini humo kwa raia na wafanyakazi wake, na kulaani taarifa kuwa raia wa kawaida wemeshambuliwa, ambapo mpaka sasa watu 150 wamekufa kutoka kila upande.

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, akitia saini kwenye mkataba wa usitishaji wa mapigano nchini mwake, 26 August 2015
UN Photo/Isaac Billy
Utawala wa Washington, unawataka viongozi wote wawili, wanasiasa na makamanda wa vikosi, kuagiza wanajeshi wao kujiepusha na makabiliano ili kuzuia mapigano zaidi, na kuagiza warudi kwenye makambi yao, amesema msemaji wa wizara hiyo, John Kirby.

"Marekani imedhamiria kuhakikisha inachukua hatua stahiki ili kuwawajibisha wahusika wa machafuko haya mapya ambayo ni wazi yanakiuka sheria za kimataifa zinazolinda binaadamu, ikiwemo kushambuliwa kwa kambi ya tume ya umoja wa Afrika nchini humo, UNMISS.

Machafuko haya yamejiri siku moja tu baada ya taifa hilo kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 5 toka taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa Sudan, Jumamosi ya wiki iliyopita, Julai 9.

Machafuko haya mapya yalianza Ijumaa ya wiki iliyopita na kuendelea hadi mwishoni mwa juma, ambapo wananchi wameonekana wakikimbia makazi yao mjini Juba, huku umoja wa Mataifa ukisema kuwa roketi na silha nzito za kivita zimetumiwa, halikadhalika ndege za kivita na vifaru.

Onyo hili la Marekani, linatolewa wakati huu baraza la usalama la umoja wa Mataifa, likifanya kikao chake cha dharula, ambapo umezitaka pande zote mbili kuzuia wanajeshi wao kukabiliana.

Nchi 15 wanachama za baraza la Usalama, zimewataka Rais Salva Kiir na makamu wake wa kwanza wa Rais Riek Machar, kuheshimu mkataba wa amani na kuhakikisha wanatekeleza maazimio ya usitishaji wa kudumu wa mapigano.

Mapigano yazuka Sudan Kusini


Msemaji wa jeshi tiifu kwa makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar ameiambia BBC kuwa majeshi yao yanakabiliana na jeshi la serikali tiifu kwa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Kanali William Gatjiath amesema kuwa wanajeshi watiifu kwa bw Machar wamevamia mji mkuu wa Juba kutoka pande zote .

Kanali Gatjiath anasema wanajeshi hao wanalipiza kisasi kufuatia mashambulizi makali kutoka kwa jeshi la rais Kiir.

Serikali haijasema lolote tangu machafuko hayo yaanze muda mchache uliopita.

Awali Wanajeshi wanamuunga mkono makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar walisema kuwa kambi yao ilishambuliwa usiku wa kuamkia leo kwa risasi na bunduki nzito nzito.

Rais Salva Kiir na makamu wa rais Riek Machar wamewasihi wafuasi wao kulinda amani.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini unasema kuwa kulitokea ufyatulianaji wa risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba..
Maeneo yanayodhaniwa kuathirika sana ni yale ya Jebal.

Ujumbe huo unasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa rasasi ulishuhudiwa karibu na kambi ya umoja wa mataifa.

Siku za hivi majuzi ziaidi ya watu 100 wanaripotiwa kuuawa mjini Juba wakati wa mapigano kati ya wafuasi wa rais Salva Kiir na makamu wa rais Riek Machar
Wawili hao walikubaliana kumaliza vita vya wenywe kwa wenyewe na wametoa wito wa kuwepo utulivu.

Ripoti za awali kutoka nchini Sudan Kusini zilisema kuwa takriban watu 100 waliuawa wakati wa mapigano kati ya wanajeshi hasimu katika mji mkuu Juba.

Hata hivyo idadi kamili bado haijulikani lakini wengi wa wale waliouawa wanaripotiwa kuwa wanajeshi.
Mapigano hayo yaliyoanza siku ya Alhamisi yaliendelea hadi mapema Jumamosi.

Mwandishi wa habari mjini Juba anasema kuwa wanajeshi wameweka vizuizi vya barabarani mjini humo.

Anasema kuwa masoko yamefunguliwa lakini watu wengi wamebaki nyumbani.
Sudan Kusini inaadhimisha miaka mitano ya uhuru wake.

Baada ya kifo cha Osama bin Laden mwanaye aapa kulipiza kisasi


Mwana wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden, ameapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya baba yake.
Katika ujumbe wa sauti uliochapishwa katika mitandao Hamza bin Laden ameapa kulipiza kisasi kwa Marekani kwa kumuua babake 2011 huko Pakistan.

Ujumbe huo wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama,", Hamza ambaye inaaminika kuwa alikuwa na babake makomando wa Marekani walipowavamia na kumtwaa ameapa kuendeleza kazi aliyoianza babake.

Ujumbe huo ni wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama,"
''Tutaendelea kuwasaka na kuwapiga popote pale mtakapokuwa mumejificha ati nyuma ya pazia za usalama kwa maovu munayoyaendeleza, Palestina, Afghanistan, Syria, Iraq, Yemen, Somalia na kote kwenye ardhi ya waislamu mnayokalia '' shirika la habari la Reuters linamnukuu.
''Na kwa wale wanaodhania kuwa tutakuwa tukilipiza kisasi mauaji ya Osma ole wenu, kwa nini sisi tutakuwa tukilinda dini ya kiislamu'' alisema Hamza.

Osama aliuawa na makomando wa marekani katika maficho yake huko Pakistan mwaka wa 2011.

Hamza ambaye kwa sasa ana umri wa kati ya miaka ishirini hivi alikuwa na babake kabla ya mashambulizi ya kigaidi ya mwaka wa 9/2001 huko Afghanistan kabla ya kukimbilia Pakistan kufuatia mashambulizi makali ya Marekani na washirika wake.

Hamza kulingana na wachanganuzi anatambulishwa na kiongozi wa kidini wa kundi hilo Ayman al-Zawahiri katika ujumbe huo unaolenga kuwavutia vijana ambao kwa sasa wamejiunga kwa wingi na kundi la Islamic state.

Sunday, 10 July 2016

Viongozi wa BAVICHA watiwa mbaroni Dodoma


Viongozi sita wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) wamekamatwa na Polisi mjini Dodoma kwa madai ya kukusudia kuikashifu Serikali.

Katika siku za karibuni, viongozi wa Bavicha wamekuwa wakitoa matamko mbalimbali ya kuwahamasisha wafuasi wake kuja mjini hapa kwa kile walichoeleza kuwa ni kuisaidia polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika Julai 23 kwa madai kuwa jeshi hilo lilishapiga marufuku mikutano ya kisiasa.

Hata hivyo, jana polisi imetoa ufafanuzi juu ya kauli yake ikisema kwamba kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara ya siasa na siyo ya ndani kama huo wa CCM..

Awali polisi waliwakamata Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Mkuu, Julius Mwita, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, George Tito, Katibu Mwenezi wa Bavicha, Edward Simbeye na Katibu Bavicha Wilaya ya Temeke, Hilda Newton na baadaye Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema, Joseph Kasambala aliyekamatwa baada ya kwenda kituo cha polisi kwa lengo la kuwawekea dhamana wenzake.

Wàziri Simbachawene awatahadharisha viongozi wa Umma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amesema sheria haziwaruhusu viongozi wa umma kuwa na kampuni binafsi zinazofanya kazi ndani ya manispaa wanazoongoza.

Waziri Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Kibwake (CCM), amesema mkurugenzi atakayebainika kutoa zabuni kwa kampuni yake binafsi wakati ni kiongozi wa umma, atachukuliwa hatua za kisheria.

Ametoa kauli hiyo juzi wakati akipokea vifaa vya kisasa likiwamo trekta na mitambo maalumu kwa ajili ya Mradi wa Uboreshaji Miji Kimkakati (TSCP), kutoka kwa Mratibu wa mradi, Davis Shemangali.

“Sidhani kama wapo wenye tabia hii. Kama wapo waache mara moja kujihusisha na mchezo huu kwani tutawachukulia hatua kali,” alisema Waziri Simbachawene.

John Mnyika asema hana mpango kuhama CHADEMA


Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amekanusha taarifa zinazodai kuwa anataka kuachana na chama hicho.

 Mnyika amesema hayo jana alipopigiwa simu ili azungumzie taarifa hizo. Mbunge huyo wa Kibamba amesisitiza kwamba huo ni uzushi.

 “Hakuna kitu kama hicho na wala sina mpango wa kuhama,” alisema.

Habari za kujiuzulu kwa Mnyika zilianza kusambaa katika vyombo vya habari kwa mara ya kwanza mwaka 2013 baada ya aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kufukuzwa uanachama.

Uvumi ulienea kwenye mitando kwamba amejivua nyadhifa zake zote na kwamba ameshakabidhi barua yake kwa katibu mkuu wakati huo, Dk Willibrod Slaa.

Julius Mtatiro anena kuhusu viongozi wa Siasa za Tanzania


Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amesema siasa za Tanzania zinakokwenda zinahitaji viongozi wapya, damu tofauti na wanaoweza kutazama mambo kisasa zaidi na kwa mahitaji ya kizazi cha sasa.

Mtatiro amesema jana kuwa  hatarajii kugombea uenyekiti katika chama hicho wala haungi mkono kurejea kwa Profesa Ibrahim Lipumba.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Mtatiro amesema kwa kipindi kirefu kumekuwa na msukumo mkubwa kutoka kwa viongozi wa chama ngazi za wilaya, wajumbe wa mkutano mkuu, wabunge, madiwani, wanachama, wafuasi na wapenzi wa kada mbalimbali kumtaka ashiriki kinyang’anyiro hicho.

Jana Mwananchi lilikwenda nyumbani kwa Profesa Lipumba ili kujua msimamo wake ndani ya CUF na kuelezwa kuwa amepumzika anajisikia vibaya.

Al-Shabaab walitikisa Jeshi la Polisi Kenya


Jeshi Polisi nchini Kenya hapo jana Jumamosi lilisema kwamba zaidi ya wapiganaji 100 wa dola la Kiislamu walivamia kituo cha polisi Kaskazini-Mashariki mwa Kenya na kujeruhi afisa mmoja na kuondoka na silaha na risasi.

Shambulizi hilo katika kituo cha polisi cha Diff katika wilaya ya Wajir, karibu na mpaka wa Somalia, lilitokea majira ya saa nne usiku siku ya Ijumaa na linadaiwa kufanywa na wapiganaji wa Al Shabaab, kutoka Somalia.

Mkuu wa polisi Joseph Boinnet amethibitisha kutokea kwa shambulio hilo na kusema kuwa maafisa waliweka upinzani mkali na kuwafukuzia mbali licha ya wapiganaji hao kuwa zaidi ya 100 wakiwa katika malori matatu na wakiwa na silaha nzito.

Kituo cha polisi cha Diff kilikumbwa na shambulio kama hili mwezi Aprili mwaka huu wakati maafisa watatu walipojeruhiwa na gari la polisi kuibiwa ambapo viongozi walisema wapiganaji karibu 100 wa Al Shabaab walishiriki pia katika uvamizi huo.

Saturday, 9 July 2016

Korea Kaskazini yarusha kombora la masafa marefu


Korea Kaskazini kwa mara nyingine imetekeleza jaribio la kombora lake la  masafa marefu kuelekea baharini.

Hili ndilo jaribio la hivi karibuni kutekelezwa na jeshi nchini humo kinyume na wito wa Umoja wa Mataifa pamoja na mataifa jirani kama Korea Kusini na Japan kuitaka kuacha majaribio hayo kwa sababu za kiusalama.

Jaribio hili limefanyika licha ya kuwepo kwa azimio la Umoja wa Mataifa kuzuia nchi hiyo ambayo inaendeleza mpango wa kutengeneza silaha za Nyuklia kwa lengo la kushambulia mataifa ya Magharibi.


Hili ni jaribio  la nne kuwahi kutekelezwa na Pyongyang tangu mwezi Januari mwaka huu wakiwa na lengo la kuwa na silaha za masafa marefu kuishambulia Marekani.

Nchi za Marekani na Korea Kusini zimekubaliana kuweka mpango wa pamoja kutega mitambo maalum kuzuia mashambulizi kama haya katika siku zijazo.

Jeshi la Polisi Nchini latoa sababu za kuzuia mikutano ya Siasa kufanyika hadharani


Jeshi la polisi nchini limeendelea kusisitiza msimamo wake wa kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa mpaka hapo hali ya usalama itakapotengemaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kamishina wa polisi operesheni na mafunzo makao makuu ya jeshi la polisi nchini Nsato Mssanzya amesema jeshi la polisi halitakubaliana na kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa ambazo  zinaweza kuchochea uvunjifu wa amani kwa jamii.

Kamishna Mssanzya amesema jeshi la polisi litaendelea kuimarisha hali ya usalama kwa wananchi wake ikiwemo kulinda usalama wa raia na mali zao huku likiwataka baadhi ya wanasiasa kufuata sheria na taratibu ambazo zimewekwa.

Mssanzya amesema jeshi la polisi limepiga marufuku maandamano pamoja na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa huku likifafanua kuwa jeshi hilo halitaingilia mikutano ya ndani inayofanywa na vyama hivyo.

Wanajeshi zaidi wauawa Sudan Kusini


Taarifa kutoka Sudan Kusini zinasema mamia ya watu, wengi wao wakiwa ni wanajeshi wameuawa katika mapambano baina ya vikosi vyenye uhasama katika mji mkuu wa Juba.
Mwandishi mmoja wa habari aliyeko mjini Juba amesema mapigano yameendelea mpaka mapema saa za asubuh ya Jumamosi.

Wanajeshi wametanda kwenye mitaa huku watu wachache wakionekana kutoka nje.
Daktari mmoja amesema mili mingi imepelekwa hospitali huku chumba cha kuhifadhia maiti kikiwa kimejaa.

Mapigano baina ya wanajeshi watiifu wa Rais Salva Kiiri dhidi ya Makamu wa rais Riek Machar yalianza tangu siku ya Alhamis.

Sudan Kusini inatimiza miaka mitano ya Uhuru na kuanzishwa kwake lakini hakuna sherehe zitakazofanywa.

Mabalozi wa Urusi wafukuzwa Marekani


Imebainika kuwa Marekani iliwafukuza maafisa wawili wa Urusi mwezi uliopita kufuatia kushambuliwa kwa mwandiplomasia wa Marekani mjini Moscow.

Afisa wa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni aliseme kuwa shambulizi hilo ambalo lilifanywa na mlinzi raia wa Urusi nje ya ubalozi wa Marekani, halikusababishwa na uchokozi.

Urusi inasema kwa mwanadiplomasia huyo alikuwa amemgonga mlinzi huyo usoni.

Marekani inailaumu Urusi kwa kuwadhulumu wanadiplomasia wake na familia zao.

Baba akesha akilinda wanawe walemavu wa ngozi


Ni mwendo wa saa nne toka jiji la Kampala nchini Uganda hadi kuyafikia makazi ya bwana Mwanje na wake zake wawili Lynda na Florence. Ni katika makazi haya bwana Mwanje ndipo anaishi na watoto wake nane wanaokadiriwa kuwa na miaka mitano hadi kumi na tatu huku watano kati yao wakiwa na ulemavu wa ngozi.

Na watoto wote watano wenye ulemavu wa ngozi amezaa na mkewe mkubwa Florence, wataalam wanaeleza kuwa ulemavu wa ngozi unatokana na upungufu wa madini ya melanin yanayohusika kuweka rangi ya ngozi, macho na nywele.

” Mara ya kwanza kupata mtoto mwenye matatizo ya ulemavu wa ngozi niliogopa sana, sikujua nini nitafanya, mwishowe niliamua kumpenda, nilimpenda zaidi” alisema bwana Mwanje.

Katika familia nyingi kumpata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ni tatizo, wengi wao huwaficha ndani kwa kuogopwa kuchekwa na majirani, hii inatokana na imani potofu inayoenezwa dhidi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi.

Kuna baadhi ya wanaume ambao huwatelekeza wake zao baada ya kuzaliwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi” kuna mambo mengi yasiyo ya kweli katika jamii yangu kuhusiana na wanangu watano kuwa walemavu wa ngozi, wanasema nilimcheka mtu mwenye ulemavu wa ngozi nilipokuwa kijana na akanipa laana na ndiyo sababu ya wanangu kuwa na ulemavu wa ngozi” alisema Florence mke mkubwa wa bwana Mwanje.

Kumekuwa na imani potofu kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi katika nchi zote za Afrika Mashariki, wapo wanaoamini miili ya watu wenye ulemavu ina nguvu ya kutajirisha watu maskini na kuwa matajiri wakubwa. Pia wapo wanaoamini wao ni mizimu ya kweli na siyo binadamu.

Katika nchi ya Tanzania na Malawi kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kutekwa na baadaye kuuwawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na baadhi wakikatwa viungo vyao wa mapanga wangali wazima, kifupi watu wenye ulemavu wanaishi kwa hofu kubwa kulingana na imani hizo kandamizi na potofu.

Nchini Uganda hali tofauti na nchini Tanzania na Malawi lakini ubaguzi wa wazi wa watu wenye ulemavu nchini Uganda ni jambo la kawaida. Katika shule nyingi wanafunzi wanagoma kukaa na watu wenye ulemavu wa ngozi kwenye dawati moja.

” Nilitaka wanangu wapate elimu bora, nikaamua kuwapeleka shule bora lakini tatizo shule iko mbali na makazi yangu, hivyo nilihofia wanangu wanaweza kutekwa. Kwasasa wanasoma shule ya kawaida iliyo jirani na makazi yangu” alisema bwana Mwanje.

“ Jambo lililowahi kunitia hofu zaidi, siku moja mwanagu Robert na wenzake walikuwa wakicheza jirani na shamba langu la mpunga. Mpaka jua linazama walikuwa bado porini wakicheza ghafla walimwona mtu kajificha na akaanza kuwafukuza hali iliyosababisha kila mmoja akimbilie uelekeo wake.

Robert alikimbilia uelekeo wake na wenzake uelekeo mmoja, kutokana na kelele za watoto yule mtu naye alikimbia na mpaka leo hatutajua alikuwa nani na lengo lake lilikuwa nini.” Alisema bwana Mwanje huku akionesha hali ya huzuni na wasiwasi.

“Tangu tukio hilo litoke natumia muda mwingi kukaa jirani na watoto wangu kuhakikisha usalama wao. ”
“ kuna muda napatwa na machungu watoto wangu wanaponiuliza kwanini wako tofauti na sisi, nawajibu kuwa hakuna kitu kibaya, wote tupo sawa ndani ya miili yetu.”

Waziri Mkuu wa India kufanya ziara nchini


Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi anawasili leo nchini kwa ajili ya ziara ya kitaifa ya siku mbili kwa lengo la kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema Modi atatumia fursa hiyo kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya nchi hizi mbili pamoja na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi.

Alisema Modi atakutana na Rais John Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo. Pia kuweka saini kwenye mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya sekta za viwanda, maji, elimu, sayansi na teknolojia na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.

Dk Mahiga alisema Modi pia atazungumza na jumuiya ya wafanyabiashara wakubwa wa India ambao baadhi yao wameshaonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa viwanda vya kutengeneza chuma, saruji, dawa ya binadamu na maji ya matunda.

“Natoa mwito kwa wafanyabiashara mbalimbali hapa nchini watumie fursa hii kushiriki ili waweze kukutana na wenzao, Kongamano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi,” alisema.

Jerry Muro anusurika ajalini


Muda mchache baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kumfungia mwaka mmoja Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro, bahati mbaya kapata balaa jingine.

Kwa mujibu wa salehjembe. blogspot, Muro amekumbana na ajali ya gari akiwa njiani kutoka Machame kijijini kwenda Machame mjini ambako yuko mapumzikoni.

Gari alilokuwa akiendesha liliteleza na kwenda kugonga kwenye karavati na tairi kupasuka.

“Hakika nimenusurika, unajua huku Machame ni milima. Halafu sasa kuna utelezi kutokana na mvua ingawa si kubwa, sasa wakati nateremka, gari likateleza na kwenda kugonga lile karavati,” alisema Muro.

“Lakini namshukuru Mungu, nimepona. Nilipata shida kupiga jeki kwenye tope mwisho nimefanikiwa na baada ya hapo nitaanza safari ya kwenda Dar es Salaam.”

Muro amefungiwa bila ya kupata nafasi ya kujitetea kwa kuwa wakati barua ya mwito kwenda TFF kwa ajili ya kusikilizwa inapelekwa, yeye alikuwa Machame mapumzikoni kwa ajili ya sikukuu.

Korea Kaskazini yawatishia amani Korea Kusini na Marekani


Marekani na Korea Kusini zimekubaliana kuweka mfumo wenye utata wa ulinzi dhidi ya makombora, kama njia ya kukakabiliana na vitisho vinayoendelea kutoka kwa Korea kaskazini.

Mfumo huo wa ulinzi unaowekwa katika maeneo yenye milima mirefu kudhibiti mashambulizi ya makombora utawekwa kujibu vitisho tisho kutoka Pyongyang, ilieleza taarifa. Haijabainika wazi ni wapi mtambo huo utawekwa na hatimae ni nani ataudhibiti.

Namna mfumo wa kukabiliana na Makombora (THAAD) unavyofanya kazi
Uchina, ambayo imekuwa ikipinga mara kwa mara mpango huo, imepinga mfumo huo tena kupitia wajumbe wa korea Kusini na Marekani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uchina amesema kuwa mfumo wa THAAD utadhuru amani na utulivu katika kanda hiyo, licha ya uwezo wake wa kugundua na kulipua makombora ya Korea Kaskazini.

"Uchina inaelezea kutoridhishwa kwake na kupinga vikali hili'', ilisema katika taarifa kupitia mtandao wake.

UN yawatia hatiani Wanajeshi wa Burundi kwa ubakaji


Umoja wa Mataifa unasema, wanajeshi wake wa kulinda amani waliowanyanyansa kimapenzi wasichana wadogo katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakolinda amani ni kutoka Burundi.

Imebainika kuwa wanajeshi hao ndio waliwanyanyasa wascihana wawili, mmoja mwenye umri wa miaka 12 na mwingine mwenye umri wa miaka 18 mwezi Mei mwaka huu.

Msemaji wa UN Stephane Dujarric amesema uchunguzi binafasi unafanyika na huenda wanajeshi hao wakajarudishwa nyumbani.


Upande wa jeshi la Burundi hawajazungumza lolote kuhusu vitendo hivyo viovu wanavyoshutumiwa baadhi ya askari wa Burundi waliojiunga katika kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Askari wa kulinda amnai wa Umoja wa Mataifa wamekua wakinyooshewa kidole kwa visa kama hivyo katika nchi mbalimbali wanakolinda amnai.

Hivi karibuni Baadhi ya askari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walishtumiwa kujihusisha na vitendo hivyo viovu, na baadaye kuchukuliwa uamuzi wa kuwarejesha nyumbani.

Ndoa za utotoni Tanzania kukoma


Mahakama kuu nchini Tanzania leo imeidhinisha umri halisi wa kuolewa kwa mtoto wa kike kuwa miaka 18. Wasichana wenye umri wa miaka 14 huolewa kwa ridhaa ya wazazi wao.

Mahakama kuu imetoa muda wa mwaka mmoja kuhakikisha kuwa Serikali inasahihisha sheria ya mwaka 1971 kifungu cha 13 kinachoruhusu Mtoto wa kike kuozwa akiwa na umri miaka 14
Wasichana wanaoolewa katika umri huu mara nyingi wanakabiliwa na unyanyasaji wa majumbani sambamba na kutengwa na jamii huku wakipewa nafasi ndogo kwa ajili ya elimu na ajira.

Huu ni ushindi mkubwa kwa wanaharakati wa Tanzania katika kupigania haki za watoto na sasa itakuwa rahisi kuwaokoa wasichana wanaoathirika na utamaduni wa kuozeshwa wakiwa wadogo.

Uamuzi huu umekuja wakati Bunge kupitisha sheria ya kifungo cha miaka 30 ama faini ya dola 2500 kwa mwanaume atayebainika kumuoa ama kumpa mimba mwanafunzi.Hata hivyo sheria hii inawatenga maelfu ya wasichana ambao si wanafunzi.

Friday, 8 July 2016

Amani ya Burundi: Mazungumzo yasogezwa mbele


Mazungumzo ya amani kuhusu nchi ya Burundi, yaliyozinduliwa mwezi May mwaka huu baada ya miezi kadhaa ya mvutano, yameahirishwa kutoka siku ya Jumamosi hadi Jumanne ya wiki ijayo nchini Tanzania, imesema taarifa ya mratibu wa mazungumzo na wanadiplomasia wanaoshiriki mazungumzo.

"Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu, mazungumzo kuhusu mzozo wa Burundi, yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kuanzia Julai 9 hadi 12 jijini Arusha, yameahirishwa, amesema Makocha Tembele, msaidizi wa rais Bejamin Mkapa anayeratibu mazungumzo hayo.

Wanasiasa kadhaa wa Burundi wamethibitisha kupokea ujumbe ukiwataarifu kuwa sasa mazungumzo yatafanyika Jumanne ya wiki ijayo", taarifa ambayo imethibitishw apia na mwanadiplomasia ya Umoja wa Ulaya ambaye hakupenda jina lake kuwekwa wazi.

Licha ya shinikizo na vitisho vya kuwekewa vikwazo kutoka Juumuiya ya kimataifa, utawala nchini Burundi umekataa katakata kukaa meza moja na viongozi wakuu wa upinzani, ikiwatuhumu wapinazani hao kushiriki njama za kutaka kuipindua Serikali mwezi Mei mwaka jana.

Nchi ya Burundi ilitumbukia kwenye machafuko ya kisiasa, wakati rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu mwezi April mwaka jana, kabla ya kuchaguliwa tena mwezi Julai.

Mpaka sasa machafuko ya Burundi, yameripotiwa kusababisha vifo vya watu 500 na tume ya umoja wa Mataifa inayohusika na wakimbizi UNHCR, inakadiria kuwa watu zaidi ya laki 3 na elfu 70 raia wa Burundi wamekimbia nchi yao.

Wamarekani weusi wauawa kikatili na Polisi weupe


Rais Obama wa Marekani amesema mauaji ya kikatili ya watu wawili weusi raia wa Marekani yaliyofanywa na polisi kama mengine yaliyotokea tukio jipya ni jambo kila Mmarekani anapaswa kulichukia.

Rais Obama amesema ubaguzi umesababisha imani ya jamii kupungua dhidi ya polisi.

Katika picha video ya hivi karibuni inayomwesha marehemu Philando Castile akivuja damu ndani ya gari huku akinyooshewa bunduki na polisi liliwekwa na rafiki yake wa kike kwenye mitandao ya kijamii.

Gavana wa Jimbo la Minisota Mark Dayton amesema hafikirii polisi waliompiga risasi na kumuua dereva huyo ambaye baadaye walimvuta na kuvunja taa za mbele kama dereva huyo angekuwa mzungu.

Amesema atahakikisha uchanguzi wa tukio hilo ufanyika.Ninaaahidi nitafanya kila liwezekanavyo utawala pia utafanya kila linalowezekana ndani ya mamlaka yetu kukamilisha uchunguzi na kama ulivyosema mbele ya Robert Heron, haki lazima iheshimiwe.Haki lazima iheshimiwe Minesota. Haki lazima iheshimiwe.

Wakati wa maandamano hayo rafiki wa kike wa marehemu alielezwa kwa uchungu kile kilichotokea kwa rafiki yake aliyeuaa.

"Haikuwa risasi moja, hazikuwa mbili,hazikuwa tatu, hazikuwa nne zilikuwa risasi tano. Bila sababu. Inawezekanaje mtu kuweka mikono yake angani na kutoa kitambulisho kwa wakati mmoja wakati wanapokueleza kwamba alikuwa na silaha.

"Alipata wakati mgumu. Ilikuwa kwenye mfuko wa bastola kwenye suruali wakati walipomvuta kutoka kwenye gari wakati waleti yake ilipokuwa katika mfuko wa nyuma. Hawakutoa muda kwenye tukio hilo. Hawakuhakikisha anapumua.

"Harakaharaka walimtoa mwenzao pembeni wakamfariji. Mahali alipoanza kupiga kelele na kulia Ooh Mungu wangu siamini hili."

Bomoabomoa kuikumba Dodoma


Nyumba 236 zitabomolewa katika Kata ya Makole, Wilaya ya Dodoma mkoani hapa ili kupisha ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma.

Akizungumza ofisini kwake jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amesema tathmini ilishafanyika kwenye maeneo hayo.

Amewahakikisha wakazi wote watakao takiwa kuhama, hakuna atakaye ondolewa bila kulipwa stahili zake zote za kisheria.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), Edward Mpanda Amesema mamlaka yake imeshatenga eneo la Ilazo Extension lenye viwanja vilivyopimwa kwa ajili ya wakazi hao.

“Tumepima viwanja 300 katika eneo hilo ambalo litajengwa pia miundombinu mingine,” amesema.

Wastani wa watu 9 hufa kila siku katika ajali barabarani


Imeelezwa kuwa wastani wa Watanzania tisa hufariki dunia kila siku kutokana na ajali za barabarani.

Idadi hiyo inatokana na vifo 1,286 vilivyochagiwa na ajali 4,177, zilizotokea kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga amesema jana kuwa ajali hizo zinajumuisha bodaboda, magari na vyombo vingine vya usafiri.

Mpinga amezitaja sababu za kutokea kwa ajali hizo kuwa ni makosa ya binadamu kwa asilimia 76, makosa yanayotokana na ubovu wa vyombo vya usafiri (16) na makosa yanayotokana na ubovu wa barabara (nane).

Lowassa ashiriki Mazishi ya Beatrice Shelukindo


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amekuwa miongoni mwa mamia ya waombolezaji walioshiriki maziko ya mbunge wa zamani, Beatrice Shelukindo (58) yaliyofanyika nyumbani kwa wazazi wake katika kata ya Olorien Jijini Arusha jana.

Viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo yaliyotanguliwa na ibada ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Jaji Mkuu mstaafu, Agustino Ramadhani, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.

Pia maziko hayo yalihudhuriwa na wabunge na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mkoa wa Tanga na Arusha, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro na viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali. Ibada ilifanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro ambako Askofu mstaafu, Simon Makundi, alisema Beatrice hakuwa fisadi na alitoa mchango mkubwa kwa familia, dini, taifa na Afrika Mashariki.

“Jiulize wewe una mchango gani hata katika familia yako, dini yako, taifa hili na hata kwa Afrika Mashariki?” Alihoji Makundi.

Aliwataka mamia ya waombolezaji wakipewa nafasi, heshima na vyeo serikalini au katika kampuni yo yote kuitunza heshima hiyo kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa na hofu ya Mungu.

Beatrice aliyezaliwa mwaka 1958 amefariki akiwa na umri wa miaka 58, jambo ambalo askofu mstaafu alisema hiyo ni neema ya Mungu.

Alisisitiza kuwa Beatrice alifanya kazi za utumishi serikalini na ubunge kwa uadilifu mkubwa na kupata heshima na serikali, dini na jamii na ndiyo maana aliweza kuhitimisha heshima hiyo hadi mwisho. Askofu Makundi alisema alipata bahati ya kuzungumza naye kabla ya mauti.

Jerry Muro afungiwa michezo


MKUU wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka na kulipa faini .

Kwa mujibu wa televisheni ya Channel 10, Muro alifungiwa baada ya kikao kilichofanyika jana.

Taarifa nyingine ambazo hazikuthibitishwa zilisema kuwa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana ilichukua hatua hiyo baada ya kikao kirefu.

Habari hizo zilizopatikana jana usiku zilisema Muro alifungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka baada ya kupatikana na hatia ya kuipinga na kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari. Kikao cha Kamati ya Maadili ya TFF, kilikaa jana bila ya Muro kuwepo kwa kuwa wakati mwaliko unatoka alikuwa nje ya Dar es Salaam.

Awali, Muro alisema alikuwa mapumzikoni Machame mkoani Kilimanjaro.

Hatahivyo, msemaji wa TFF, Alfred Lucas alisema jana saa 1:50 usiku kuwa kikao hicho kilikuwa kikiendelea na alishangaa taarifa hizo zilipatikana wapi.

“Na mimi kuna watu wamenipigia wamesema kuna taarifa katika mitandao inasema Jerry kafungiwa, sijui wamezitoa wapi kwani na mimi niko hapa nje na kikao kinaendelea, lakini taarifa kamili kesho saa nne asubuhi”, alisema Lucas.

Thursday, 7 July 2016

Makatibu Tawala wa Wilaya wateule wanahitaji mafunzo


Baadhi ya makada wa CCM walioshindwa kwenye  mbio za urais na ubunge kuteuliwa kushika nafasi za Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), wamezua mjadala kwa kile kilichoelezwa kuwa nafasi hizo ni za kiutendaji hivyo zinahitaji wasomi na wenye uzoefu serikalini.

Makada hao ni miongoni mwa watu 40 wapya kati ya 134 waliotangazwa juzi na Ofisi ya Rais-Utumishi kushika nafasi hizo kwenye uongozi wa wilaya.

Miongoni mwa makada waliotangazwa kuteuliwa kuwa Ma-DAS ni Amos Siyamtemi, ambaye aligombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, lakini akaishia ndani ya mchakato wa CCM, Kasilda Mgeni, mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Star TV ambaye alikuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM na aligombea ubunge wa viti maalumu mwaka 2010 bila ya mafanikio.

Wengine ni Mtella Mwampambwa, Aboubakar Assenga, Jasinta Mboneko, Gift Msuya, Hashim Mkomba, Edward Mpogolo na Adam Mzee, ambao wamewahi kugombea ubunge, udiwani au kushika nafasi kwenye ngazi tofauti za uongozi wa CCM.

Katibu mkuu wa Wizara ya Utumishi, Dk Laurian Ndumbaro amesema kuna theluthi moja ya wateule wanaohitaji mafunzo ya muda mfupi ili kuwaandaa kukabiliana na changamoto za majukumu mapya waliyokabidhiwa.

Amesema wengi wana elimu ya kutosha na wanachohitaji ni kuzifahamu sheria na taratibu za utekelezaji wa majukumu yao.

Mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana amesema: “Kama tungetaka kutenda haki, nafasi hizo zingetangazwa.”

Amesema uofisa tawala ni nafasi kubwa katika uendeshaji wa wilaya na Serikali kwa ujumla na hivyo unahitaji mtu aliye ndani serikalini na mwenye uzoefu.

Kaswende na Kisonono tishio Uingereza


Magonjwa ya zinaa yameanza kuenea kwa kasi sana nchini Uingereza.
Utafiti umebaini kuwa Maradhi ya Kaswende na Kisonono yamenea kwa kasi kubwa nchini humo katika kipindi cha miaka 3.

Idadi ya visa vya maambukizi ya Kaswende vilikuwa kwa kati ya asilimia 76%, kutoka kwa visa 3001 hadi visa 5,288 kuanzia mwaka wa 2012 hadi mwaka wa 2015.

Kwa upande mwengine visa vya maambukizi ya kisonono vilikuwa kwa kasi kubwa ya asilimia 53%, kutoka visa 26,880 vya maambukizi hadi visa 41,193 .

Cha kustaajabisha ni kuwa visa hivyo vya maambukizi ya magonjwa ya zinaa vinapatikana sana miongoni mwa wanaume wanaoshiriki mapenzi na wanaume wenza.

Chlamydia ilitajwa kuwa moja ya maradhi yaliyopimwa zaidi katika wakati huo wa utafiti.
Watu walioambukizwa ugonjwa huo walikaribia nusu ya wale wote waliowahi kupimwa magonjwa ya zinaa,hii ni takriban 434,456 mwaka wa 2015.

Msaada watolewa kupambana na Homa ya manjano


Shirika la Msaada Mwekundu hapo Jumatatu lilitoa wito wa msaada wa dharura wa dola milioni 1.4 ili kukabiliana na kuenea kwa homa ya manjano nchini Angola ukiwa mlipuko mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 30.

Kufikia sasa, zaidi kidogo ya dola milioni 15 za homa ya manjano zimepelekwa Angola pamoja na nchi jirani ya DRC lakini uhaba wa fedha na ugumu wa kutengeneza chanjo vimepelekea upungufu huo.

Homa ya manjano maarufu 'Yellow Fever' ni ugonjwa unaoenezwa na mbu. Mbu wanaoeneza homa ya manjano ndio wanaoeneza Zika, homa ya Dengue pamoja na Chikungunya.

Homa ya manjano mara nyingi haijioneshi dalili na wengi walioambukizwa dalili hazijitokezi, hata hivyo takriban asilimia 15 ya wagonjwa huathiriwa vibaya huku aslimia 50 wakifa kutokana na maradhi hayo wanapokosa matibabu.

Makosa ya barabarani yaongezeka Mkoani Mwanza


Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabara kimekamata makosa 11, 088 kwa kipindi cha Juni kutoka makosa 10,389 yaliyotokea Mei.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema jana kuwa  kuongezeka kwa idadi ya makosa hayo kumetokana na umakini wa askari wa usalama barabarani katika kudhibiti wavunjaji sheria.

Amesema kutokana na makosa hayo,  wamekusanya zaidi ya Sh329.7 milioni zikiwa ni tozo za faini.

“Hata hivyo, makosa makubwa ya uhalifu yameongezeka Juni kufikia 232, ikilinganishwa na 197 ya Mei,” amesema Msangi.

Wednesday, 6 July 2016

JPM asema pesa za bure zimeisha


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema kwamba watu waliokuwa wanapata fedha za bure bure wameanza kusema kwamba fedha zimeisha.

Rais Dkt. Magufuli ameyasema hayo alipokuwa akitoa hotuba wakati wa kushiriki hafla ya Baraza la Eid el Fitri iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.

''Watu waliokuwa wanapata pesa za bure bure wameanza kusema pesa zimeisha, hauwezi kupata pesa kama haufanyi kazi '' -Amesema Dkt. Magufuli.

Rais amesisitiza kwamba katika hatua za serikali yake kuleta heshima serikalini ni lazima watu wachache waumie kwa manufaa ya wengi.

''Nchi hii imejaa madini ya kila aina na juzi imegundulika helium na bado rasilimali nyingine lakini cha kushangaza bado tupo masikini lazima tushughulikie hili na katika kuleta ufanisi lazima wachache waumie ili wengi ambao walikuwa wanadhulumiwa wanufaike na taifa lao'' Amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais amewataka waumini wote wa dini ya kiislamu kusherekea kwa amani na kudumisha amani ya nchi kwa kufuata yale yote ambayo viongozi wa dini wamefundisha muda wote wa mfungo.

Akimkaribisha mgeni rasmi Mufti wa Tanzania Abubakar Zuberi amewataka waislamu kuwa na upendo na kudumisha amani kwa maslahi ya taifa letu.

Zaidi ya watu 100 wanusurika katika ajali ya moto mkoani Iringa


Zaidi ya watu 100 wamenusurika kifo baada ya moto kuteketeza kituo cha kulelea watoto cha Faraja kilichopo Mgongo kata ya Nduli manispaa ya Iringa na kusababisha zaidi ya watoto 70 ambao ni wanafunzia wa shule mbalimbali za kituo hicho cha kulelea watoto wa mazingira hatarishi kukosa mahali pa kulala.

Moto huo uliozuka majira ya saa kumi na moja jioni na kudumu hadi saa 11 alfajiri ya leo umeteketeza kabisa jengo la mabweni ya wanafunzi hao huku wenyewe wakiwa wametoka kwaajili ya matembezi hali inayoonekana kama muujiza.

Kufuatia hali hiyo uongozi wa mkoa wa Iringa umefika kujionea uharibifu huo na kutoa misaada mbalimbali yakiwemo magodoro na mabranketi kwaajili ya kusaidia maisha ya watoto wa kituo hicho ambao wameunguliwa na vifaa vyao yakiwemo madaftari pamoja na nguo zao.

Veronica nziku anatoa shukrani kwa mkuu wa mkoa na msafara wake kwa niaba ya wenzake wa kituo hicho ambapo serikali ya mkoa licha ya kukabidhi msaada huo imewaomba watu mbalimbali kujitolea kusaidia kituo hicho kwa lengo la kurejesha maisha ya watoto hao kama yalivyokuwa zamani.

Raia waunda vikosi kupambana na Boko Haram


Majuma mawili yaliyopita, Umar Mohammed alikamata mshukiwa kutoka kundi la Boko Haram aliekuwa akijaribu kuingia kwenye mji wa kaskazini mashariki wa Maiduguri akiwa amebeba bomu.

Mohammed ni mmoja kutoka kikosi maalum cha kiraiya maarufu 'Civilian Joint Task Force' (JTF) ambacho kimeidhinishwa na serikali ya jimbo la Borno tangu mwaka wa 2013 kwa lengo la kukabiliana na Boko Haram.

Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi kaskazini mashariki mwa Nigeria na pia kwenye eneo la ziwa Chad kwa miaka saba huku likiuwa zaidi ya watu 20,000 na kusababisha wengine milioni 2.7 kukosa makao.

Operesheni ya kijeshi kwenye eneo hilo imemaliza nguvu za Boko Haram na hata kuliondoa kwenye maeneo ya mjini.

Makundi kama vile 'JTF' pamoja na mengine takriban dazeni moja kwenye eneo hilo pia yamesaidia pakubwa katika kuangamiza kundi hilo.

Migomo yaathiri shughuli za kitaifa Zimbabwe


Nchini Zimbabwe wafanyikazi wa serikali wamesusia kwenda kazini katika kile wanaharakati wametaja kuwa ni kususiwa kwa shughuli zote za kitaifa.

Maandamano hayo yanatokana na hali mbaya ya kiuchumi nchini humo.

Mitaa ya miji mikuu nchini Zimbabwe imetulia tulii, maduka na masoko yamefungwa.

Kampeni ya kuwataka raia wa taifa hilo kusalia makwao ilianza kwenye mitandao ya kijamii, kutokana na ufisadi unaoendelea , pamoja na usimamizi mbaya wa uchumi wa taifa hilo.

Mitandao ya kijamii ilizimwa kwa kipindi cha saa nne.

Maandamano yalianza wiki iliyopita karibu na mpaka wa taifa hilo na Afrika Kusini, baada ya sheria ya kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa nyingi kutoka Afrika Kusini kuanza kutekelezwa.

Maandamano ya leo ndio makubwa zaidi kuwai kufanyika nchini Zimbabwe dhidi ya serikali.

Maandamano hayo yanafuatia mgomo wa madaktari na wauguzi.

Aidha maandamano ya madereva wa teksi na wafanyibiashara dhidi ya vizuizi vya polisi ambavyo wanadai huwa ni vituo vya kudai hongo.

Visa vingi vya ukiukaji wa haki za kibinadamu vinavyodaiwa kutekelezwa na polisi dhidi ya umma vilichapishwa katika mitandao ya kijamii.

Kwa sasa mgogoro wa kiuchumi unashuhudiwa nchini humo, na kupelekea uhaba mkubwa wa pesa.

Wafanyikazi wa umma wamekataa kurejea kazini pasi na kulipwa malimbikizi ya mishahara yao.

Kampeini hiyo inadaiwa kuanzishwa na kasisis mmoja Ivan Mawareery ambaye aliwataka Wazimbabwe wavalie mavazi yenye rangi za bendera ya taifa kama njia yao ya kulalamikia kudhulumiwa kwa haki zao za kimsingi.

Lionel Messi ahukumiwa kifungo jela


Mchezaji nyota wa Argentina na Barcelona Lionel Messi amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela baada ya kupatikana na makosa ya kutumia ulaghai wakati wa ulipaji ushuru, vyombo vya habari nchini Uhispania vinaripoti.

Babake, Jorge Messi, pia amehukumiwa kufungwa jela kwa kuilaghai Uhispania €4.1m (£3.2m; $4.6m) kati ya 2007 na 2009.

Wakati wa kesi, waendesha mashtaka walisema maeneo salama yenye kinga dhidi ya ushuru Belize na Uruguay yaliyumiwa kuficha mapato kutokana na uuzaji wa haki za picha za mchezaji huyo.

Lakini Messi amesema hakufahamu lolote kuhusu masuala yake ya kifedha.

Wawili hao hata hivyo hawatarajiwi kufungwa jela.
Chini ya mfumo wa haki nchini Uhispania, mtu anaweza kutumikia kifungo chochote kilicho chini ya miaka miwili nje ya gereza.

Messi na baba yake pia wanaweza kukata rufaa katika Mahakama ya Juu nchini humo.

Raia wa Nigeria adakwa na dawa za kulevya JNIA

Jeshi la Polisi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam limemnasa raia wa Nigeria, aliyetambulika kwa jina la Dede Eke (45) baada ya kudaiwa kukutwa na madawa ya kulevya aina ya heroine kilo tano uwanjani hapo.

Akizungumza na Uwazi, ofisini kwake Ijumaa iliyopita, Kamanda waPolisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, ACP Martin Otieno alithibitisha kukamatwa kwa Mnigeria huyo siku hiyo akasema kulitokana na kuimarisha ulinzi uwanjani hapo na kufungwa mashine za kisasa za uchunguzi.

“Ni kweli tumemkamata Mnigeria Bede Eke katika Uwanja wa Ndege Dar na kilo tano za dawa za kulevya aina ya heroine wakati akitaka kuondoka kwenda Lagos, Nigeria kwa ndege.

Dawa hizo zimepelekwakwa mkemia mkuu kwa uchunguzi na kujua thamani yake.

“Dede alikuwa ameficha madawa hayo katika begi dogo jeusi ambalo alishonea madawa ndani kisha akalitumbukiza ndani ya begi kubwa, amenishangaza, alidhani hatupo makini” alisema kamanda huyo na kuongeza kuwa "polisi wanamhoji mtuhumiwa huyo kujua alikozipata na upelelezi ukikamilika tutamfikisha mahakamani."

Tuesday, 5 July 2016

Mabasi ya City Boy yafungiwa kufanya safari


Siku moja baada ya kutokea ajali ya mabasi iliyosababisha vifo vya watu 30 na majeruhi kadhaa, Kampuni ya mabasi ya City Boy imefungiwa kufanya biashara hiyo kwa muda usiojulikana.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Maweni, Manyoni, mkoani Singida baada ya mabasi ya kampuni hiyo, moja likitokea Dar es Salaam na lingine likitokea Kahama kuelekea Dar es Salaam kugongana.

Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), David Mziray amesema leo kuwa kampuni hiyo ina miliki mabasi 12 na yote yamefungiwa kufanya safari yoyote kuanzia leo.

“Mabasi hayo yamefungiwa kuanzia leo kwa muda usiojulikana, ukaguzi wa mabasi yao utaanza kufanyika kupitia jeshi la polisi,” amesema Mziray.

Mkimbizi Jela miaka 30 kwa ubakaji


Mahakama ya Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma, imemhukumu kwenda jela miaka 30 mkimbizi kutoka Kongo, Charles Godfrey (22) anayeishi katika kambi ya wakimbizi ya Nduta kwa kosa la kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 15.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Peter Makala alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 4, mwaka huu, Saa 5:00 usiku.

Aliendelea kudai kuwa baada ya mshitakiwa kutekeleza azma yake alitaka kukimbia, lakini raia wema walimkamata na kumfikisha polisi.

Baada ya kusomewa mashtaka, Hakimu wa Mahakama hiyo, Erick Marleye alimtaka mshtakiwa ajitetee, aliiomba mahakama imwonee huruma kwa kile alichodai kuwa ana watoto wadogo wanaomtegemea.

Hata hivyo, Mahakama baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo bila kuacha shaka, ilimhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 gerezani.

Hakimu Maeleye alisema adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia za kunyanyasa watoto kingono.

Jacob Zuma kufanya ziara Ufaransa Julai 12.


Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma atafanya ziara ya kikazi nchini Ufaransa wiki ijayo. Rais zuma atakuwa nchini Ufaransa kuanzia Julai 12 kwa minajili ya kushiriki hasa katika maadhimisho ya mia moja ya vita vya "Delville Wood" dhidi ya askari wa Ujerumani ambapo walishiriki zaidi ya askari 3,000 wa Afrika Kusini katika Vita Vikuu vya Dunia.

Kisha Marais wa nchi za Ufaransa na Afrika Kusini watajadili masuala ya ushirikiano na biashara.

Ufaransa bado ni mshirika muhimu katika masuala ya biashara wa Afrika Kusini, amethibitisha Waziri wa mambo ya Nje wa Afrika Kusini kabla ya ziara ya ziara hii. Mwaka jana, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka Ufaransa kwa Afrika Kusini uliikia Euro bilioni 1.5 na biashara kati ya nchi hizi mbili, zaidi ya Euro bilioni 2.

Alipoulizwa kuhusu kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya aiwapo kunaweza kubadilisha mahusiano ya Afrika Kusini na Ulaya, hasa na Ufaransa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Maite Nkoana-Mashabane amejibu kwa umakini "hatuna taarifa yoyote kuhusu kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, tumeona tu kwenye televisheni. Tunaambiwa kwamba hali hii itakuwa na athari hasi juu ya biashara yetu na nchi za ukanda mzima. Kwa sasa, hatujahisi chochote. Wala sisi si wanachama wa Umoja wa Ulaya. Tunachoweza tu kusema, ni hongera kwa demokrasia! "

Wakati wa mkutano kati ya Marais hao wawili kutafanyika mkutano kabambe kati ya viongozi wa makampuni kutoka Afrika Kusini na Ufaransa kwa kuendeleza uwekezaji na biashara. Pamoja na ukuaji wa Afrika Kusini ambao hauzidi 0.6% mwaka huu, Pretoria itaendelea kuwa na haja ya wadau wote inaoshirikiyana nao.

China yafanya mazoezi ya Kijeshi baharini


China inafanya mazoezi ya kijeshi kusini mwa bahari ya China siku chache kabla ya uamuzi muhimu wa mahakama kuhusu mzozo ulio eneo hilo la bahari.

Mazoezi hayo yanafanyika karibu na visiwa vinavyozozaniwa vya Paracel.

Mahakama ya haki mjini Hague inatarajiwa kutoa uamuzi wake wiki ijayo katika kesi iliyowasilishwa na Ufilipino.

China tayari imesema kuwa haitakubali uamuzi huo.
Gazeti moja la serikali The Global Times linasema kuwa China inastahili kujiandaa kukabiliana na Marekani.

Jose Mourinho awapa makavu Wenger na Van Gaal


Limekuwa jambo la kufurahisha kwa kocha mpya wa Manchester United, Jose Mourinho kuwa akirushiana maneno na kocha mwenzake wa Arsenal, Arsene Wenger tangu alipokuwa akiifundisha Chelsea na sasa jambo hilo limeanza kujirudia akiwa na Man United.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari, Mourinho alionekana kuzungumza maneno ambayo yalionekana wazi kumlenga Wenger pamoja na kocha aliyepita kuinoa Manchester United, Louis Van Gaal.

“Mameneja wengine wameshinda kombe miaka 10 iliyopita na wengine hawajaweza kabisa. Mara ya mwisho mimi nimeshinda kombe mwaka uliopita, kwahiyo kama nina vitu vingi vya kurekebisha basi linganisha na wengine,

“Ukweli ni kuwa hilo jambo sio muhimu kwangu, ninacheza dhidi yangu mwenyewe, nina mambo ya kuboresha kwangu sio kwa ajili ya wengine ila mimi na hiyo ndiyo kawaida yangu, siwezi kufanya kazi bila mafanikio,” alisema Mourinho.

Aidha kocha huyo alimzungumzia Giggs na kusema kuwa ” Sio wajibu wangu kuwa Giggs hayupo klabuni, kazi ambayo Ryan alikuwa akihitaji Manchester United ni kuwa meneja,

“Hilo sio wajibu wangu, wamiliki na Mr. Woodward walinitaka mimi na ni muda ambao Ryan alitaka kuwa meneja, hata mimi nilichagua kuwa kocha miaka iliyopita lakini wengi wetu tunaanza kwa kuwa makocha wasaidizi,” alisema kocha huyo.

Kuhusu nafasi ya Rooney katika kikosi chake, Mourinho alisema “Jambo moja ambalo siwezi kulibadili ni kuhusu kubadili nafasi yake ya kufunga magoli, anaweza asiwe mshambuliaji, lakini kwangu hawezi kuwa namba 6, atacheza ndani ya mita 50 kutoka goli la adui,

“Wachezaji wengi wanauwezo wa kutoa pasi lakini kazi ngumu ni kufunga magoli, anaweza kuwa namba 9 au namba 10 au namba 9.5 lakini sio namba 6 au 8,” aliongeza Mourinho.

Waziri Nchemba atoa ahadi kwa Waislamu Nchini


Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, amesema kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha taratibu, ratiba na maadhimisho muhimu ya madhehebu ya dini nchini, yanafanyika bila kuvurugwa na baadhi ya watu mwenye nia mbovu.

Mwigulu ambaye pia ni mbunge Jimbo la Iramba Magharibi, aliyasema hayo kwenye hafla ya kufuturisha baada ya viongozi na wananchi wa dhehebu la kiislamu kutoka wilaya zote za mkoa wa Singida. Futari hiyo iliandaliwa na mwenyekiti wa CCM mkoa na mbunge wa viti maalum, Martha Mlata.

Alisema madhehebu ya dini nchini yameendelea kuiwezesha Tanzania iendelee kudumisha amani na utulivu hivyo ni wajibu wa serikali kuyaimarishia ulinzi ili wananchi wake wazidi kupata mafundisho ambayo yatasaidia wananchi wenye nia mbaya wanabadilika na kuwa watu wema.

“Kutokana na mchango huo ambao pamoja na faida zake nyingi ikiwemo wananchi kujiletea maendeleo yao kwa uhuru mpana, sisi wa wizara ya mambo ya ndani, hatukubali ustawi wa madhehebu ya dini uchafuliwe kwa namna yoyote ile”,alisisitiza.

Alisisitiza zaidi, Mwigulu alisema waumini wa dini ya kiislamu wasiwe na hofu wala wasi wasi wowote, kuelekea siku kuu ya Iddi Elftiri na kwamba wataisherehekea bila usumbufu wa aina yo yote.

“Hata ndugu zetu wanaotarajia kwenda kuhiji mwaka huu, wasiwe na hofu yoyote, tutahakikisha hakuna mtu au kikundi cha watu kitakachochafua taratibu zao za kwenda kutimiza nguzo muhimu za dhehebu lao la dini,” alisema Mwigulu.

Kwa upande wake, Mlata alisema ameandaa hafla hiyo ya futari baada ya kusukumwa na imani kwamba Watanzania siku zote, niwa ni wamoja hawabaguliwi na itikadi ya kisiasa wala kwa dini zao.

“Kila Mtanzania anaheshimu imani ya dini ya mwenzake. Kitendo hiki kina mchango mkubwa sana kwenye amani na utulivu wetu, na ndio maana nchi yetu imeendelea kuwa kisiwa cha amani,” alisema mwenyekiti huyo.

Mlata ambaye ni mwimbaji mahiri nchini wa nyimbo za kwaya, pia alitoa msaada wa vitabu vipya vya quran 100 na maboksi matano ya tende.

JPM kufurahishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi


Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imevuka lengo la kukusanya kodi kwa zaidi ya asilimia 100 kwa kukusanya Tsh. Bilioni 74.098. kati ya Julai 1, 2015 hadi June 30, 2016.

Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Kodi katika Wizara hiyo, Bw. Dennis Masami wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Saba Saba.

“Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya Tsh. bilioni 70 na hadi kufikia Juni 30, 2016 kiasi cha Tsh. 74,098,902,895.20/= kimekusanywa sawa na asilimia 106 ya zaidi ya lengo,” alisema Masami.

Masami amesema kwamba ukusanyaji huu wa ufanisi umetokana na elimu iliyotolewa na Wizara kwa walipa kodi na kuwaandikia hati za madai wadaiwa sugu ambao walikuwa hawalipi kodi kwa wakati.

Kwa mujibu wa Masami mashauri 5000 yamefunguliwa ambapo Wizara imeshinda mashauri 2000 na imepewa hati ya kukamata mali ambayo ni deni la zaidi ya Tsh. bilioni 6 kati ya hizo zaidi ya bilioni 3 zimelipwa na wadeni wengine wanaendelea kulipa.

Aidha, amewataka wamiliki wote wa ardhi kulipa kodi kwa wakati na kwamba kodi ya ardhi hulipwa kila ifikapo Julai 1 ya kila mwaka katika Halmashauri, Manispaa na Makao Makuu ya Wizara na kuongeza kuwa kulipa kodi ni wajibu wa kila mmiliki kwa mujibu wa kifungu cha 33(1) cha sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999.

“Kwa watakao kaidi kutimiza masharti hayo watachukuliwa hatua za kisheria chini ya fungu la 50 sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999; pamoja na kuwafikisha mahakamani, kukamata mali ili kufidia deni au kufuta milki,” alisema Masami.

Ni wazi kuwa kutokana na makusanyo hayo, Wizara ya Ardhi itakuwa ni moja ya wizara ambayo inamfurahisha Rais Magufuli kutokana na dhamira yake ya kuhakikisha makusanyo yanakua ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo.

Mtoto wa Nduli Idd Amin Dada akosoa sherehe za Entebbe


Mwana wa aliyekuwa kiongozi wa Uganda Idi Amin Dada amepinga sherehe za maadhimisho ya miaka 40 tangu kutekelezwa kwa operesheni ya makomando wa Israel uwanja wa ndege wa Entebbe.

Makomando hao walifika kuwaokoa mateka Wayahudi waliokuwa wanazuiliwa na wanamgambo wa Palestina waliokuwa wameteka ndege ya shirika la Air France.

Bw Hussein Lumumba Amin amesema ni makosa kwa serikali ya Uganda na nchi jirani za Afrika kushiriki sherehe hizo pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bw Amin, anasema baada ya kutekelezwa kwa shambulio hilo 1976, Umoja wa Afrika ulilaani kitendo hicho.
Aidha, amesema si haki kwa babake, Idi Amin, kuoneshwa kama mhusika katika utekaji nyara wa ndege hiyo.

Anasema baba yake alikuwa anatekeleza wajibu wa upatanishi na kwamba hata aliwafaa mateka waliokuwa wanazuiliwa. Aidha, alikuwa anatetea haki za Wapalestina.

“Kama Amin angekuwa anapendelea upande mmoja wakati huo, mateka hao huenda labda wangezuiliwa gereza kuu la Luzira au afisi iliyoogopwa sana ya makachero wa serikali ambapo hawangeweza kutoroka,” Bw Lumumba anasema.

Anasema Bw Amin aliwaokoa mateka hao kwa kuhakikisha ndege hiyo, baada ya kutekwa, iliweza kutua Libya na kuongezwa mafuta kabla ya kuendelea na safari hadi Uganda.

Netanyahu: Israeli inataka uhusiano na Afrika
Kabla ya hapo, anasema ndege hiyo ilikuwa inazunguka angani bahari ya Mediterranea na haikuwa na mafuta ya kutosha kufika Uganda.

Kiongozi huyo wa zamani, alimsihi kiongozi wa Libya wakati huo, Kanali Muamar Gaddafi, aruhusu ndege hiyo kuongezwa mafuta.

Bw Lumumba anasema Idi Amin Dada alihusika kama mpatanishi
Wakati huo, Bw Lumumba anasema kwenye taarifa yake, serikali za nchi za Kiarabu zilikuwa zimekataa ndege hiyo itue nchi zao.

“Kuingilia kati kwake huenda kuliokoa mateka wote na wahudumu wa ndege kutoka kwa mkasa wa kuanguka baharini,” anasema Bw Lumumba.
Anaeleza kuwa uwanja wa ndege, Idi Amin, angewazuru mateka na alihakikisha walipewa chakula na malazi mema. Mateka takriban 100 waliokolewa.

“Habari zinazoenezwa kuhusu kisa hicho cha Entebbe zinafanya ionekane kana kwamba Amin mwenyewe alikuwa mtekaji nyara. Makusudi, wamekaa kimya kuhusu usaidizi wowote ambao huenda (Amin) alitoa kwa mateka hao wa Israeli wakati huo,” anasema Lumumba.

Nduguye Bw Netanyahu, Luteni Kanali Yonatan "Yoni" Netanyahu aliyeongoza makomando 29 wa Israeli ndiye pekee kutoka Israel aliyeuawa wakati wa operesheni hiyo. Wanajeshi 20 wa Uganda waliuawa.

Tanzania na Uganda zajadili ujenzi wa Bomba la mafuta


Uganda na Tanzania zimeanza upya mazungumzo utekelezaji wa makubaliano baina ya viongozi wa mataifa hayo mawili kupitisha mradi wa bomba la mafuta kupitia Hoima Tanga badala ya Hoima - Lamu Kenya.

Ujumbe wa Uganda unaongozwa na waziri wa kawi Irene Muloni huku Tanzania wakiongozwa na Prof Sospeter Muhongo.

Uganda ilielezea wasiwasi wa mabomba ya mafuta kushambuliwa na wanamgambo wa Alshabab.

Wengine wanaohudhuria mazungumzo hayo huko Hoima ni wawakilishi wa kampuni ya kuchimba mafuta yenye asili yake nchini Uingereza Tullow, mjumbe wa kampuni ya kuuza mafuta ya Total yenye asili yake nchini Ufaransa na kisha kampuni ya kichina ya CNOOC inayotekeleza mradi wenyewe wa kuchimba na kuweka bomba la mafuta Kuanzia Hoima hadi bandari ya Tanga.

Bomba hilo la mafuta litakwenda kilomita 1,400km kuanzia Hoima, hadi kwenye bandari ya Tanga.

Mada kuu ya mazungumzo hayo huko Hoima ni utekelezaji wa miradi kwa kuzungumzia hali halisia.

Kwa mfano maswala ya ardhi itakayotumika kwa mradi huo itamilikiwa na nani na itatwaliwa vipi kutoka kwa uma, pia kuna swala la ukubwa wa ardhi yenyewe, wanadani wanasema kuwa mradi huo ulikuwa umependekezwa utekelezwe kwenye ardhi ya takriban mita 20 ,sasa hilo linaonekana kupata upinzani na hivyo kunahoja mbadala ukubwa huo upunguzwe katika mradi huo utakaotekelezwa kwa umbali wa kilomita 1430.

Kenya iliamua kujenga bomba la mafuta kutoka Turkana hadi Lamu
Aidha swala la ujenzi wa mtambo wa kusafishia mafuta wenye thamani ya dola bilioni 2.5 uliopata pigo baada ya Serikali ya Uganda kukatiza mazungumzo na kampuni moja ya Urusi pia utajadiliwa.

Uganda imeanza mazungumzo mbadala na kampuni moja ya ujenzi kutoka Korea Kusini.

Uganda ilikuwa imependekeza kujenga bomba la mafuta safi mkabala na bomba la mafuta la Hoima -Tanga.

Mkurugenzi wa usafirishaji wa mafuta nchini Uganda Robert Kasande akizungumza na wanahabari alisema kuwa tayari wajumbe wamekubaliana mambo mengi kati ya maswala makuu yaliyohitaji kujadiliwa.

Rais John Magufuli atengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo (TIB) na kumteua mwingine


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa mamlaka  aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha sheria ya tafsiri za sheria (Interpretation of Laws Act)  Sura 1, leo tarehe 5 Julai, 2016 ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya TIB Prof. William Lyakurwa.

Kufuatia hatua hiyo, kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 9 (2) cha ya Sheria ya mashirika ya umma (Public Corporations Act) Sura 257, Mhe. Rais amemteua Prof. Palamagamba J. A. M. Kabudi kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya TIB kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kufuatia mabadiliko hayo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango  kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha sheria ya sheria ya tafsiri za sheria (Interpretation of Laws Act)  Sura 1,  ametengua uteuzi wa Wajumbe Bodi ya Benki ya Maendeleo ya TIB.

Aidha, kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 9 (1) cha ya Sheria ya mashirika ya umma (Public Corporations Act, Sura 257) Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango ameteua wajumbe wapya wa Bodi wafuatao kwa kipindi cha miaka mitatu:

1.Gen (Rtd) Mabula Mashauri

2.Razack B. Lokina

3.Rose Aiko

4.Joseph Bwechweshaija

5.Said Seif Mzee

6.Arnold M. Kihaule

7.Maduka Paul Kessy

8.Charles Singili

Uteuzi  wa Mwenyekiti na Wajumbe wapya wa Bodi unaanza tarehe leo 5 Julai, 2016.