Tuesday, 5 July 2016
Waziri Nchemba atoa ahadi kwa Waislamu Nchini
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, amesema kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha taratibu, ratiba na maadhimisho muhimu ya madhehebu ya dini nchini, yanafanyika bila kuvurugwa na baadhi ya watu mwenye nia mbovu.
Mwigulu ambaye pia ni mbunge Jimbo la Iramba Magharibi, aliyasema hayo kwenye hafla ya kufuturisha baada ya viongozi na wananchi wa dhehebu la kiislamu kutoka wilaya zote za mkoa wa Singida. Futari hiyo iliandaliwa na mwenyekiti wa CCM mkoa na mbunge wa viti maalum, Martha Mlata.
Alisema madhehebu ya dini nchini yameendelea kuiwezesha Tanzania iendelee kudumisha amani na utulivu hivyo ni wajibu wa serikali kuyaimarishia ulinzi ili wananchi wake wazidi kupata mafundisho ambayo yatasaidia wananchi wenye nia mbaya wanabadilika na kuwa watu wema.
“Kutokana na mchango huo ambao pamoja na faida zake nyingi ikiwemo wananchi kujiletea maendeleo yao kwa uhuru mpana, sisi wa wizara ya mambo ya ndani, hatukubali ustawi wa madhehebu ya dini uchafuliwe kwa namna yoyote ile”,alisisitiza.
Alisisitiza zaidi, Mwigulu alisema waumini wa dini ya kiislamu wasiwe na hofu wala wasi wasi wowote, kuelekea siku kuu ya Iddi Elftiri na kwamba wataisherehekea bila usumbufu wa aina yo yote.
“Hata ndugu zetu wanaotarajia kwenda kuhiji mwaka huu, wasiwe na hofu yoyote, tutahakikisha hakuna mtu au kikundi cha watu kitakachochafua taratibu zao za kwenda kutimiza nguzo muhimu za dhehebu lao la dini,” alisema Mwigulu.
Kwa upande wake, Mlata alisema ameandaa hafla hiyo ya futari baada ya kusukumwa na imani kwamba Watanzania siku zote, niwa ni wamoja hawabaguliwi na itikadi ya kisiasa wala kwa dini zao.
“Kila Mtanzania anaheshimu imani ya dini ya mwenzake. Kitendo hiki kina mchango mkubwa sana kwenye amani na utulivu wetu, na ndio maana nchi yetu imeendelea kuwa kisiwa cha amani,” alisema mwenyekiti huyo.
Mlata ambaye ni mwimbaji mahiri nchini wa nyimbo za kwaya, pia alitoa msaada wa vitabu vipya vya quran 100 na maboksi matano ya tende.
Labels:
Ulinzi na Usalama
Location:
Singida, Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment