Showing posts with label Ulinzi na Usalama. Show all posts
Showing posts with label Ulinzi na Usalama. Show all posts

Sunday, 17 July 2016

Tanzania na tishio la Ugaidi


Tanzania imefaulu kuepuka mashambulizi ya kigaidi kama yaliyoshuhudia katika mataifa jirani kanda ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo Shambulizi la hivi punde dhidi ya msikiti mmoja nchini Tanzania limeibua tishio la kuibuka kwa ugaidi nchini humo.

Thursday, 14 July 2016

Wanajeshi wa Uganda waingia nchini Sudan Kusini

Hali ya usalama bado ni ya wasiwasi nchini Sudan Kusini licha ya hali ya utulivu kurejea, baada ya mapigano ya mwishoni mwa wiki iliyopita. Hakuna mapigano Alhamisi hii Julai 14 kwa siku ya tatu mfululizo.

Lakini nchi nyingi za kigeni zimeendelea kuwarejesha nyumbani raia wao. Na Alhamisi hii asubuhi, msafara wa majeshi ya Uganda umeingia katika ardhi ya Sudan Kusini, ukiwa na sababu rasmi, kuwarejesha nyumbani raia wa Uganda.

Askari zaidi ya mia moja na malori hamsini kutoka Uganda wameingia katika ardhi ya Sudan Kusini Alhamisi hii Julai 14. Hatua hiyo ilitangazwa siku moja kabla, na msafara ulichelewa kutokana na uamuzi wa Serikali ya Sudan Kusini kufunga mipaka yake.

"Vikosi vyetu vya vya jeshi viko njiani vikieleea katika mji wa Nisitu, kilomita 30 ana mji wa Juba. Hatuna nia ya kwenda mbali zaidi ya mji wa Nisitu, wala nia ya kwenda hadi katika mji wa Juba. Tayari kuna raia 2,000 wa Uganda ambo wanasubiri kurejeshwa nyumbani. Tunaamini kwamba operesheni hii itadumu siku 10, hadi 20, "amesema msemaji wa serikali ya Uganda.

Kuhusu muda wa operesheni, kumekuwa na hisia tofauti. Afisa wa Idara ya Ujasusi ya Uganda amelielezea shirika la habari la AFP kwamba vikosi vya jeshi la Uganda vnaweza kukaa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa mjini Juba, na kuongeza, "tumefanya hivyo katika siku za nyuma, kwa nini tusifanye hivyo kwa sasa? "

Marekani kwa upande wake, tayari imetangaza kwamba imewatuma askari 47 katika mji wa Juba, "kulinda raia na mali ya Marekani." Serikali ya Marekani imeongeza: "kwa sasa mjini Djibouti, askari wa ziada wako tayari kutumwa nchini Sudan Kusini kama itahitajika. "

Monday, 11 July 2016

Sudan Kusini hali si shwari, ndege za kivita zatumika katika mapigano


Uganda imetangaza kwamba itatuma wanajeshi wake katika mpaka wake na Sudan Kusini baada ya mapigano kuzuka upya nchini humo.

Msemaji wa jeshi la Uganda Paddy Ankunda amesema wanajeshi hao watatumwa kuzuia mapigano kuenea hadi maeneo ya Uganda.

Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa mataifa, linawaomba viongozi wakuu wa serikali ya Sudan Kusini, kuyadhibiti majeshi yao.

UN inasema kuwa mashambulio dhidi ya raia na makao makuu pamoja na kambi ya Jeshi ya Umoja wa mataifa, ni uhalifu wa kivita.

Walinda amani wawili wa umoja wa mataifa kutoka Uchina, wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Umoja wa mataifa unasema kwamba, mataifa jirani na Uchina yanafaa kujiandaa kutuma majeshi zaidi nchini humo, ikiwa hali ya usalama itaendelea kudorora .

Wanajeshi wakishika doria mabarabarani katika mji mkuu wa Juba
Hata hivyo baraza hilo litahitaji kuidhinisha vikosi zaidi.

Kwa sasa wanajeshi wa umoja wa mataifa walioko Juba ni elfu 13 pekee.
Mapigano yazuka tena Juba, Sudan Kusini.

Umoja wa mataifa unasema kuwa, walinda amani wanafaa kutumia kila mbinu kuwalinda raia.

Waandishi wa habari wameiambia BBC kuwa ndege za helikopta zimetumika kurusha risasi pande zote huku zikishambulia majengo ya maskani ya bwana Machar.

Wanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir na wale watiifu kwa Riek Machar wamekuwa wakipigana tangu Alhamisi.

Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika makao makuu ya kambi ya kijeshi ya umoja wa mataifa.

Vifaru vya kivita vinaonekana katika barabara za mji mkuu Juba, huku wakaazi wakijifungia ndani ya majumba yao. Mamia ya watu wameuwawa tangu ghasia hizo zianze upya siku tano zilizopita.

Mapigano yaliyoripotiwa kutokea katika uwanja wa ndege mjini Juba, yamesitishwa, huku mashirika mbalimbali ya usafiri wa ndege kuingia na kutoka mjini Juba, likiwemo shirika la ndege nchini Kenya -KQ yamesitisha usafiri.

Mapigano yazuka Sudan Kusini


Msemaji wa jeshi tiifu kwa makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar ameiambia BBC kuwa majeshi yao yanakabiliana na jeshi la serikali tiifu kwa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Kanali William Gatjiath amesema kuwa wanajeshi watiifu kwa bw Machar wamevamia mji mkuu wa Juba kutoka pande zote .

Kanali Gatjiath anasema wanajeshi hao wanalipiza kisasi kufuatia mashambulizi makali kutoka kwa jeshi la rais Kiir.

Serikali haijasema lolote tangu machafuko hayo yaanze muda mchache uliopita.

Awali Wanajeshi wanamuunga mkono makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar walisema kuwa kambi yao ilishambuliwa usiku wa kuamkia leo kwa risasi na bunduki nzito nzito.

Rais Salva Kiir na makamu wa rais Riek Machar wamewasihi wafuasi wao kulinda amani.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini unasema kuwa kulitokea ufyatulianaji wa risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba..
Maeneo yanayodhaniwa kuathirika sana ni yale ya Jebal.

Ujumbe huo unasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa rasasi ulishuhudiwa karibu na kambi ya umoja wa mataifa.

Siku za hivi majuzi ziaidi ya watu 100 wanaripotiwa kuuawa mjini Juba wakati wa mapigano kati ya wafuasi wa rais Salva Kiir na makamu wa rais Riek Machar
Wawili hao walikubaliana kumaliza vita vya wenywe kwa wenyewe na wametoa wito wa kuwepo utulivu.

Ripoti za awali kutoka nchini Sudan Kusini zilisema kuwa takriban watu 100 waliuawa wakati wa mapigano kati ya wanajeshi hasimu katika mji mkuu Juba.

Hata hivyo idadi kamili bado haijulikani lakini wengi wa wale waliouawa wanaripotiwa kuwa wanajeshi.
Mapigano hayo yaliyoanza siku ya Alhamisi yaliendelea hadi mapema Jumamosi.

Mwandishi wa habari mjini Juba anasema kuwa wanajeshi wameweka vizuizi vya barabarani mjini humo.

Anasema kuwa masoko yamefunguliwa lakini watu wengi wamebaki nyumbani.
Sudan Kusini inaadhimisha miaka mitano ya uhuru wake.

Sunday, 10 July 2016

Al-Shabaab walitikisa Jeshi la Polisi Kenya


Jeshi Polisi nchini Kenya hapo jana Jumamosi lilisema kwamba zaidi ya wapiganaji 100 wa dola la Kiislamu walivamia kituo cha polisi Kaskazini-Mashariki mwa Kenya na kujeruhi afisa mmoja na kuondoka na silaha na risasi.

Shambulizi hilo katika kituo cha polisi cha Diff katika wilaya ya Wajir, karibu na mpaka wa Somalia, lilitokea majira ya saa nne usiku siku ya Ijumaa na linadaiwa kufanywa na wapiganaji wa Al Shabaab, kutoka Somalia.

Mkuu wa polisi Joseph Boinnet amethibitisha kutokea kwa shambulio hilo na kusema kuwa maafisa waliweka upinzani mkali na kuwafukuzia mbali licha ya wapiganaji hao kuwa zaidi ya 100 wakiwa katika malori matatu na wakiwa na silaha nzito.

Kituo cha polisi cha Diff kilikumbwa na shambulio kama hili mwezi Aprili mwaka huu wakati maafisa watatu walipojeruhiwa na gari la polisi kuibiwa ambapo viongozi walisema wapiganaji karibu 100 wa Al Shabaab walishiriki pia katika uvamizi huo.

Saturday, 9 July 2016

Baba akesha akilinda wanawe walemavu wa ngozi


Ni mwendo wa saa nne toka jiji la Kampala nchini Uganda hadi kuyafikia makazi ya bwana Mwanje na wake zake wawili Lynda na Florence. Ni katika makazi haya bwana Mwanje ndipo anaishi na watoto wake nane wanaokadiriwa kuwa na miaka mitano hadi kumi na tatu huku watano kati yao wakiwa na ulemavu wa ngozi.

Na watoto wote watano wenye ulemavu wa ngozi amezaa na mkewe mkubwa Florence, wataalam wanaeleza kuwa ulemavu wa ngozi unatokana na upungufu wa madini ya melanin yanayohusika kuweka rangi ya ngozi, macho na nywele.

” Mara ya kwanza kupata mtoto mwenye matatizo ya ulemavu wa ngozi niliogopa sana, sikujua nini nitafanya, mwishowe niliamua kumpenda, nilimpenda zaidi” alisema bwana Mwanje.

Katika familia nyingi kumpata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ni tatizo, wengi wao huwaficha ndani kwa kuogopwa kuchekwa na majirani, hii inatokana na imani potofu inayoenezwa dhidi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi.

Kuna baadhi ya wanaume ambao huwatelekeza wake zao baada ya kuzaliwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi” kuna mambo mengi yasiyo ya kweli katika jamii yangu kuhusiana na wanangu watano kuwa walemavu wa ngozi, wanasema nilimcheka mtu mwenye ulemavu wa ngozi nilipokuwa kijana na akanipa laana na ndiyo sababu ya wanangu kuwa na ulemavu wa ngozi” alisema Florence mke mkubwa wa bwana Mwanje.

Kumekuwa na imani potofu kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi katika nchi zote za Afrika Mashariki, wapo wanaoamini miili ya watu wenye ulemavu ina nguvu ya kutajirisha watu maskini na kuwa matajiri wakubwa. Pia wapo wanaoamini wao ni mizimu ya kweli na siyo binadamu.

Katika nchi ya Tanzania na Malawi kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kutekwa na baadaye kuuwawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na baadhi wakikatwa viungo vyao wa mapanga wangali wazima, kifupi watu wenye ulemavu wanaishi kwa hofu kubwa kulingana na imani hizo kandamizi na potofu.

Nchini Uganda hali tofauti na nchini Tanzania na Malawi lakini ubaguzi wa wazi wa watu wenye ulemavu nchini Uganda ni jambo la kawaida. Katika shule nyingi wanafunzi wanagoma kukaa na watu wenye ulemavu wa ngozi kwenye dawati moja.

” Nilitaka wanangu wapate elimu bora, nikaamua kuwapeleka shule bora lakini tatizo shule iko mbali na makazi yangu, hivyo nilihofia wanangu wanaweza kutekwa. Kwasasa wanasoma shule ya kawaida iliyo jirani na makazi yangu” alisema bwana Mwanje.

“ Jambo lililowahi kunitia hofu zaidi, siku moja mwanagu Robert na wenzake walikuwa wakicheza jirani na shamba langu la mpunga. Mpaka jua linazama walikuwa bado porini wakicheza ghafla walimwona mtu kajificha na akaanza kuwafukuza hali iliyosababisha kila mmoja akimbilie uelekeo wake.

Robert alikimbilia uelekeo wake na wenzake uelekeo mmoja, kutokana na kelele za watoto yule mtu naye alikimbia na mpaka leo hatutajua alikuwa nani na lengo lake lilikuwa nini.” Alisema bwana Mwanje huku akionesha hali ya huzuni na wasiwasi.

“Tangu tukio hilo litoke natumia muda mwingi kukaa jirani na watoto wangu kuhakikisha usalama wao. ”
“ kuna muda napatwa na machungu watoto wangu wanaponiuliza kwanini wako tofauti na sisi, nawajibu kuwa hakuna kitu kibaya, wote tupo sawa ndani ya miili yetu.”

Wednesday, 6 July 2016

Raia waunda vikosi kupambana na Boko Haram


Majuma mawili yaliyopita, Umar Mohammed alikamata mshukiwa kutoka kundi la Boko Haram aliekuwa akijaribu kuingia kwenye mji wa kaskazini mashariki wa Maiduguri akiwa amebeba bomu.

Mohammed ni mmoja kutoka kikosi maalum cha kiraiya maarufu 'Civilian Joint Task Force' (JTF) ambacho kimeidhinishwa na serikali ya jimbo la Borno tangu mwaka wa 2013 kwa lengo la kukabiliana na Boko Haram.

Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi kaskazini mashariki mwa Nigeria na pia kwenye eneo la ziwa Chad kwa miaka saba huku likiuwa zaidi ya watu 20,000 na kusababisha wengine milioni 2.7 kukosa makao.

Operesheni ya kijeshi kwenye eneo hilo imemaliza nguvu za Boko Haram na hata kuliondoa kwenye maeneo ya mjini.

Makundi kama vile 'JTF' pamoja na mengine takriban dazeni moja kwenye eneo hilo pia yamesaidia pakubwa katika kuangamiza kundi hilo.

Tuesday, 5 July 2016

China yafanya mazoezi ya Kijeshi baharini


China inafanya mazoezi ya kijeshi kusini mwa bahari ya China siku chache kabla ya uamuzi muhimu wa mahakama kuhusu mzozo ulio eneo hilo la bahari.

Mazoezi hayo yanafanyika karibu na visiwa vinavyozozaniwa vya Paracel.

Mahakama ya haki mjini Hague inatarajiwa kutoa uamuzi wake wiki ijayo katika kesi iliyowasilishwa na Ufilipino.

China tayari imesema kuwa haitakubali uamuzi huo.
Gazeti moja la serikali The Global Times linasema kuwa China inastahili kujiandaa kukabiliana na Marekani.

Waziri Nchemba atoa ahadi kwa Waislamu Nchini


Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, amesema kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha taratibu, ratiba na maadhimisho muhimu ya madhehebu ya dini nchini, yanafanyika bila kuvurugwa na baadhi ya watu mwenye nia mbovu.

Mwigulu ambaye pia ni mbunge Jimbo la Iramba Magharibi, aliyasema hayo kwenye hafla ya kufuturisha baada ya viongozi na wananchi wa dhehebu la kiislamu kutoka wilaya zote za mkoa wa Singida. Futari hiyo iliandaliwa na mwenyekiti wa CCM mkoa na mbunge wa viti maalum, Martha Mlata.

Alisema madhehebu ya dini nchini yameendelea kuiwezesha Tanzania iendelee kudumisha amani na utulivu hivyo ni wajibu wa serikali kuyaimarishia ulinzi ili wananchi wake wazidi kupata mafundisho ambayo yatasaidia wananchi wenye nia mbaya wanabadilika na kuwa watu wema.

“Kutokana na mchango huo ambao pamoja na faida zake nyingi ikiwemo wananchi kujiletea maendeleo yao kwa uhuru mpana, sisi wa wizara ya mambo ya ndani, hatukubali ustawi wa madhehebu ya dini uchafuliwe kwa namna yoyote ile”,alisisitiza.

Alisisitiza zaidi, Mwigulu alisema waumini wa dini ya kiislamu wasiwe na hofu wala wasi wasi wowote, kuelekea siku kuu ya Iddi Elftiri na kwamba wataisherehekea bila usumbufu wa aina yo yote.

“Hata ndugu zetu wanaotarajia kwenda kuhiji mwaka huu, wasiwe na hofu yoyote, tutahakikisha hakuna mtu au kikundi cha watu kitakachochafua taratibu zao za kwenda kutimiza nguzo muhimu za dhehebu lao la dini,” alisema Mwigulu.

Kwa upande wake, Mlata alisema ameandaa hafla hiyo ya futari baada ya kusukumwa na imani kwamba Watanzania siku zote, niwa ni wamoja hawabaguliwi na itikadi ya kisiasa wala kwa dini zao.

“Kila Mtanzania anaheshimu imani ya dini ya mwenzake. Kitendo hiki kina mchango mkubwa sana kwenye amani na utulivu wetu, na ndio maana nchi yetu imeendelea kuwa kisiwa cha amani,” alisema mwenyekiti huyo.

Mlata ambaye ni mwimbaji mahiri nchini wa nyimbo za kwaya, pia alitoa msaada wa vitabu vipya vya quran 100 na maboksi matano ya tende.

Monday, 4 July 2016

Vienna waandamana kupinga mauji ya Istanbul


Mamia ya watu waliobeba bendera nyekundu za Uturuki nyingine zikiwa na urefu wa mita 10 waliandamana jana jumapili kuelekea uwanja wa Joseph eneo la kihistoria la Vienna.

Waandamanaji hao walikuwa wakipinga mashambulizi ya wiki iliyopita katika uwanja wa ndege wa Instanbul uliouwa watu 45 na karibu 250 kujeruhiwa, wanashutumu sehemu ya serikali ya Austria inayounga mkono wanamgambo wa chama cha PKK -Kurdistan Workers Party ambao wanajulikana kama magaidi katika nchi zote za Austria na Uturuki.

“Serikali ya Austria inabidi iweke msimamo wake dhidi yao alisema Metlhem mwenye umri wa miaka 27” wanaruhusu itokee hapa”.

“Kama wapo kwenye wilaya yeyote lazima waondolewe aliongeza Mustafa Koca mwanafunzi wa mawasiliano ya kompyuta mwenye umri wa miaka 19.

Saturday, 2 July 2016

Serikali ya Bangladesh yatangaza siku mbili za maombolezo kufuatia shambulizi la kigaidi


Serikali ya Bangladesh imetangaza siku mbili za maombolezo baada ya watu 20 wengi wao raia wa kigeni kuuliwa na wanajihadi wa Kiislamu.

Akilihutubia taifa siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu Sheikh Hasina amelaani mauaji hayo na kuwataka wanajihadi hao kuacha kutekeleza mauaji dhidi ya watu wasiokuwa na hatia kwa kisingizio cha kupigania dini ya Kiislamu ambayo amesema ni dini ya amani.

Jeshi nchini humo linasema, wanajihadi hao walivamia mkahawa mmoja jijini Dhaka Ijumaa usiku na kuwateka wateja waliokuwemo na baadaye kuwauawa kwa kuwapiga risasi.

Jeshi lilifanikiwa kumaliza operesheni kujaribu kuwaokoa mateka hao baada ya saa 12 na kuwauawa wanajihadi sita huku mmoja akikamatwa na wateka wengine zaidi ya 10 wakiokolewa.

Kundi la Islamic State limekiri kutekeleza shambulizi hili.

Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi amesema raia wa nchi yake ni miongoni mwa watu waliuliwa.

Ripoti kutoka Italia zinasema raia wake 10 ni miongoni mwa watu hao walipoteza maisha.

Serikali ya Japan inasema raia wake pia ni miongoni mwa watu waliouawa.

Waliotekwa mgahawa wa Dhaka waokolewa


Mateka 13 wameokolewa kutoka katika mgahawa wa Dhaka ambapo wapiganaji wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislam walikuwa wamewakamata mateka baada ya Makomando wa Bangladesh waliojihami vyema kwa silaha kuvamia eneo hilo leo Jumamosi

Mateka hao ikiwa ni pamoja na wageni watatu , kumi raia wa Bangladesh, wameokolewa baada ya makabiliano makali ya risasi kati yao na polisi, maafisa wamesema.

Mpiga picha wa AFP ambaye yupo katika eneo la tukio amesema aliweza kusikia milio mikubwa ya risasi wakati vikosi vya usalama vilipozindua operesheni ya uokozi zaidi ya saa 10 baada ya wanamgambo hao kuwakamata mateka.

Mateka watano wameokolewa katika dakika chache za kuanza kwaoperesheni hiyo, amesema Tuhin Mohammad Masoud kamanda wa juu wa kikosi cha haraka cha makomando wasomi wa Bangladeshi ambao walivamia mgahawa huo.

Friday, 1 July 2016

Watu tisa wauawa kwa kupigwa risasi nchini Kenya


Takriban watu sita wameuawa leo Ijumaa baada ya watu waliokuwa na bunduki kushambulia mabasi mawili nchini Kenya karibu na mpaka wa Somalia.

Mkuu wa Polisi nchini Kenya amethibitisha kwamba maafisa wa polisi wamepata miili ya watu sita lakini akaongeza kuwa operesheni ya kuwasaka magaidi waliotekeleza mauaji hayo imeanza.

Raia wanne na maafisa wawili wa kulinda usalama ambao walikuwa wamejihami wanaaminika kuwa kati ya waliouawa.

Kulingana na gazeti la 'Daily Nation,' mashambulizi hayo yalitokea katika eneo la Elwak, kaunti ya Mandera, nchini Kenya.

Mashambulizi kama hayo katika eneo hilo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya yamekuwa yakitekelezwa na kundi la wanamgambo la Al-Shabaab, walio na makao yao katika nchi jirani ya Somalia. I

UN kulikabidhi majukumu ya Ulinzi na Usalana Jeshi la Polisi nchini Libya


Umoja wa Mataifa unarejesha majukumu ya ulinzi na usalama wa Liberia kwa polisi wa taifa hilo.

Vikosi vya ulinzi vya Umoja wa Mataifa vimekuwa katika majukumu ya kuhakikisha utii wa sheria katika taifa hilo la Afrika Magharibi kwa takribani miaka 13.

Katika kipindi hicho taifa hilo lilivurugwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo maelfu ya watu waliuwawa na wengine waliachwa bila ya makazi.

Umoja wa Mataifa ulionekana mdhamini wa kuaminika wa usalama katika kipindi ambacho kitu pekee kilichokuwa miongoni mwa makabila ni hali ya kutoaminiana.

Lakini janga la ugonjwa wa Ebola la hivi karibuni liliyaweka makundi hayo pamoja na kupunguza hali ya kutofautiana.

Thursday, 30 June 2016

Jambazi sugu Dar mikononi mwa Polisi


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa sugu wa ujambazi aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu Abdallah Bushiri Said ambaye anadaiwa kushiriki matukio mbali mbali ya Uporaji na mauaji ambaye pia anadaiwa kuwa mshirika Mkuu wa Abuu Seif aliyeuawa juzi wakati wa mapambano na Polisi eneo la Buguruni jijini Dar es salaam.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum CP Simon Siro amesema mtuhumiwa huyo ambaye anashikiliwa amekiri kuhusika na matukio makubwa ya unyang’anyi wa kutumia silaha ikiwemo ya mabenki, matukio ya uporaji wa silaha katika vituo vya polisi likiwemo la sitaki shari.

Aidha, jeshi hilo limetangaza kumsaka mtuhumiwa mwingine hatari wa ujambazi Heri Suleiman Mpopezi mwenye asili ya Pemba ambaye alikuwa mwajiri wa kikosi cha JKU Zanzibar na kuacha kazi na kujitumbukiza katika ujambazi wa kutumia silaha.

Bomu laripuka na kuua watu 18 Somalia


Habari kutoka Somalia zinasema kuwa watu 18 wameuawa baada ya bomu kulipuka na kuharibu kabisa basi walimokuwa wakisafiria katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara lililipua gari lililokuwa limewabeba abiria. Wote waliouawa walikuwa raia.

Mashambulizi hayo yalitokea katika mji wa karibu wa Lafole.

Inadhaniwa kuwa washambuliaji hao walikuwa wakilenga gari la wanajeshi lililokuwa karibu.
Mara kwa mara wapiganaji wa Al-Shaabab hulenga wanajeshi wa Serikali.

Uwanja wa Ndege watwaliwa na Waasi nchini Syria


Wapiganaji wa waasi wa Syria wanaosaidiwa na Marekani walichukua udhibiti wa uwanja mdogo wa ndege uliotumika kama kambi na kundi la Islamic State karibu na mpaka wa Irak mapema hapo jana.

Kambi ya jeshi la anga huko Hamdan ilitumika kama kituo muhimu cha kijeshi cha Islamic State karibu na mji wa Al-Bukamal, kilomita chache kutoka Irak.

Kambi hiyo ya jeshi la anga ilitekwa saa kadhaa baada ya kuanzishwa mashambulizi siku ya Jumanne yaliyokuwa na lengo la kufunga njia inayotumiwa na kundi la ugaidi kuingia Syria na Irak.

Kundi la Islamic State lilichukua udhibiti wa Al-Bukamal mwaka 2014 kwa ajili ya operesheni zao za kijeshi na mara moja kuondoa mpaka kati ya Irak na Syria.

Mapigano makali yaripotiwa kusini mwa Burundi


Mapigano makali yanaripotiwa tangu Alhamisi hii Asubuhi katika kijiji cha Mubuga mtaa wa Gasanda, mkoani Bururi, kusini mwa Burundi. Mapigano hayo ni kati ya vikosi vya usalama vikishirikiana na jeshi na kundi la waasi.

Mpaka sasa hasara kufuatia mapigano hayo haijajulikana, lakini chanzo cha polisi kinabaini kwamba mpiganaji mmoja ameuawa na watu wawili wamejeruhiwa, huku wapiganaji watano wakikamatwa na silaha zao.

Kiongozi wa vijana wakereketwa wa chama madarakani (Imbonerakure) na askari polisi wamejeruhiwa kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Bururi, Christian Nkurunziza.

“Mapema asubuhi tulipata taarifa kwamba kuna kundi la majambazi 11 wenye silaha ambao walikua katika kijiji cha Mubuga, vikosi vya usalama viliwaona na kuanza kupambana nao”, amesema mkuu wa mkoa wa Bururi, akihojiwa kwa njia ya simu na RFI.

“Jambazi mmoja ameuawa na wengine watano wamekamatwa”, Christian Nkurunziza ameongeza.

Jambazi au majambazi ni neno linalotumiwa mara kwa mara na serikali, ikimaanisha wapiganaji wa makundi ya waasi yaliyoanzishwa baada ya maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza.

Kwa mujibu wa shahidi ambaye hakutaka jina lake litajwe, “askari polisi mmoja na kijana kutoka kundi la vijana wa chama madarakani (ambao Umoja wa Mataifa unawaita wanamgambo) wamejeruhiwa”.

Mkuu wa mkoa wa Bururi amebaini kuhusu kijana huyo kutoka kundi la vijana wa chama tawala (Imbonerakure) kwamba “mtu aliyejeruhiwa ni raia wa kawaida ambaye alikua aliitikia wito wa serikali wa kushirikiana na vikosi vya usalama kwa kuwakamata majambazi hao.”

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mubuga wameyatoroka makazi yao na wengine wamesema kuwa na hofu ya kuwa huenda mapigano hayo yakachukua muda mrefu.

Mapigano hayo yanatokea wakati ambapo serikali ya Bujumbura imekua ikibaini kwamba tayari imerejesha hali ya utulivu nchini kote.

Hata hivyo hali ya usalama imeendelea kudorora katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, ambapo magruteni na mauaji ya kuvizia au visa vya ulipizaji kisasi vimekua vikiripotiwa.

Machafuko nchini Burundi yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 500, kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na zaidi ya watu 270,000 kukimbilia nje ya nchi kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi, UNHCR.

Wednesday, 29 June 2016

Watatu wauawa na Polisi Tanga


Jeshi la Polisi mkoani Tanga limewahakikishia wananchi kwamba eneo la amboni lipo salama baada ya kuwakamata watuhumiwa watatu, Bunduki 2 aina ya SMG, bastola moja, risasi 30, mapanga na silaha nyingine katika msako maalum ulioshirikisha na vyombo vya ulinzi na usalama.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Leonard Paulo amesema silaha hizo zimepatikana zikiwa zimefukiwa ardhini ambapo watu waliokamatwa wanaaminika ndiyo waliohusika na mauaji ya watu 8 katika Mtaa wa kibatini.

Kamanda Paulo amesema watuhumiwa hao watatu wamefariki kutokana na majeraha waliyopata katika mapambano na vyombo vya usalama akiwemo kiongozi mkubwa wa kundi hilo ambaye ametambuliwa kwa jina la Abu Seif.

Aidha kamanda Paulo ametoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa mbalimbali zitakazowezesha kubaini wahalifu na kuwahakikishia wananchi kuwa eneo la amboni liko salama na limedhibitiwa.

Watu wasiopungua 40 wauawa Sudan Kusini


Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa watu wasiopungua 40 wameuawa katika mapigano yaliyotokea hivi karibuni katika mji wa Wau na kubaini kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka.

Tume ya umoja wa mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, imeweka nyenzo maalum za usalama kuzunguka kambi yake iliyoko kwenye mji wa Wau, kufuatia kuzuka kwa mapigano kati ya wapiganaji wenye silaha na wanajeshi wa Serikali, SPLA.

Kwenye taarifa iliyotolewa na UNMISS, imesema kuwa inaendelea kutoa ulinzi kwa zaidi ya raia elfu 1, ambao wamenaswa kwenye mapigano yaliyoanza mwishoni mwa juma lilillopita.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa baada ya kufikiria kwa kina, iliamua kufungua milango yake siku ya Jumapili na kuruhusu mamia ya raia kuingia kwenye kambi yake, wakikimbia mapigano hayo.

Waziri wa Habari Michael Makuei, amesema kuwa maiti za raia 39 zimepatikana ikiwa ni pamoja na maiti nne za askari polisi.

Katika taarifa iliyotolewa na wakuu wa jimbo la Wau, baada ya kikao cha baraza la usalama la mji huo toka kulipozuka mapigano hayo Jumamosi ya wiki iliyopita, mkuu wa polisi kwenye mji huo, Chol Thuc amesema hali imeanza kurejea kama kawaida.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini alisema kuwa vikosi vyake vilipigana na makundi yaliyokuwa yamejihami pamoja na wale waliowataja kuwa wapiganaji wa makabila.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mapigano kwenye mji huo, ambapo maelfu ya raia wameendelea kuyakimbia makazi yao kwa hofu ya kiusalama.

Mashirika hayo yanautaka umoja wa Mataifa kuingilia kati hali hiyo, kwa kuvisaidia vikosi vya Serikali kukabiliana na makundi ya wapiganaji wenye silaha ambao wameendelea kutekeleza mashambulizi ya kushtukiza kwenye maeneo mengi ya nchi.