Showing posts with label Michezo na Burudani. Show all posts
Showing posts with label Michezo na Burudani. Show all posts

Friday, 8 July 2016

Jerry Muro afungiwa michezo


MKUU wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka na kulipa faini .

Kwa mujibu wa televisheni ya Channel 10, Muro alifungiwa baada ya kikao kilichofanyika jana.

Taarifa nyingine ambazo hazikuthibitishwa zilisema kuwa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana ilichukua hatua hiyo baada ya kikao kirefu.

Habari hizo zilizopatikana jana usiku zilisema Muro alifungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka baada ya kupatikana na hatia ya kuipinga na kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari. Kikao cha Kamati ya Maadili ya TFF, kilikaa jana bila ya Muro kuwepo kwa kuwa wakati mwaliko unatoka alikuwa nje ya Dar es Salaam.

Awali, Muro alisema alikuwa mapumzikoni Machame mkoani Kilimanjaro.

Hatahivyo, msemaji wa TFF, Alfred Lucas alisema jana saa 1:50 usiku kuwa kikao hicho kilikuwa kikiendelea na alishangaa taarifa hizo zilipatikana wapi.

“Na mimi kuna watu wamenipigia wamesema kuna taarifa katika mitandao inasema Jerry kafungiwa, sijui wamezitoa wapi kwani na mimi niko hapa nje na kikao kinaendelea, lakini taarifa kamili kesho saa nne asubuhi”, alisema Lucas.

Wednesday, 6 July 2016

Lionel Messi ahukumiwa kifungo jela


Mchezaji nyota wa Argentina na Barcelona Lionel Messi amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela baada ya kupatikana na makosa ya kutumia ulaghai wakati wa ulipaji ushuru, vyombo vya habari nchini Uhispania vinaripoti.

Babake, Jorge Messi, pia amehukumiwa kufungwa jela kwa kuilaghai Uhispania €4.1m (£3.2m; $4.6m) kati ya 2007 na 2009.

Wakati wa kesi, waendesha mashtaka walisema maeneo salama yenye kinga dhidi ya ushuru Belize na Uruguay yaliyumiwa kuficha mapato kutokana na uuzaji wa haki za picha za mchezaji huyo.

Lakini Messi amesema hakufahamu lolote kuhusu masuala yake ya kifedha.

Wawili hao hata hivyo hawatarajiwi kufungwa jela.
Chini ya mfumo wa haki nchini Uhispania, mtu anaweza kutumikia kifungo chochote kilicho chini ya miaka miwili nje ya gereza.

Messi na baba yake pia wanaweza kukata rufaa katika Mahakama ya Juu nchini humo.

Tuesday, 5 July 2016

Jose Mourinho awapa makavu Wenger na Van Gaal


Limekuwa jambo la kufurahisha kwa kocha mpya wa Manchester United, Jose Mourinho kuwa akirushiana maneno na kocha mwenzake wa Arsenal, Arsene Wenger tangu alipokuwa akiifundisha Chelsea na sasa jambo hilo limeanza kujirudia akiwa na Man United.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari, Mourinho alionekana kuzungumza maneno ambayo yalionekana wazi kumlenga Wenger pamoja na kocha aliyepita kuinoa Manchester United, Louis Van Gaal.

“Mameneja wengine wameshinda kombe miaka 10 iliyopita na wengine hawajaweza kabisa. Mara ya mwisho mimi nimeshinda kombe mwaka uliopita, kwahiyo kama nina vitu vingi vya kurekebisha basi linganisha na wengine,

“Ukweli ni kuwa hilo jambo sio muhimu kwangu, ninacheza dhidi yangu mwenyewe, nina mambo ya kuboresha kwangu sio kwa ajili ya wengine ila mimi na hiyo ndiyo kawaida yangu, siwezi kufanya kazi bila mafanikio,” alisema Mourinho.

Aidha kocha huyo alimzungumzia Giggs na kusema kuwa ” Sio wajibu wangu kuwa Giggs hayupo klabuni, kazi ambayo Ryan alikuwa akihitaji Manchester United ni kuwa meneja,

“Hilo sio wajibu wangu, wamiliki na Mr. Woodward walinitaka mimi na ni muda ambao Ryan alitaka kuwa meneja, hata mimi nilichagua kuwa kocha miaka iliyopita lakini wengi wetu tunaanza kwa kuwa makocha wasaidizi,” alisema kocha huyo.

Kuhusu nafasi ya Rooney katika kikosi chake, Mourinho alisema “Jambo moja ambalo siwezi kulibadili ni kuhusu kubadili nafasi yake ya kufunga magoli, anaweza asiwe mshambuliaji, lakini kwangu hawezi kuwa namba 6, atacheza ndani ya mita 50 kutoka goli la adui,

“Wachezaji wengi wanauwezo wa kutoa pasi lakini kazi ngumu ni kufunga magoli, anaweza kuwa namba 9 au namba 10 au namba 9.5 lakini sio namba 6 au 8,” aliongeza Mourinho.

Sunday, 3 July 2016

Diamond Platinum akubali kumpa heshima Ali Kiba


Meneja wa Diamond, Babu Tale ameonyesha kuwa wao hawana tatizo na Alikiba baada ya kupost kipande cha video kinachoonyesha picha ya msanii huyo ndani ya studio ya Wasafi Records.

Ni muda mrefu imezungumzwa kuwa Diamond na Alikiba wana bifu mpaka kupelekea kuanzishwa kwa baadhi ya team za mitandaoni za kukejeli mafanikio ya msanii wa team nyingine lakini hiyo ni dalili kuwa ipo siku itabaki historia tu.

Babu Tale alipost kipande hicho cha video kinachoonyesha baadhi ya picha za wasanii wakubwa Bongo akiwemo Marehemu Bi Kidude, Mr Blue, Dully Sykes, Juma Nature, Q Chief, Alikiba na wengine wengi.

Je, hiyo inaweza ikawa ndiyo kiki ya kuikaribisha video ya wimbo mpya wa Diamond aliowashirikisha P Square ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni?

Friday, 1 July 2016

Kocha Omog atua rasmi Simba SC


Kocha mpya wa Simba, Joseph Omog amewasili alfajiri hii tayari kwa kuingia mkataba wa kuifundisha timu hiyo.

Baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Omog alipokewa na Katibu mpya wa Simba, Patrick Kahemele na kupelekwa moja kwa moja katika hoteli atakayofikia.

Kocha huyo ambaye awali aliifundisha Azam FC na kuipa ubingwa wa kihistoria, hakuzungumza chochote kutokana na kulalamika uchovu wa safari ingawa alionyesha kuwa na furaha huku akitamka kuwa amefurahia kurudi nchini kujiunga na marafiki zake wengine.

Omog, raia wa Cameron amewasili nchini majira ya saa 8:35 usiku akitokea kwao, leo anatarajiwa kutambulishwa rasmi na uongozi wa Simba zoezi ambalo litatanguliwa na tukio la kusaini mkataba.

Wednesday, 29 June 2016

JPM Mgeni Rasmi mechi ya wabunge wapenzi wa Simba na Yanga


Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mechi ya wabunge mashabiki wa Simba na Yanga inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini hapa jana Mwenyekiti wa Bunge Sports Klabu, William Ngeleja, alisema kuwa mechi hiyo inafanyika mahususi kwa ajili ya kuchangia madawati kwa ajili ya shule za msingi na sekondari nchini.

“Mechi hiyo ambayo huandaliwa na kuchezwa kila mwaka baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti, awamu hii italenga kuisaidia serikali kuchangia madawati ili kusaidia tatizo la upungufu wa madawati lililopo nchini.”

Alisema, mechi hiyo itatanguliwa na michezo ya utangulizi ambayo ni mpira wa pete na kuvuta kamba, kipindi hiki imeandaliwa na Ofisi ya Bunge tofauti na miaka mingine, ambapo huwa inaandaliwa na wabunge wenyewe.

Ngeleja alifafanua kuwa, katika maandalizi hayo Bunge litashirikiana na wadau mbalimbali ambao wataombwa kuunga mkono kwa kuchangia madawati. Alisema, kutakuwa na kituo cha kukusanyia madawati hayo, ambacho kitakuwa ni hapa bungeni na yatakabidhiwa kwa Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah.

“Sisi tunahitaji madawati, lakini mtu akiamua kutuchangia pesa pia tutashukuru hatutakataa tutazitumia kununulia madawati,” alisema.

Kufuatia maandalizi hayo, wameunda kamati ya maandalizi ambayo itazunguka kwa wadau kwa ajili ya kukusanya mchango huo wa madawati.

Alikitaja kikosi kinachoundwa na kamati hiyo ambayo itaongozwa na Mwenyekiti wa kamati ambaye ni Mbunge wa Ulyankulu, John Kadutu, wengine ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabibu.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Busega, Rafael Chegeni, Mbunge wa Igunga, Dalay Kafumu, Mbunge wa Segerea, Bonna Kalua na Mbunge wa Morogoro Mjini, Mohamed Abood.

Ngeleja aliwataja wengine kuwa ni Mbunge Salim Hassan Turki, Mbunge wa Iringa na kocha wa timu ya soka ya Bunge Vanance Mwamoto, Mbunge wa Viti Maalumu Zainabu Vullu na makatibu wawili ambao ni watumishi wa Bunge.

Akijibu swali la kama kususa kwa wabunge wa upinzani kutaathiri mchezo huo, Njeleja alisema hakutaleta athari yoyote katika mechi hiyo, kwani wabunge waliopo ukijumlisha na wafanyakazi wanafikia mia sita, hivyo hawawezi kupwaya.

“Juzi tumecheza pale uwanjani, tulikuwa na mechi na Mtwara na Tabora na tuliwafunga, wachezaji tunao wa kutosha,” alisisitiza.

Aidha, Ngeleja alibainisha kuwa shindano hilo litahudhuriwa na wasanii mbalimbali kutoka ndani ya nchi ambao nao watatumbuiza lakini pia watakuwa na mechi ya utangulizi. Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo maalumu, Zungu, alisema madawati yatakayopatikana yatagawiwa nchi nzima.

“Tunawaomba, vyombo vya habari kuwasaidia kwani lengo letu ni zuri, jambo hilo lichukuliwe kwa uzito ili wadau wajitokeze kwa wingi,” alisema. Naye Mjumbe wa kamati hiyo aliwasihi waandishi wa habari, kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Taswa), kushiriki katika kuchangia mchango huo wa madawati.