Wednesday, 29 June 2016

JPM Mgeni Rasmi mechi ya wabunge wapenzi wa Simba na Yanga


Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mechi ya wabunge mashabiki wa Simba na Yanga inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini hapa jana Mwenyekiti wa Bunge Sports Klabu, William Ngeleja, alisema kuwa mechi hiyo inafanyika mahususi kwa ajili ya kuchangia madawati kwa ajili ya shule za msingi na sekondari nchini.

“Mechi hiyo ambayo huandaliwa na kuchezwa kila mwaka baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti, awamu hii italenga kuisaidia serikali kuchangia madawati ili kusaidia tatizo la upungufu wa madawati lililopo nchini.”

Alisema, mechi hiyo itatanguliwa na michezo ya utangulizi ambayo ni mpira wa pete na kuvuta kamba, kipindi hiki imeandaliwa na Ofisi ya Bunge tofauti na miaka mingine, ambapo huwa inaandaliwa na wabunge wenyewe.

Ngeleja alifafanua kuwa, katika maandalizi hayo Bunge litashirikiana na wadau mbalimbali ambao wataombwa kuunga mkono kwa kuchangia madawati. Alisema, kutakuwa na kituo cha kukusanyia madawati hayo, ambacho kitakuwa ni hapa bungeni na yatakabidhiwa kwa Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah.

“Sisi tunahitaji madawati, lakini mtu akiamua kutuchangia pesa pia tutashukuru hatutakataa tutazitumia kununulia madawati,” alisema.

Kufuatia maandalizi hayo, wameunda kamati ya maandalizi ambayo itazunguka kwa wadau kwa ajili ya kukusanya mchango huo wa madawati.

Alikitaja kikosi kinachoundwa na kamati hiyo ambayo itaongozwa na Mwenyekiti wa kamati ambaye ni Mbunge wa Ulyankulu, John Kadutu, wengine ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabibu.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Busega, Rafael Chegeni, Mbunge wa Igunga, Dalay Kafumu, Mbunge wa Segerea, Bonna Kalua na Mbunge wa Morogoro Mjini, Mohamed Abood.

Ngeleja aliwataja wengine kuwa ni Mbunge Salim Hassan Turki, Mbunge wa Iringa na kocha wa timu ya soka ya Bunge Vanance Mwamoto, Mbunge wa Viti Maalumu Zainabu Vullu na makatibu wawili ambao ni watumishi wa Bunge.

Akijibu swali la kama kususa kwa wabunge wa upinzani kutaathiri mchezo huo, Njeleja alisema hakutaleta athari yoyote katika mechi hiyo, kwani wabunge waliopo ukijumlisha na wafanyakazi wanafikia mia sita, hivyo hawawezi kupwaya.

“Juzi tumecheza pale uwanjani, tulikuwa na mechi na Mtwara na Tabora na tuliwafunga, wachezaji tunao wa kutosha,” alisisitiza.

Aidha, Ngeleja alibainisha kuwa shindano hilo litahudhuriwa na wasanii mbalimbali kutoka ndani ya nchi ambao nao watatumbuiza lakini pia watakuwa na mechi ya utangulizi. Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo maalumu, Zungu, alisema madawati yatakayopatikana yatagawiwa nchi nzima.

“Tunawaomba, vyombo vya habari kuwasaidia kwani lengo letu ni zuri, jambo hilo lichukuliwe kwa uzito ili wadau wajitokeze kwa wingi,” alisema. Naye Mjumbe wa kamati hiyo aliwasihi waandishi wa habari, kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Taswa), kushiriki katika kuchangia mchango huo wa madawati.

No comments:

Post a Comment