Showing posts with label Ugaidi. Show all posts
Showing posts with label Ugaidi. Show all posts

Friday, 15 July 2016

Makumi wauawa katika Shambulizi la kigaidi Mjini Nice, Ufaransa


Zaidi ya watu 70 wameripotiwa kuuawa katika shambulio lililotokea katika mji wa Nice kaskazini mwa Ufaransa.

Lori lililokuwa likienda mwendo kasi lilijiingiza katika mkusanyiko wa watu waliokuwa wakiangalia maonesho ya fataki kuadhimisha siku ya kitaifa ya Bastille, ambayo huja na shamra shamra kila mwaka.

Mwendesha mashtaka katika mji wa Nice, Jean- Michel Pretre amesema lori hilo liliendelea kutembea kilo mita mbili kabla ya polisi kumpiga risasi dereva.

Bunduki na makombora yameripotiwa kukutwa ndani ya lori hilo.

Wakazi wa mji huo wa Nice wameshauriwa kutulia majumbani.

Rais Francois Hollande amerudi mjini Paris kwa ajili ya kufanya kikao cha dharura.

Hali ya tahadhari iliyowekwa toka kutokea kwa shambulio lililofanywa na Islamic State mjini Paris, bado iko palepale nchini Ufaransa.

Monday, 11 July 2016

Baada ya kifo cha Osama bin Laden mwanaye aapa kulipiza kisasi


Mwana wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden, ameapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya baba yake.
Katika ujumbe wa sauti uliochapishwa katika mitandao Hamza bin Laden ameapa kulipiza kisasi kwa Marekani kwa kumuua babake 2011 huko Pakistan.

Ujumbe huo wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama,", Hamza ambaye inaaminika kuwa alikuwa na babake makomando wa Marekani walipowavamia na kumtwaa ameapa kuendeleza kazi aliyoianza babake.

Ujumbe huo ni wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama,"
''Tutaendelea kuwasaka na kuwapiga popote pale mtakapokuwa mumejificha ati nyuma ya pazia za usalama kwa maovu munayoyaendeleza, Palestina, Afghanistan, Syria, Iraq, Yemen, Somalia na kote kwenye ardhi ya waislamu mnayokalia '' shirika la habari la Reuters linamnukuu.
''Na kwa wale wanaodhania kuwa tutakuwa tukilipiza kisasi mauaji ya Osma ole wenu, kwa nini sisi tutakuwa tukilinda dini ya kiislamu'' alisema Hamza.

Osama aliuawa na makomando wa marekani katika maficho yake huko Pakistan mwaka wa 2011.

Hamza ambaye kwa sasa ana umri wa kati ya miaka ishirini hivi alikuwa na babake kabla ya mashambulizi ya kigaidi ya mwaka wa 9/2001 huko Afghanistan kabla ya kukimbilia Pakistan kufuatia mashambulizi makali ya Marekani na washirika wake.

Hamza kulingana na wachanganuzi anatambulishwa na kiongozi wa kidini wa kundi hilo Ayman al-Zawahiri katika ujumbe huo unaolenga kuwavutia vijana ambao kwa sasa wamejiunga kwa wingi na kundi la Islamic state.

Saturday, 2 July 2016

Mji wa Baidoa washambuliwa na Al-Shabaab

Mashahidi na maafisa wa usalama nchini Somalia wamesema Jumamosi kwamba watoto wawili waliuwawa kufuatia shambulizi la bomu lililofanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab huko kusini-magharibi mwa Somalia katika mji wa Baidoa.

Mfanyakazi mmoja wa gari la wagonjwa, Yahya Isak Hassan, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika eneo la Hawlwadag mahala ambapo makombora yalipigwa.

Hassan alisema kwamba mizunguko 11 ya makombora ilipiga maeneo kadhaa na kuuwa watoto wawili, wote wasichana wenye umri wa miaka minne na mitano.

Hassan alisema msichana mmoja alifariki papo hapo kombora lilipopiga nyumba yao na mtoto wa pili alifariki akiwa hospitali. Watu 19 wengine walijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Thursday, 30 June 2016

Tishio la Dola la Kiislam kuikumba Kenya


Imebainika kwamba ushawishi wa kundi la Dola la Kiislamu Afrika Mashariki umeongezeka kwa kuwaandikisha vijana wa Kenya kuendesha mapambano ya jihadi nchi za nje na baadhi yao kurudi Kenya kuitishia nchi hiyo.

Mashirika ya ujasusi nchini Kenya yanakadiria kwamba takriban wanaume na wanawake 100 yumkini wakawa wamekwenda kujiunga na kundi la Dola la Kiislamu nchini Libya na Syria na kuzusha wasi wasi kwamba baadhi yao huenda wakarudi nchini humo kufanya mashambulizi kwa Kenya na katika vituo vya kigeni, katika nchi ambayo tayari ni muhanga wa mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika kila mara nchini humo.

Rashid Abdi mchambuzi mwandamizi katika Shirika la Kimataifa la Kushughulikia Mizozo ambalo ni jopo la ushauri lilioko katika mji mkuu wa Kenya Nairobi amesema, "Kwamba hivi sasa kuna tishio la kweli linaloikabili Kenya kutoka kundi la Dola la Kiislamu na hatari hiyo itazidi kuongezeka."

Tatizo la wafuasi wa itikadi kali ambao mara nyingi ni watu wenye shauku lakini wasiokuwa na mafunzo, kupatiwa mafunzo stadi ya kigaidi na kundi la Dola la Kiislamu na kurudi nyumbani kufanya mashambulizi ni tatizo ambalo tayari mataifa ya Ulaya yanakabiliana nalo na yumkini hivi karibuni likawa pia ni tatizo kwa Kenya.

Mshauri elekezi wa masuala ya usalama na afisa polisi wa zamani George Musamali ameliita hilo kuwa ni "bomu linasubiri kuripuka."Amesema watu kwenda Libya au Syria sio tatizo kwa Kenya tatizo ni kile watakachokifanya wakati watakaporudi.

Wanajeshi wa Kenya kufuatia shambulio katika chuo kikuu cha Garissa 2015.
Shambulio la kwanza la kigaidi la Al-Qaeda nchini Kenya ilikuwa ni kuripuliwa kwa ubalozi wa Marekani hapo mwaka 1998 na hivi karibuni kabisa yalikuwa ni mauaji katika chuo kikuu cha Garissa mwaka jana lakini tishio la Dola la Kiislamu ni jipya na bado kueleweka vyema.

Hapo mwezi wa Machi wanaume wanne walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutaka kwenda Libya kuijunga na kundi la Dola la Kiislamu.

Baadae hapo mwezi wa Mei polisi ya Kenya ilitangaza kukamatwa kwa mwanafunzi wa udaktari,mke wake na shoga yake wanaotuhumiwa kuwaandikisha watu kujiunga na kundi la Dola la Kiislamu na kupanga shambulio la kibiolojia kwa kutumia anthrax.

Inasemekana wanafunzi wengine wawili wa udaktari wamekimbia.
Wanafunzi wa Kenya katika kumbukumbu ya shambulio la chuo kikuu cha Garissa.

Wiki tatu baadae polisi ya Kenya ilitangaza kukamatwa kwa wanachama wengine wawili wa mtandao wa kundi la Dola la Kiislamu ambao ulikuwa ukitaka kujipenyeza Kenya ili kuweza kufanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Wakenya wasiokuwa na hatia.

Polisi ilisema imegunduwa vitu ambayo hutumiwa na magaidi kutengeneza mabomu ya kienyeji pamoja na mikuki na mishale iliotiwa sumu.

Wakati baadhi ya wataalamu wanatupilia mbali ishara ya shambulio kubwa lainyemelea Kenya wanakiri kwamba kuna tishio la dhati la kundi la Dola la Kiislamu kupandikiza itikadi kali,kuandikisha watu kujiunga nalo na baadae kuwarudisha nyumbani.