Showing posts with label Tanzia. Show all posts
Showing posts with label Tanzia. Show all posts

Friday, 8 July 2016

Lowassa ashiriki Mazishi ya Beatrice Shelukindo


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amekuwa miongoni mwa mamia ya waombolezaji walioshiriki maziko ya mbunge wa zamani, Beatrice Shelukindo (58) yaliyofanyika nyumbani kwa wazazi wake katika kata ya Olorien Jijini Arusha jana.

Viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo yaliyotanguliwa na ibada ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Jaji Mkuu mstaafu, Agustino Ramadhani, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.

Pia maziko hayo yalihudhuriwa na wabunge na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mkoa wa Tanga na Arusha, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro na viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali. Ibada ilifanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro ambako Askofu mstaafu, Simon Makundi, alisema Beatrice hakuwa fisadi na alitoa mchango mkubwa kwa familia, dini, taifa na Afrika Mashariki.

“Jiulize wewe una mchango gani hata katika familia yako, dini yako, taifa hili na hata kwa Afrika Mashariki?” Alihoji Makundi.

Aliwataka mamia ya waombolezaji wakipewa nafasi, heshima na vyeo serikalini au katika kampuni yo yote kuitunza heshima hiyo kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa na hofu ya Mungu.

Beatrice aliyezaliwa mwaka 1958 amefariki akiwa na umri wa miaka 58, jambo ambalo askofu mstaafu alisema hiyo ni neema ya Mungu.

Alisisitiza kuwa Beatrice alifanya kazi za utumishi serikalini na ubunge kwa uadilifu mkubwa na kupata heshima na serikali, dini na jamii na ndiyo maana aliweza kuhitimisha heshima hiyo hadi mwisho. Askofu Makundi alisema alipata bahati ya kuzungumza naye kabla ya mauti.

Sunday, 3 July 2016

Beatrice Shelukindo afariki dunia


Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilindi Beatrice Shellukindo (CCM) ameaga dunia jana Jijini Arusha.

Akithibitisha kifo hicho Katibu wa CCM Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga, Hawa Nanganyau alisema marehemu  ameugua tangu  mwaka 2014 akisumbuliwa na tatizo la mgongo pamoja na miguu.

Beatrice mpaka anafikwa na umauti alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC)  kupitia Wilaya ya Kilindi.

Katibu huyo wa CCM  amesema marehemu ameacha watoto watatu wote wa kiume  na atazikwa siku ya Jumatano saa sita mchana jijini Arusha.

Friday, 1 July 2016

Kanisa la RC latanga kifo cha Padri wa DRC


Askofu wa Butembo-Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sikuli Paluku Melchisédech, ametangaza kifo cha Padri Malumalu kilichotokea Alhamisi Juni 30 2016 katika mji wa Dallas nchini Marekani.

"Tunatoa rambirambi zetu kwa familia ya Padri Apollinaire Malumalu, kwa makuhani wote, kwa waumini wa Kanisa Katoliki la Butembo-Beni na wale wote ambao wamehuzunishwa na taarifa hii ya kusikitisha," imebaini taarifa iliyotolewa na Kanisa Katoliki.

Taarifa ya kifo cha Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) imethibitishwa na ndugu yake, Emmanuel Tavulya.

"Padri Apollinaire Malulmalu alikuwa mgonjwa. Aliumwa kwa muda mrefu. Kwa siku ya leo, Mwenye Enzi Mungu kuamua vinginevyo, kinyume na yale ambayo tlikua tukitarajia. Ni kweli kwamba Mungu kampenda zaidi. Padri Malumalu amefariki dunia saa 4:30 usiku (saa za mjini Kinshasa), karibu 10:30 alaasiri, saa za mjini Dallas, " amesema Emmanuel Tavulya.

Alisema kuwa hana maelezo kuhusu mpango wa kuusafirisha mwili wa marehemu na lini mazishi yatafanyika, akielezea kuwa marehemu alikuwa Mkuu wa Dayosisi ya Butembo-Beni na rais wa zamani wa CENI.

"Kwa sasa, nitapendelea kuishia kwa hii habari ya huzuni kwa sababu kutakuwa na maandalizi mazima kwa ajili shughuli hii. Mtapewa taarifa katika masaa au siku za mbele, " Bw Tavulya ameongeza.

Padri Apollinaire Malumalu alikua Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini DRC mara mbili. Kwanza kati ya mwaka 2006 na 2011. Na alikua Mwenyekiti wa tume hiyo wakati wa uchaguzi wa rais na wa wabunge mwaka 2006. Alirudi kuwa Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi mwaka 2013 kabla ya kujiuzulu mwaka 2015 kwa sababu za kiafya. Alikwenda kufanyiwa matibabu nchini Marekani.

Tarehe 1 Juni, balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini Marekani, François Balumuene, alitangaza kifo cha Padri Malumalu kwa vyombo vya habari. Taarifa iliyokanushwa na msemaji wa serikali ya Congo ambaye wakati huo alibaini kwamba mapigo ya moyo wa Mwenyekiti wa zamani wa CENI bado yanasikika.

Sunday, 26 June 2016

Tanzia: Antony Gervase Mbassa (Mb.) afariki


Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Mkoani Kagera kwa Tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amefariki Usiku wa kuamkia Leo.

Dk. Anthony Gervase Mbassa (Chadema) amefariki Usiku wa Kuamkia leo Jumapili Juni 26, 2016. Chanzo hakijajulikana kwani amepatwa na umauti ghafla.