Friday, 15 July 2016

BAVICHA wakubali yaishe Mkutano Mkuu wa CCM


Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Mkoa wa Rukwa  limetangaza kuwa hawatakwenda  kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bavicha mkoani humo, Aida Khenan amesema wametii agizo la Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe la kuwazuia kwenda Dodoma.

“Tumeheshimu agizo la Mbowe ambalo limejaa busara na hekima kubwa  japokuwa  tulikuwa tayari kwenda Dodoma,” amesema Khenan ambaye pia  ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema).

Katibu wa Bavicha Mkoa wa Rukwa, Deogratis Kashatila  ameishauri Serikali  ya CCM isivizuie  vyama  vya  siasa kufanya mikutano kwa kuwa nchi ilisharidhia mfumo wa vyama vingi kwani ni kinyume na katiba.

Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi alinukuliwa akisema baraza hilo limeamua kuzuia mkutano huo wa CCM kutokana na tamko la Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yote ya kisiasa. “Hakuna mkutano wowote wa siasa unaotakiwa kufanyika, iweje CCM waandae mkutano huo, sisi vijana wa Chadema tutakuwapo Dodoma kuzuia,” amesema

No comments:

Post a Comment