Baadhi ya makada wa CCM walioshindwa kwenye mbio za urais na ubunge kuteuliwa kushika nafasi za Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), wamezua mjadala kwa kile kilichoelezwa kuwa nafasi hizo ni za kiutendaji hivyo zinahitaji wasomi na wenye uzoefu serikalini.
Makada hao ni miongoni mwa watu 40 wapya kati ya 134 waliotangazwa juzi na Ofisi ya Rais-Utumishi kushika nafasi hizo kwenye uongozi wa wilaya.
Miongoni mwa makada waliotangazwa kuteuliwa kuwa Ma-DAS ni Amos Siyamtemi, ambaye aligombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, lakini akaishia ndani ya mchakato wa CCM, Kasilda Mgeni, mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Star TV ambaye alikuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM na aligombea ubunge wa viti maalumu mwaka 2010 bila ya mafanikio.
Wengine ni Mtella Mwampambwa, Aboubakar Assenga, Jasinta Mboneko, Gift Msuya, Hashim Mkomba, Edward Mpogolo na Adam Mzee, ambao wamewahi kugombea ubunge, udiwani au kushika nafasi kwenye ngazi tofauti za uongozi wa CCM.
Katibu mkuu wa Wizara ya Utumishi, Dk Laurian Ndumbaro amesema kuna theluthi moja ya wateule wanaohitaji mafunzo ya muda mfupi ili kuwaandaa kukabiliana na changamoto za majukumu mapya waliyokabidhiwa.
Amesema wengi wana elimu ya kutosha na wanachohitaji ni kuzifahamu sheria na taratibu za utekelezaji wa majukumu yao.
Mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana amesema: “Kama tungetaka kutenda haki, nafasi hizo zingetangazwa.”
Amesema uofisa tawala ni nafasi kubwa katika uendeshaji wa wilaya na Serikali kwa ujumla na hivyo unahitaji mtu aliye ndani serikalini na mwenye uzoefu.
No comments:
Post a Comment