Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na washtakiwa wa kesi ya uchochezi, akiwamo mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu dhidi yake ikisema ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi mwisho.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, mwandishi, Idrissa Jabir Yunus na mchapishaji wa gazeti hilo, Ismail Mehboob.
Hakimu Thomas Simba amesema kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo tofauti na inavyodhaniwa na washtakiwa hao.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi hiyo kwa kuandika na kuchapisha makala katika gazeti la Mawio la Januari 14-20, mwaka huu yenye kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar.”
Awali, Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala aliweka pingamizi akidai Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa Kifungu cha Sheria ya Magazeti kilichotumiwa kuwashtaki kinatumika Tanzania Bara tu na si Zanzibar.
Amedai Tanzania ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano inayojitegemea na kwamba mashtaka hayo yanazungumziwa kuwa yanasababisha chuki dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikikiliza.
Hata hivyo, katika uamuzi wake jana, Hakimu Simba alifafanua kuwa kifungu cha Sheria ya Magazeti kilichotumika kuwashtaki kinatumika hata Zanzibar.
Pia, Mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja nyingine ya pingamizi la upande wa utetezi la uhalali wa shtaka la tatu, ikisema liko mahakamani kiusahihi.
Wakili Kibatala katika pingamizi lake kuhusiana na shtaka hilo alidai maelezo hayakidhi vigezo vya kisheria kulifanya liwe la uchochezi na hayako wazi ili washtakiwa wajitetee, hivyo aliiomba mahakama kulifuta.
Hakimu Simba alikubaliana na hoja za upande wa mashtaka kuwa shtaka hilo ni sahihi na linajitosheleza.
No comments:
Post a Comment