Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema kwamba watu waliokuwa wanapata fedha za bure bure wameanza kusema kwamba fedha zimeisha.
Rais Dkt. Magufuli ameyasema hayo alipokuwa akitoa hotuba wakati wa kushiriki hafla ya Baraza la Eid el Fitri iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.
''Watu waliokuwa wanapata pesa za bure bure wameanza kusema pesa zimeisha, hauwezi kupata pesa kama haufanyi kazi '' -Amesema Dkt. Magufuli.
Rais amesisitiza kwamba katika hatua za serikali yake kuleta heshima serikalini ni lazima watu wachache waumie kwa manufaa ya wengi.
''Nchi hii imejaa madini ya kila aina na juzi imegundulika helium na bado rasilimali nyingine lakini cha kushangaza bado tupo masikini lazima tushughulikie hili na katika kuleta ufanisi lazima wachache waumie ili wengi ambao walikuwa wanadhulumiwa wanufaike na taifa lao'' Amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais amewataka waumini wote wa dini ya kiislamu kusherekea kwa amani na kudumisha amani ya nchi kwa kufuata yale yote ambayo viongozi wa dini wamefundisha muda wote wa mfungo.
Akimkaribisha mgeni rasmi Mufti wa Tanzania Abubakar Zuberi amewataka waislamu kuwa na upendo na kudumisha amani kwa maslahi ya taifa letu.
No comments:
Post a Comment