Showing posts with label Habarii za Kisiasa. Show all posts
Showing posts with label Habarii za Kisiasa. Show all posts

Wednesday, 22 June 2016

Charles Kitwanga anena, mjengoni Dodoma wiki ijayo


Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema yupo imara na amerejea nchini akiwa na matumaini mapya.
Pamoja na hali hiyo, amesema kuwa hivi sasa anajipanga kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha anaisaidia nchi pamoja na wapigakura wake na kuwa na maendeleo ya kweli na Jumatano ya Julai 29, ataripoti bungeni.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana baada ya kurejea akitokea nchini Israel ambako alikwenda kwa shughuli zake binafsi. Alisema licha ya mtihani uliomkuta, kwa sasa yupo imara kwa ajili ya kuwatumikia wapigakura wake kwa kuwawakilisha vema ndani ya Bunge.

“Niko imara kabisa na nina nguvu na matumaini mapya, nimeingia nchini jana (juzi) nikitokea nchini Israel ambako nilikuwa na shughuli zangu binafsi. Unajua mimi ni mtaalamu (wa mawasiliano) na wewe unajua kabla sijaingia kwenye siasa nilikuwa nafanya nini.

“Kifupi ninasema nilikwenda Israel kwa shughuli zangu binafsi kabisa ambazo kwa kipindi cha wiki tatu nilizokuwa huko nimefanya. Hata wanaosema nilikwenda kulia kwa Bwana nao ni mawazo yao, maana unajua ile ni nchi takatifu kutokana na historia yake,” alisema Kitwanga.

Alipoulizwa amepokeaje hatua ya kufutwa kwake kazi na Rais John Magufuli kwa kile kilichoelezwa ni ulevi, alisema kwa sasa hawezi kusemea jambo hilo kwani aliyemteua ndiye mwenye mamlaka ya kumwajibisha.

“Rais ni mtu mkubwa anaweza kufanya jambo lolote ili mradi havunji sheria, hata kilichotokea kwangu ni mamlaka yake halali, ingawa Mungu ndiye muweza wa kila jambo. Mimi ni Mkristo safi, nasi tumefundishwa kusamehe saba mara sabini na kusahau yaliyopita,” alisema.

Akieleza mikakati yake, Kitwanga alisema kuwa baada ya kuripoti bungeni wiki ijayo, atakuwa na ziara ya wiki tano ndani ya jimbo lake ambako atazungumza na wapigakura wake na kueleza yaliyomsibu hatua kwa hatua.

“Sitaki kuingia ndani sana ila mengine nitayasema nikiwa jimboni, lakini si kwa lengo la kubishana na mtu, na uzuri kila hatua ambayo nimepitia hata wapigakura wangu walikuwepo kwa uwakilishi wa madiwani wa Misungwi ambao walikuwa mjini Dodoma,” alisema.

Mei 21, mwaka huu, Rais Magufuli alimng’oa Kitwanga kuhudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na madai ya ulevi, huku taarifa zaidi za ndani zikieleza kuwa alianza kushughulikiwa bila yeye mwenyewe kujua.

Tuesday, 21 June 2016

Trump amfukuza kazi Kampeni Meneja wake


Mgombea mtarajiwa wa chama cha Republikan Donald Trump amemfukuza kazi kampeni meneja wake Corey Lewandoski.

“Leandowski hatafanya kazi nasi tena kwenye kampeni” msemaji wa kampeni Hope Hicks alisema hayo Jumatatu . Hicks alitoa shukrani kwa kazi nzuri ya Lewarndowski.

Lewandowski ambaye alifanya kazi na Trump tangu Juni mwaka jana alililezwa na wachambuzi wengi wa siasa kama mtu mwenye mahusiano mabaya na waandishi wa habari kadhaa na pia mahusiano yalioingia doa na baadhi ya maafisa wa chama cha Republikan.

Alizungumzwa na kufuatiliwa sana baada ya shutuma za kumsukuma vibaya mwandishi wa habari wa kike huko Florida wakati wa kipindi cha kampeni za awali. Lewandowski pia alikuwa na mvutano na mwenyekiti wa kampeni za Trump Paul Manafort.

Kura za maoni za Trump zimekuwa zikishuka na anakumbana na watu wanaompinga ndani ya chama cha Republikan ambao wana wasi wasi juu ya matamshi yake makali.

Sunday, 19 June 2016

Ndoa zinazovunjika nchini zaongezeka


Takwimu za kuvunjika kwa ndoa zinaongezeka kwa kasi na sasa siyo kifo kinachowatenganisha wapendanao, bali sheria hulazimika kuchukua mkondo wake.

Idadi ya talaka zilizosajiliwa na Wakala wa Usajili wa Vizazi, Vifo, Talaka na Ndoa (Rita) kwa mwaka 2013/14 ni  99;  mwaka  2014/15  zilikuwa talaka 150.

Kwa mujibu wa Rita licha ya kuwa ndoa nyingi zinavunjika, lakini hazivunjwi kisheria na talaka zinazotolewa ni batili kwa sababu hazitambuliwi na wakala huyo.

Meneja wa Mawasiliano, Taarifa na Elimu kwa Umma wa Rita, Josephat Kimaro amesema kuachana kienyeji au kupeana talaka zisizotambuliwa na Rita kuna madhara lukuki,  ikiwamo kukosa mirathi, kushindwa kuoa au kuolewa na kusababisha migogoro kwenye familia.

Saturday, 18 June 2016

Pigo jingine tena kwa Wabunge wa Upinzani


Wabunge wawili wa Viti Maalumu wa Chadema, Suzan Lyimo na Anatropia Theonest wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa  kusema uongo bungeni.

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema  bungeni Dodoma jana kuwa  kwa kutumia Kanuni ya 63 (8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, ameridhia mapendekezo ya taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyowatia hatiani wabunge hao baada ya kuwahoji na kushindwa kuthibitisha madai yao.

Katika adhabu hiyo ,  Lyimo amesimamishwa kuhudhuria vikao vitano kuanzia jana hadi Juni 24, huku Theonest akisimamishwa kuhudhuria vikao vitatu kuanzia jana hadi Juni 22.

Wawakilishi hao pia, hawataruhusiwa kuingia viwanja vya Bunge na watakatwa nusu ya mishahara yao na posho kwa kipindi watakachokuwa wakitumikia adhabu hizo, kwa mujibu wa masharti ya kanuni ya 75 za Kanuni za Kudumu za Bunge.

Wakenya wakoshwa na Rais Magufuli


Makamu mkuu wa  Shule Kuu ya Biashara ya Strathmore (SBS) ya jijini Nairobi, Dk Vincent Ogutu amesema Wakenya wamefurahi kuona namna Rais John Magufuli anavyopinga ufisadi kwa kusimamia sheria.

Akizungumza kwenye mkutano wa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi (CEOrt) juzi, amesema  Serikali zina sheria nyingi nzuri, lakini hazina viongozi wenye uwezo wa kuzisimamia ipasavyo.

Amesema anatamani kuona nchi za Afrika Mashariki zinapata aina moja ya mafunzo ya uongozi kwa kuwa tofauti nyingi zilizokuwapo awali zimeondolewa.

Mkurugenzi wa SBS, Dk George Njenga amesema upo umuhimu kwa viongozi kufundishwa maadili ili waondokane na tabia ya kuwajengea hofu wananchi.

Dr. Besigye aomba aachiwe kwa Dhamana


Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani nchini Uganda cha FDC, Dr Kizza Besigye, amewasilisha jalada kwenye mahakama kuu ya jijini Kampala, akiomba kupatiwa dhamana.

Besigye, ambaye kwa sasa anashikiliwa kwenye gereza la Luzira akikabiliwa na mashtaka ya uhaini baada ya kutangaza kujiapisha mwenyewe kama rais wa Uganda, aliwasilisha maombi ya kupatiwa dhamana June 7.

Besigye ambaye kwenye maombi yako alitumia anuani ya gereza la Luzira kama makazi yake, aliandika sababu 10 kwa mahakama kwanini ikubali kumuachia kwa dhamana, ikiwemo kufikisha umri wa miaka 60 na kutoingilia upelelezi unaoendelea dhidi yake.

Haya yanajiri wakati huu ambapo juma hili, mahakama kuu iliukatalia upande wa mashtaka kuhamisha kesi ya Besigye kutoka jijini Kampala.
Uamuzi wa Besigye kuomba kupatiwa dhamana umekuja baada ya majuma kadhaa ya kushuhudia kesi yake ikiahirishwa mahakamani kwa kile upande wa mashtaka unadai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Ofisi ya mwendesha mashtaka nchini Uganda wameiambia mahakama kuwa, Besigye hana vigezo vya kupewa dhamana kutokana na kosa lenyewe pamoja na uwezekano wa yeye akiwa nje kuingilia upelelezi unaoendelea.

Vyama vya upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Uganda, zinakosoa mfumo wa mahakama kuingiliwa na mamlaka za Serikali, ambapo wanadai kuwa maamuzi yanayotolewa na majaji kwenye kesi hiyo, yamekuwa ya kuegemea upande wa Serikali.

Mara kadhaa wabunge wa upinzani wamekuwa wakishinikiza Serikali kumuachia huru Besigye, ambapo wakati wa usomwaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2016/17, wabunge hao waliingia na mabango na kupiga kelele kumtaka Rais Museveni amuachie huru.

Wanaharakati Mombasa waikosoa Mahakama


Mahakama nchini Kenya imetupilia mbali pingamizi lililokuwa limewasilishwa kupinga mtu mmoja kufanyiwa uchunguzi wa njia ya haja kubwa kubaini ikiwa alikuwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja au la.

Uamuzi wa mahakama kutupilia mbali pingamizi hili, umekosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yanasema kuwa kuruhusu Polisi kufanya uchunguzi huo unaenda kinyume na haki za binadamu.

Kesi hiyo iliwasilishwa na watu wawili waliopinga hatua ya Polisi kuomba mahakama kuruhusu mtuhumiwa kufanyiwa vipimo vya sehemu ya haja kubwa ili kuwasaidia kujua ikiwa alikuwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja au la.

Jaji Anyara Emukule wa mahakama kuu ya mjini Mombasa, akisoma uamuzi wake, amesema kuwa Polisi haikuwa na njia nyingine kuthibitisha ikiwa mtuhumiwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja au la, ila kwa kumfanyia vipimo vya sehemu yake ya haja kubwa.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya, mtu anayebainika kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja atakabiliwa na kifungo cha miaka 14 jela licha ya kuwa hakuna kesi nyingi zinazohusu ushoga kwenye taifa hilo.

Mtuhumiwa ameruhusiwa kukata rufaa kupinga kufanyiwa uchunguzi huo.

Waziri Mkuu Cameron ashtushwa kifo cha Mbunge


Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron naye pia ameshtushwa na tukio la mauaji ya mwanasiasa huyo akisema haya ni maafa makubwa na ni habari za kushitusha. Ametoa rambirambi kwa mume wa mawanasiasa huyo Brendan, watoto wake wawili na familia yake kwa ujumla. Cameron amesema Uingereza imempoteza mwanasiasa na mbunge ambaye alikuwa hodari katika masuala ya kampeni na akifanya hivyo kwa moyo wake wote na kuwa watu wameshitushwa na mauaji hayo.

Awali watu kadhaa waliokuwa na nyuso za majonzi walikusanyika nje ya jengo la bunge la nchi hiyo katika hafla ya kumkumbuka mwanasiasa huyo, tukio ambalo limehudhuriwa pia na kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn.

Cox ambaye alichaguliwa kuwa mbunge mwaka jana tayari alikuwa amejijengea umaarufu kutokana na jitihada zake za kuishawishi serikali ya nchi hiyo kufanya zaidi katika kuwasaidia wakimbizi wanaotokea nchini Syria na pia kampeni yake ya kuhamasisha Uingereza kuendelea kubakia katika Umoja wa Ulaya.

Kampeni za kura ya maoni zasimama Uingereza


Zikiwa zimesalia siku sita kabla ya kuitishwa kwa kura ya maoni pande zinazohasimiana ambazo zinapiga kampeni kuu nga mkono kujiondoa au kubaki kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya zilisimasha kampeni zake hizo na wanasiasa nao wameungana kupinga mauaji hayo.

Hata hivyo wachambuzi wamehoji iwapo muuaji anaweza kuchochewa na maudhui ya kampeni hizo ambazo zimekuwa zikiendelea ambazo zimeibua mvutano mkubwa kwa kugusia masuala ya kitambulisho cha kitaifa pamoja na masuala ya uhamiaji.

Gazeti la Times nchini humo limeripoti kuwa Cox ambaye anakuwa mbunge wa kwanza kuuawa tangu mwaka 1990 amekuwa akiandamwa na ujumbe wa vitisho uliotumwa kwake katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Kwa mujibu wa gazeti hilo polisi nchini humo walikuwa wakifikiria kuweka ulinzi wa ziada na kuongeza kuwa kulikuwa hakuna uhusiano na ujumbe huo uliotumwa na tukio hilo la mauaji hapo .

Aliyemuua mbunge Uingereza ni mgonjwa wa akili


Taifa la Uingereza limekumbwa na hali ya majonzi kufuatia kuuawa kwa mbunge mmoja kutoka katika chama cha upinzani nchini humo cha Labour Jo Cox .

Mbunge wa chama cha Labour Jo Cox aiyeuawa
Tayari taarifa kuhusu mshukiwa wa mauaji ya mbunge huyo, Thomas Mair, zimeanza kujitokeza. Kwa mujibu wa nduguye wa kiume, bwana huyo mwenye umri wa miaka 52, anatibiwa ugonjwa wa akili. Kituo kinachopinga ubaguzi nchini Marekani, Southern Poverty Law, kimesema mtuhumiwa huyo amekuwa akiliunga mkono kwa miaka kadhaa kundi la wanazi mambo leo la National Alliance na amewahi kulichangia kifedha. Kwa mujibu wa polisi, chanzo cha shambulio hilo bado hakijulikani.

Jo Cox , mwenye umri wa miaka 41 na ambaye amekuwa msitari wa mbele katika kampeni ya kuhamasisha Uingereza kuendelea kubaki katika Umoja wa Ulaya, aliuawa nje ya maktaba moja ambako mara nyingi amezoea kukutana na wananchi wa jimbo lake la uchaguzi katika kijiji anachotoka cha Birstall kilichoko kaskazini mwa Uingereza hapo jana tarehe 16,06,2016.

Mashahidi wa mkasa huo wanasema mwanasiasa huyo ambaye ni mama wa watoto wawili alipigwa risasi mara kadhaa na pia kuchomwa kisu.
Mmoja wa mashahidi wa tukio hilo Clarke Rothwell alisikika akisema kuwa mtu aliyehusika na mauaji hayo alisikika akipaza sauti kabla na baada ya tukio akisema " Uingereza kwanza "

Friday, 17 June 2016

Waziri Mkuu wa Brazil ajiuzulu kwa kashfa


Waziri wa utalii nchini Brazil,Henrique Alves amejiuzulu siku moja baada ya kushutumiwa kujihusisha katika kampeni zisizo halali za kujipatia fedha kutoka kwa wanyonyaji wakubwa wa rushwa wa taifa wa kampuni ya mafuta, Petrobras. Alves ni waziri wa tatu kujiuzulu katika wa utawala wa raisi Michel Temer ambaye yuko katika muhula wa serikali iliyojaa kashfa.
Waziri Alves akiwa bado anazipinga tuhuma hizo.
Jumatano ,mahakama kuu imetoa ushaidi kutoka kwa mmoja wa wakuu wa Pretrobas, Sergio Machado ambaye amewahusisha wanasiasa ishirini wenye majina makubwa akiwemo raisi Temer ambaye pia amepinga kuhusika kuwasaidia wanachama wa chama chake katika harakati hizo zisizo halali.

Watoto wapatao elfu 5 watumika Jeshini Somalia-UNICEF


Afisa mmoja mkuu na idara ya watoto ya umoja mataifa UNICEF, anasema takriban watoto elfu 5 wanatumiwa kama wanajeshi huko Somalia, pale Al shabab inapoendelea na kampeni zake za uandikishaji.

Katika mahojiano na idhaa ya kisomali ya sauti ya Amerika, Susannah Price, afisa mkuu wa mawasiliano wa UNICEF, alisema uandikishaji na utumiaji wa watoto kama wanajeshi umeorodheshwa na idadi yake inashtusha.

Anasema hali ni mbaya sana, takriban hadi watoto elfu 5 ni wanajeshi. Anasema tunajuwa kwamba Al Shabab ina kampeni ya kuandikisha watoto, mara nyengine kwa kutumia vishawishi huku wakiwapatia pesa au chakula. Watoto waliopo katika kambi za waliopoteza makazi wanalengwa zaidi na Al shabab.

Hapo siku za nyuma, inakadiriwa watoto elfu 2 hadi 3, wakiwa na umri mdogo wa hata miaka 9, waliandikishwa katika vikosi vya kijeshi vya Somali, hayo ni kwa mujib wa UNICEF.

Bi Price ametaka viongozi wa Somalia kutoa kipaumbele kwa ulinzi wa haki za watoto na kubuni mazingira salama kwa watoto wa Somalia

Thursday, 16 June 2016

Mauaji ya waandamanaji Ethiopia wanajeshi wahusika


Kundi la haki za binadamu linasema wanajeshi wa usalama wa Ethiopia yamewaua zaidi ya watu 400 toka mwezi Novemba katika kupambana na waandamanaji katika jimbo la Oromia.

Katika ripoti mpya iliyotolewa, kundi la Human Rights Watch linasema wanajeshi wakifyatua mara kwa mara risasi za moto kwa waandamanaji wa Oromia baada ya kutoa onyo hafifu ama kutotoa kabisa huku wakati mwingine wakijaribu kutumia njia na juhudi za kutawanya mkusanyiko bila kuhatarisha maisha.

Taarifa imeeleza kwamba wengi wa wale waliouwawa walikuwa wanafunzi ikijumuisha watoto walio chini ya miaka 18.

Kundi hilo la haki za binadamu pia limesema polisi wamewakamata watu elfu kumi toka maandamano yaanze, na wengi wanashikiliwa bila kushitakiwa ama bila kuwa na fursa ya wanasheria na wana familia.

CCM hawajang'ata meno badala yake wamemuuma Gwajima


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu wanahabari,

Bila ya shaka mmepata habari kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa siku ya Jumapili ya tarehe 11/06/2016 akiwa kanisani kwake, Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima alitoa kauli za uongo, uchochezi na uchonganishi dhidi ya Chama cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt John Pombe Magufuli, Viongozi wa CCM, Watendaji wa CCM na Serikali ya Awamu ya nne.

Mchungaji Gwajima amedai ati kwamba lipo kundi la wanaCCM wanaozunguka sehemu mbalimbali za nchi wakishawishi wanachama na wakimshawishi Mwenyekiti wa sasa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ili aendelee na Uenyekiti na kuleta hoja ya kutenganisha kofia ya Uenyekiti wa CCM na Urais wa nchi.

Napenda kuwafahamisha wana CCM, wapenzi wa CCM na wananchi kwa jumla kuwa madai hayo ya Mchungaji Gwajima ni uongo mtupu na hayana hata chembe ya ukweli. Ni mambo ya uzushi na hadithi ya kufikirika. Watu hao hawapo kwani kama wangekuwepo habari hizo zingekwishajulikana Chamani kupitia mfumo mahiri wa usalama na maadili wa ndani ya Chama cha Mapinduzi. Chama chenyewe kingekwishawatambua watu hao na kuwachukulia hatua zipasazo za udhibiti na nidhamu.

Kama mambo hayo yangekuwepo viongozi wa Chama wa Mikoa, Wilaya na Matawi waliofuatwa wangekuwa ndiyo wa kwanza kuwafichua. Habari za namna hiyo hazijapokelewa kutoka popote na kutoka kwa kiongozi yeyote wa Chama. Kama kweli Mchungaji Gwajima anawajua watu hao awataje hadharani na aseme walikwenda kumuona nani, wapi na lini kufikisha ujumbe wao huo hasi dhidi ya CCM.

Napenda kusisitiza kuwa habari za namna hiyo hazipo katika Chama cha Mapinduzi. Kwa hakika kinachoendelea sasa Mikoani na Wilayani ni maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum ambapo Mwenyekiti wa CCM wa sasa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atastaafu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli atachaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya. Hakuna jambo lingine.

Nafurahi kuwafahamisha Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwamba kazi ya maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum inakwenda vizuri kabisa. Shughuli hiyo inasimamiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara Ndugu Rajabu Luhwavi kwa niaba ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Kwa mujibu wa hatua iliyofikiwa sasa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa inaweza kukutana siku yoyote kupanga tarehe ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa uhakika.

Sisi katika Chama cha Mapinduzi hatushangazwi ingawaje tunasikitishwa na kauli za uongo, uchochezi na uchonganishi za Mchungaji Gwajima dhidi ya Chama cha Mapinduzi. Ana chuki iliyopitiliza dhidi ya CCM na Mwenyekiti wake. Yeye ni mtu ambae hajawahi kuitakia mema CCM. Hata yeye mwenyewe amekiri kwenye mahubiri yake ya tarehe 11 Juni, 2016 kuwa “alitaka CCM ishindwe katika chaguzi zilizopita na ndivyo anavyotaka iwe hivyo hata sasa, ili Chama chake cha upinzani kishinde.

Mchungaji Gwajima pia hana mapenzi na wala hamtakii mema Rais Dkt John Pombe Magufuli. Kwanza, hakutaka ashinde uchaguzi kwani alimpigania kwa hali na mali mgombea wa UKAWA. Pili, hataki adumu na kufanikiwa katika kazi yake ya Urais, ndiyo maana anatoa ushauri usiokuwa na mashiko na wakihasidi dhidi ya Mheshimiwa Rais. Anamshauri ati kwamba atoke Chama cha Mapinduzi na kuanzisha Chama chake. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais lazima awe mwanachama wa Chama fulani cha siasa. Hivyo basi, Rais John Pombe Magufuli akitoka CCM anapoteza Urais na Makamu wa Rais anakuwa Rais na CCM inaendelea kuongoza. Yeye atakuwa hana chake. Hivyo Rais wetu atakuwa amepata au atakuwa ameharibikiwa? Huo kweli ni ushauri wa mtu anayedai kuwa na mapenzi mema na Mheshimiwa John Magufuli? La hasha! Huo ni ushauri wa adui yake na wala siyo wa mtu rafiki na mwenye huruma na mapenzi na Rais wetu.

Mchungaji Gwajima anataka kufanya “danganya toto”. Napenda kumhakikishia yeye na genge lake kuwa “CCM hatudanganyiki na Rais Magufuli ndiyo kabisa “hadanganyiki.

JUKATA yamtaka Rais Magufuli atangaze marejeleo ya mchakato wa Katiba


Jukwaa la katiba Tanzania (JUKATA) limemtaka Rais Dk John Pombe Magufuli kulitangazaa taifa tarehe ya kurejea kwenye mchakato wa katiba mpya na namna ya kukamilisha hatua iliyobaki kuelekea kura ya maoni.
Hatua hizo ni pamoja na kuitishwa kwa mkutano mkuu wa kitaifa wa katiba ambao utalazimika kupitia maudhui ya katiba inayopendekezwa ikilinganishwa na rasilimali ya tume ya mabadiliko ya katiba kwa lengo la kuainisha malalamiko yanayotolewa na wananchi .
Mwenyekiti wa bodi ya Jukwaa la katiba Tanzania Deus Kibanda amewaambia waandishi wa habari wakati anatoa mapendekezo kwa serikali juu ya sheria zilizopitwa na wakati  ya mwaka 2011 na ile ya kura ya maoni ya 2013 ambayo imeendelea kutumika hadi leo bila ya kufanyiwa  marekebisho.
Aidha Bw. KIbamba ameeleza kuwa sababu kuu ya kufufua upya mjadala kuhusu mchakato wa katiba ni kutokana na uzoefu wa JUKATA kwenye michakato ya katiba duniani na hasa barani Afrika ambako viongozi wapya wanapoingia madarakani huwa na tabia ya kupuuza maswala yaliyoanzishwa na watangulizi wao na kujielekeza katika masuala wanayoamini yanafaa kwa kwa wananchi na utawala wao.

Bulgaria yajitoa NATO dhidi ya Urusi

Waziri mkuu wa Bulgaria amesema nchi yake haitojiunga na mpango maalum wa kijeshi uliopendekezwa na Jumuiya ya kujihami ya NATO wenye lengo la kuvikabili vikosi vya Urusi katika bahari nyeusi kwasababu nchi yake haiko tayari kuona vita katika eneo hilo. Tamko la Bulgaria limekuja siku moja baada ya Urusi kuonya dhidi ya hatua yoyote ya kuongeza uwepo wa kijeshi kwenye eneo hilo. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na rais Rosen Plevneliev, waziri mkuu Boiko Borisov amesema hataki kuona meli za kijeshi zikielea katika maeneo ya kitalii.Rais Plevneliev kwa upande wake ameitaja Bulgaria kuwa nchi ya amani. Mvutano kati ya Urusi na Jumuiya ya kujihami ya NATO umeongezeka na hasa  tangu ulipozuka mgogoro wa Ukraine pamoja na kudunguliwa ndege ya Uturuki mwezi Novemba.

Maandamano dhidi ya Ubaguzi wa rangi yafanyika Afrika Kusini


Afrika Kusini inaadhimisha miaka 40 tangu maandamano ya wanafunzi wa Soweto, walipopinga ubaguzi wa rangi katika elimu kwa kulazimishwa kusomeshwa kwa lugha ya Ki-Afrikaan.
Mamia ya wanafunzi walifariki katika vurugu zilizojiri wakati serikali ya ukoloni ya wazungu makaburu ilipotumia nguvu kupita kiasi, kujaribu kuzima maandamano hayo.
Maandamano hayo yalikuwa kama mwanzo wa kuelekea hatua za kumalizwa kwa utawala wa makaburu wa Afrika Kusini.
Makamu wa rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa, ameweka shada la maua kwenye kaburi la kijana Hector Pietersen.

Image caption
Afrika Kusini
Ni picha ya mwili wa kijana huyo uliokuwa unabebwa na mwanafunzi mwenzake baada ya kupigwa risasi na polisi.
Picha hiyo ilibua hamasa na hasira kubwa na kuufanya ulimwengu kulaani ukatili uliokuwa ukiendelezwa na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

Sheria dhidi ya Ugaidi yaidhinishwa Israel

Israel imepitisha sheria mpya ya kupambana na ugaidi ambayo serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na mrengo wa kulia ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu imesema inaimarisha mapambano dhidi ya ugaidi ingawa kwa upande mwingine wakosoaji wanasema sheria hiyo inakwenda kinyume na demokrasia.Kwa mujibu wa radio ya Israel miongoni mwa mambo mengine sheria hiyo inasema kwamba mtu atakayehukumiwa kifungo cha maisha  kwa kosa la ugaidi  hukumu yake hiyo haiwezi tena kupunguzwa katika kipindi cha miaka 15 ya mwanzo.Kadhalika kwa mara ya kwanza hatua ya kuchimba mahandaki imetajwa kama kosa la uhalifu chini ya sheria hiyo mpya.Sheria hiyo mpya ya kupambana na ugaidi Israel ilipendekezwa na chama cha kiyahudi cha siasa kali na imepitishwa na wabunge 57 na kupingwa na wabunge 16 katika bunge la Knesset lenye idadi jumla ya wabunge 120.

China yaipa onyo Marekani kuhusu Tibet


China imeionya Marekani kukoma kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake kwa kutumia suala la Tibet baada ya rais wa Marekani Barack Obama kukutana na kiongozi wa kiroho mwenye ushawishi mkubwa wa watu wa Tibet Dalai Lama katika ikulu ya Marekani. Onyo hilo la China limetolewa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Lu Kang.
Kadhalika wizara hiyo ya mambo ya nje ya China imesema kwamba njama zozote za kutaka kulitumia suala la Tibet kuingilia mambo ya ndani ya taifa hilo itahujumu usalama wa taifa hilo na mshikamano wa kimadhehebu hautofanikiwa.

Urusi kusitisha mapigano kwa saa 48 Syria

Urusi imetangaza katika dakika za mwisho usitishwaji mapigano kwa muda wa saa 48 katika mkoa ulioharibiwa vibaya na vita wa Aleppo hapo jana usiku ikiwa ni saa chache baada ya serikali ya Marekani kumuonya rais Bashar al Assad na mshirika wake huyo Urusi kwamba wanabidi waheshimu makubaliano ya kitaifa ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi Februari. Mkoa huo muhimu wa kaskazini mwa Syria wa Aleppo umekumbwa na mapigano makali na kuharibiwa kabisa katika vita vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 280,000. Taarifa za shirika linalofuatilia hali ya haki za binadamu la Syria lenye makao yake London Uingereza zinasema wapiganaji kadhaa wameuwawa katika mapigano mapya kati ya vikosi vya serikali, waasi na wapiganaji wa jihadi kusini mwa mji wa Aleppo jana. Hata hivyo tangazo la Urusi la kusitisha vita kwa siku mbili halikutoa ufafanuzi nchi hiyo imejadiliana na nani kuhusiana na hatua hiyo.