Saturday, 18 June 2016

Aliyemuua mbunge Uingereza ni mgonjwa wa akili


Taifa la Uingereza limekumbwa na hali ya majonzi kufuatia kuuawa kwa mbunge mmoja kutoka katika chama cha upinzani nchini humo cha Labour Jo Cox .

Mbunge wa chama cha Labour Jo Cox aiyeuawa
Tayari taarifa kuhusu mshukiwa wa mauaji ya mbunge huyo, Thomas Mair, zimeanza kujitokeza. Kwa mujibu wa nduguye wa kiume, bwana huyo mwenye umri wa miaka 52, anatibiwa ugonjwa wa akili. Kituo kinachopinga ubaguzi nchini Marekani, Southern Poverty Law, kimesema mtuhumiwa huyo amekuwa akiliunga mkono kwa miaka kadhaa kundi la wanazi mambo leo la National Alliance na amewahi kulichangia kifedha. Kwa mujibu wa polisi, chanzo cha shambulio hilo bado hakijulikani.

Jo Cox , mwenye umri wa miaka 41 na ambaye amekuwa msitari wa mbele katika kampeni ya kuhamasisha Uingereza kuendelea kubaki katika Umoja wa Ulaya, aliuawa nje ya maktaba moja ambako mara nyingi amezoea kukutana na wananchi wa jimbo lake la uchaguzi katika kijiji anachotoka cha Birstall kilichoko kaskazini mwa Uingereza hapo jana tarehe 16,06,2016.

Mashahidi wa mkasa huo wanasema mwanasiasa huyo ambaye ni mama wa watoto wawili alipigwa risasi mara kadhaa na pia kuchomwa kisu.
Mmoja wa mashahidi wa tukio hilo Clarke Rothwell alisikika akisema kuwa mtu aliyehusika na mauaji hayo alisikika akipaza sauti kabla na baada ya tukio akisema " Uingereza kwanza "

No comments:

Post a Comment