Showing posts with label Elimu. Show all posts
Showing posts with label Elimu. Show all posts

Sunday, 3 July 2016

Wanaojihusisha na Rushwa ya Ngono Vyuoni kitanzini


Umoja wa walimu, wanafunzi na wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu jijini Dar es Salaam, umekemea vitendo vya rushwa ya ngono vyuoni kwamba vinadhalilisha, kunyanyasa na kumuondolea binadamu heshima yake.

Walisema pia kuwa waathirika wa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono, wanaathirika kisaikolojia.

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Umoja wa kupambana na rushwa ya ngono vyuoni ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Colman Msoka baada ya semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia (GTI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Women Fund Tanzania.

Alisema kuwa rushwa ya ngono imekuwa ikisababisha magonjwa, vifo, mfarakano na kulipiziana kisasi.

Dk Msoka alisema kuwa vitendo hivyo pia vinasababisha watumishi hewa, wataalamu wabovu, utendaji kazi duni, nidhamu mbovu miongoni mwa wanafunzi, waajiri, walimu, wanafunzi na makundi mengine.

“Kushamiri kwa vitendo hivi vya rushwa ya ngono kunatokana na imani iliyopo kwa baadhi ya wanawake na wanaume kuwa na mafanikio yao yatapatikana kwa urahisi zaidi kwa kutoa rushwa ya ngono. Mafanikio hayo ni pamoja na kupata kazi, elimu, kufaulu mitihani au kupata fursa nyinginezo,’’alisema.

Mkoa wa Morogoro watekeleza agizo la Madawati kwa asilimia 93


SERIKALI ya mkoa wa Morogoro imefanikiwa kutengeneza madawati 217, 819 kati ya 233,816 yaliyokuwa yakihitajika kwa shule zote za msingi na sekondari zilizopo mkoani Morogoro.

Mkuu wa mkoa huo, Dk Kebwe Stephen alisema hayo juzi mara baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za mkoa huo walioteuliwa na Rais John Magufuli hivi karibuni.

Dk Kebwe alisema kati ya madawati yaliyotengenezwa ni 146,912 kwa shule za msingi sawa na asilimia 91 , wakati mahitaji ni 162,248, na katika wa shule za sekondari, madawati yaliyokamilishwa ni 70, 898 sawa na asilimia 99, wakati mahitaji yake ni 71,568 .

“Mpaka sasa mkoa umefanya vizuri kwa kufikisha asilimia 95 ya mahitaji kamili ya madawati na kuna madawati 5, 138 ya shule ya msingi na mengine 698 kwa shule za sekondari yanaendelea kutengenezwa kwa mafundi,” alisema.

Aliwataka wakuu wapya wa wilaya hizo kuhakikisha kuwa upungufu uliopo madawati katika halmashauri yakamilishwe ifikapo Julai 10, mwaka huu .

Aliwataka pia wakuu hao wa wilaya hizo kuhakikisha wanajipanga kutekeleza na kukamilisha agizo la ujenzi wa maabara, madarasa na vyoo katika shule ambazo zina upungufu kwenye maeneo yao.

Mkuu wa mkoa aliwataka kuhakikisha wanasimamia suala la mapato ya halmashauri ili yaongezeke na kuwezesha huduma bora kutolewa kwa wananchi, kupiga vita kwa vitendo na kuchukua hatua pale yanapojitokeza masuala ya ubadhirifu wa mali za umma, rushwa na uzembe kazini kwa watendaji wote waliopo chini ya wilaya zao.

Thursday, 30 June 2016

Bilioni 33 zatengwa kukarabati Shule kongwe 88 Tanzania Bara


Serikali ya Awamu ya Tano imetenga Sh bilioni 33 kwa ajili ya mpango maalum wa ukarabati mkubwa na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali, yakiwemo majengo ya madarasa, mabweni na nyumba za walimu katika shule kongwe za sekondari za serikali nchini.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango huo katika Shule ya Sekondari ya Mzumbe iliyopo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Profesa Ndalichako alisema mpango huo wa miaka miwili utahusisha shule kongwe 88 za serikali kwa kufanyiwa ukarabati mkubwa wa miundombinu, majengo ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni, majengo ya chakula na uboreshaji wa maabara na vitendea kazi vyake.

Waziri huyo alikuwa pia mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Elimu Tanzania iliyofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mzumbe na kuhudhuriwa na wadau wa sekta ya elimu wakiwemo wakuu wa shule za sekondari za serikali na maofisa elimu wa mikoa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Alisema utekelezaji wa mpango huo unatarajia kuanza wakati wotote baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali na kuanza kutumika na utaanza kwa awamu ya kwanza ambako shule kongwe 33 zitahusika.

“Tumekadiriwa kuwa kila shule itagharimu shilingi bilioni moja na kwa maana hiyo shule 33 zimeingizwa awamu ya kwanza. Fedha hiyo inaweza ikapungua kulingana na mazingira ya kitadhimini ya uchakavu wa majengo,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema uboreshaji wa elimu ni pamoja na ubora wa majengo na miundombinu mingine katika shule hizo, na lengo la kuzirejesha katika uhalisia wake wa zamani wa kuwa na mandhari nzuri za kuvutia wanafunzi, walimu na wazazi.

“Shule hizi tumeziweka katika mpango maalumu wa miaka miwili kukarabatiwa majengo yake, miundombinu ya kufundishia, vifaa vya kila somo, vitabu vya kufundishia na kujifunzia, vifaa vya kutosha vya maabara na kuboresha makazi ya walimu,” alifafanua Profesa Ndalichako.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais Tamisemi, Juma Kaponda, alimpongeza Waziri Ndalichako kwa kusimamia uboreshaji wa shule kongwe za sekondari na kuomba wadau mbalimbali waliosoma shule kongwe hizo na wanazo nyadhifa kubwa serikalini na sekta binafsi kuona wanao wajibu wa kuchangia maboresho hayo.

Thursday, 23 June 2016

Ubalozi wa Kuwait nchini watoa msaadawa madawati 300


Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa madawati 300 toka Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya kutatua tatizo la uhaba wa madawati katika shule za msingi hapa nchini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Maiga kwa niaba ya serikali alisema kuwa amesema kuwa kupokea madawati hayo ni sehemu ya kutekeleza wito wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

“Waziri Mkuu alitutaka sisi katika nafasi zetu tuwashirikishe wadau mbalimbali ili kuweza kutekeleza adhma ya serikali ya kutatua tatizo la wanafunzi kukaa chini ili waweze kupata mazingira bora ya kupata elimu, alisema Balozi Maige.
Balozi Maiga aliongeza kuwa Kuwait iko tayari kuisaidia nchi ya Tanzania kwa kuwajengea uwezo wataalam toka Tanzania kwa kuwapa elimu ya mafuta na gesi kwani Kuwait ina uzoefu mkubwa katika sekta ya mafuta na gesi.

Naye Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jaseem Al Najem alisema kuwa Serikali ya Kuwait itaendelea kutoa misaada kwa serikali ya Tanzania kadri itakavyowezekana pindi pale itakapohitajika.

Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (TUMa) Arusha chatoa milioni 10 kuchangia madawati


Shilingi milioni 10 zimetolewa na Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Makumira kilichopo wilayani Arumeru kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Wilson Nkambaku, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Joseph Parsalaw alisema ametoa msaada huo baada ya mkuu huyo wa wilaya kufika ofisini kwake na kuomba msaada kwa ajili ya madawati katika halmashauri hiyo.

Aidha, alisema chuo hicho siyo kwamba ni tajiri, lakini kimeona elimu ni jambo la msingi kwa watoto walioko shuleni, hivyo ni vyema wakapatiwa mahitaji ya lazima kama madawati ili waweze kusoma katika mazingira mazuri badala ya kukaa chini.

Akimshukuru mkuu huyo wa chuo baada ya kupokea fedha hizo mbele ya watumishi, mbunge na madiwani wa Halmashauri ya Meru, Nkambaku alisema alilazimika kuomba madawati wiki iliyopita kutokana na halmashauri hiyo kukabiliwa na ukosefu wa madawati.

“Agizo la Rais John Magufuli linataka watoto kusoma katika mazingira bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini ifikapo Juni 30 mwaka huu na katika wilaya yangu nimebakiza idadi ndogo ya madawati, ambayo nitaikamilisha kabla ya tarehe hiyo kwa kushirikiana na kamati nilizounda,” alisema.

Kwa mujibu wa Nkambaku, kiasi hicho cha fedha kitawezesha utengenezwaji wa madawati 200, ambapo yatapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya madawati inayohitajika.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru , Bakari Sajini alisema baada ya agizo la Rais, walifanya ukaguzi wa madawati katika shule zote za halmashauri hiyo na kubaini kuwa wana upungufu wa madawati 4,683. Alisema mpaka sasa wamekamilisha madawati 4,303 na wamebakiza madawati 380 pekee.

Mkurugenzi hiyo alitaja wadau wengine waliochangia madawati hayo kwa nyakati tofauti kuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Arusha iliyochangia Sh milioni 18, Chama Cha Mapinduzi (CCM) madawati 10, wakuu wa idara wa halmashauri ambao kila mmoja amechangia dawati moja na Mkuu wa Wilaya, Nkambaku ambaye amechangia madawati 10

Sunday, 19 June 2016

Mhe. Kikwete na changamoto za Elimu nchini


Jana Rais mstaafu, Mhe. Jakaya Kikwete alisema licha ya upatikanaji wa elimu ya msingi na sekondari ni bure, Serikali pekee haiwezi kutatua changamoto zilizopo.

Kikwete alisema hayo jana wakati wa matembezi ya hisani kwa ajili ya kuchangia gharama za elimu yanayoendeshwa na Taasisi ya Binti Foundation kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Kikwete, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Nne alisema mtoto anayeishi katika mazingira ya umaskini, elimu bure bado inakuwa ni changamoto kwake kwa ana mahitaji mengi ambayo mzazi anatakiwa ayagharamie ikiwamo chakula, sare za shule na mengine muhimu.

“Mtoto anayehudhuria masomo lakini nguo zake zimechanika, atakuwa darasani, hana furaha atabaki mnyonge tofauti na wenzake. Hapo atashindwa kuitumia ipasavyo haki yake ya msingi ya kupata elimu kutokana na mazingira anayoishi,” alisema.