Thursday, 23 June 2016

Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (TUMa) Arusha chatoa milioni 10 kuchangia madawati


Shilingi milioni 10 zimetolewa na Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Makumira kilichopo wilayani Arumeru kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Wilson Nkambaku, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Joseph Parsalaw alisema ametoa msaada huo baada ya mkuu huyo wa wilaya kufika ofisini kwake na kuomba msaada kwa ajili ya madawati katika halmashauri hiyo.

Aidha, alisema chuo hicho siyo kwamba ni tajiri, lakini kimeona elimu ni jambo la msingi kwa watoto walioko shuleni, hivyo ni vyema wakapatiwa mahitaji ya lazima kama madawati ili waweze kusoma katika mazingira mazuri badala ya kukaa chini.

Akimshukuru mkuu huyo wa chuo baada ya kupokea fedha hizo mbele ya watumishi, mbunge na madiwani wa Halmashauri ya Meru, Nkambaku alisema alilazimika kuomba madawati wiki iliyopita kutokana na halmashauri hiyo kukabiliwa na ukosefu wa madawati.

“Agizo la Rais John Magufuli linataka watoto kusoma katika mazingira bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini ifikapo Juni 30 mwaka huu na katika wilaya yangu nimebakiza idadi ndogo ya madawati, ambayo nitaikamilisha kabla ya tarehe hiyo kwa kushirikiana na kamati nilizounda,” alisema.

Kwa mujibu wa Nkambaku, kiasi hicho cha fedha kitawezesha utengenezwaji wa madawati 200, ambapo yatapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya madawati inayohitajika.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru , Bakari Sajini alisema baada ya agizo la Rais, walifanya ukaguzi wa madawati katika shule zote za halmashauri hiyo na kubaini kuwa wana upungufu wa madawati 4,683. Alisema mpaka sasa wamekamilisha madawati 4,303 na wamebakiza madawati 380 pekee.

Mkurugenzi hiyo alitaja wadau wengine waliochangia madawati hayo kwa nyakati tofauti kuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Arusha iliyochangia Sh milioni 18, Chama Cha Mapinduzi (CCM) madawati 10, wakuu wa idara wa halmashauri ambao kila mmoja amechangia dawati moja na Mkuu wa Wilaya, Nkambaku ambaye amechangia madawati 10

No comments:

Post a Comment