Sunday, 3 July 2016

Mkoa wa Morogoro watekeleza agizo la Madawati kwa asilimia 93


SERIKALI ya mkoa wa Morogoro imefanikiwa kutengeneza madawati 217, 819 kati ya 233,816 yaliyokuwa yakihitajika kwa shule zote za msingi na sekondari zilizopo mkoani Morogoro.

Mkuu wa mkoa huo, Dk Kebwe Stephen alisema hayo juzi mara baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za mkoa huo walioteuliwa na Rais John Magufuli hivi karibuni.

Dk Kebwe alisema kati ya madawati yaliyotengenezwa ni 146,912 kwa shule za msingi sawa na asilimia 91 , wakati mahitaji ni 162,248, na katika wa shule za sekondari, madawati yaliyokamilishwa ni 70, 898 sawa na asilimia 99, wakati mahitaji yake ni 71,568 .

“Mpaka sasa mkoa umefanya vizuri kwa kufikisha asilimia 95 ya mahitaji kamili ya madawati na kuna madawati 5, 138 ya shule ya msingi na mengine 698 kwa shule za sekondari yanaendelea kutengenezwa kwa mafundi,” alisema.

Aliwataka wakuu wapya wa wilaya hizo kuhakikisha kuwa upungufu uliopo madawati katika halmashauri yakamilishwe ifikapo Julai 10, mwaka huu .

Aliwataka pia wakuu hao wa wilaya hizo kuhakikisha wanajipanga kutekeleza na kukamilisha agizo la ujenzi wa maabara, madarasa na vyoo katika shule ambazo zina upungufu kwenye maeneo yao.

Mkuu wa mkoa aliwataka kuhakikisha wanasimamia suala la mapato ya halmashauri ili yaongezeke na kuwezesha huduma bora kutolewa kwa wananchi, kupiga vita kwa vitendo na kuchukua hatua pale yanapojitokeza masuala ya ubadhirifu wa mali za umma, rushwa na uzembe kazini kwa watendaji wote waliopo chini ya wilaya zao.

No comments:

Post a Comment