Sunday, 3 July 2016
BAVICHA wasema watauzuia Mkutano Mkuu wa CCM
Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limesema litazuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaotarajiwa kufanyika mwezi huu mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makamu mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi alisema Bavicha imeamua kuzuia mkutano huo kutokana na tamko la Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yote ya kisiasa.
“Tunaungana na tamko la Jeshi la Polisi, tunaungana na tamko la Rais John Magufuli pia hakuna mkutano wowote wa siasa unaotakiwa kufanyika, iweje CCM waandae mkutano huo, sisi vijana wa Chadema tutakuwepo pale Dodoma kuzuia mkutano huo,” alisema.
Ingawa Patrick hakufafanua ni njia zipi ambazo zitatumika kuzuia mkutano huo, lakini alisema watatumia njia halali kuhakikisha mkutano huo hautafanyika kama ambavyo mikutano ya vyama vingine imezuiliwa.
Jeshi la Polisi lilizuia kufanyika mikutano yote ya kisiasa, jambo ambalo lilipingwa na Chadema mahakamani kwa kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Katibu Mkuu wa Bavicha, Julias Mwita alisema vijana wa Chadema pia wanapinga tamko la Rais Magufuli la kuomba wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Rwanda, ili watoe mafunzo kwa watendaji wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) kwa lengo la kuhakikisha kila fedha inayokusanywa inaonekana katika mtandao.
Alisema Tanzania ina vijana wengi wasomi ambao wana utaalam katika mambo ya Tehama ambao hawana ajira, Rais anaweza kuwatumia kuliko kuchukua wataalam kutoka Rwanda.
Labels:
Habari za Kisiasa
Location:
Dodoma, Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment