Wednesday, 22 June 2016
Mashambulizi ya Boko Haram yasababisha chakula kukosekana Diffa, Niger
Wanamgambo wa kundi la Boko Haram, wamewalazimisha takriban watu laki 3 kutafuta hifadhi katika eneo la Diffa kusini mashariki mwa Niger, eneo ambalo tayari linakabiliana na ukosefu wa usalama wa chakula uliokithiri. Mashirika ya kutoa misaada yanahangaika kutoa maji ya kutosha na chakula kwa maelfu ya watu waliotoroka mashambulizi mapya katika mji wa mpakani wa Bosso mwezi huu.
Kila siku ni mlolongo mkubwa wa watu wanaoshikilia madebe ya manjano, katika mojawapo ya mifereji iliyopo huko Kidjendi, kambi iliyopo takriban kilomita 40 Kutoka Diffa, kusini mashariki mwa Niger.
Cheldou Malou anaishi katika kambi na wanafamilia wake saba, anasema, kuna watu wengi. "Mara nyengine wanaleta madebe mawili lakini wanajaza moja tuu. Ninakuja asubuhi, lakini sipati maji ya kutosha kwa hivyo nnarejea mchana."
Malou na familia yake ni miongoni mwa watu takriban elfu 50 waliotoroka eneo karibu na mji wa mpakani wa Bosso, kufuatia shambulizi la Boko Haram hapo Juni 3.
Wengi waliacha kila kitu nyuma na kutembea kwa siku kadhaa kabla kukusanyika katika kambi jangwani. Walijenga makazi kwa kutumia mikeka ya majani na plastiki zilizogawiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali. Makazi hayo yako hatarini kupeperuka kila mara upepo unapovuma.
Watu waliopoteza makazi huko Diffa Niger, wakisali chini ya makazi yalotengenezwa na majani.
Kidjendi pekee ina wakimbizi takriban elfu 40, na watu walopoteza makazi.
Mkuu wa shirika la madaktari wasio na mipaka kitengo cha Uhispania huko Niger, Elmounzer Ag Jiddou, anasema hakuna maji ya kutosha. Jiddou anasema, hali walio nayo kwa wakati huu inaweza kusababisha mizozo kwa sababu idadi ya maji wanaopata haitoshi, hasa kutokana na hali ya joto iliopo.
Siku chache zilizopita, mapigano kwenye kisima huko Kidjendi, yalipelekea mtu mmoja kufariki.
Baadhi ya wakulima waliopoteza makazi waliweza kutoroka na mifugo yao, na sasa, ngombe na punda wanasambaa kwenye kambi pia ni chanzo cha mivutano.
Chakula nacho kiko haba:
Yamgana Goni mkimbizi hapo Kidjendi alisema hakuna chakula wala makazi. Anasema, hamna chochote, na ana hofu wanawe 9 watakufa na njaa. Wafanyakazi wa kutoa misaada wanasema chanzo cha kutoa msaada bora ni kuwepo kwa usalama.
Lakini licha ya ongezeko la kijeshi, Boko Haram linaendelea kufanya mashambulizi ya hapa na pale katika eneo hilo, na hivyo watu wanaendela kuhama hama, na hivyo kufanya ugawaji wa misaada kuwa kugumu.
Diffa tayari ilikuwa na wakimbizi elfu 240 na na watu waliopoteza makazi, pale mji wa Bosso uliposhambuliwa.
Mashirika ya kutoa misaada yanaonya kuwa mizozo ya kibinadamu huenda ikaendelea katika eneo hilo kote katika eneo la ziwa Chad.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment