Wednesday, 22 June 2016

Yanga SC Uturuki kuna nini?


TIMU ya soka ya Yanga imerejea tena Uturuki kuweka kambi kujiandaa na mchezo wake wa pili Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) dhidi ya TP Mazembe wiki ijayo.

Yanga ilianza vibaya michuano hiyo baada ya mwishoni mwa wiki kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini kutoka kwa Mo Bejaia ya nchini Algeria.

Awali Yanga iliweka kambi ya wiki moja nchini Uturuki kabla ya kumenyana na Mo Bejaia ya Algeria, ambapo baadaye ilisema ingerejea nchini jana.

Hata hivyo jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdetit aliliambia gazeti hili kuwa wameamua timu hiyo irejee Uturuki ili ipate muda mzuri wa kujiandaa na kwamba itarejea nchini siku mbili kabla ya mchezo wao na TP Mazembe ambao utachezwa Juni 28 mwaka huu.

“Tunaamini kambi ya Uturuki itawezesha timu yetu kufanya vyema kwenye mchezo wa pili, Mwalimu Hans Pluijm anaendelea na mazoezi na wachezaji na mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo na Mo Bejaia anaendelea kuyafanyia kazi, ”alisema Deusdetit.

Naye Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema timu hiyo imeendelea na mazoezi mepesi jana asubuhi .

“Mazoezi tunaendelea nayo, wachezaji walikimbia asubuhi alfajiri ili kutafuta pumzi za kutosha,” alisema.

Akizungumzia suala la hewa ya Uturuki, Meneja huyo alisema hali ya hewa ya nchi kwa sasa inaendana na ya Dar es Salaam.

“Hakuna baridi kali, hali ya hewa kama Dar es Salaam, tunashukuru mazoezi yanaendelea vizuri na timu itakuwa kwenye kiwango kizuri kwa kuwa hali ya hewa ya huku inashabihiana na ya huko Dar es Salaam, ”alisema.

No comments:

Post a Comment