Wednesday, 22 June 2016

Zaidi ya Wanajeshi 30 wa Libya wauawa

Karibu wanajeshi 34 wanaounga mkono serikali ya Libya waliuawa jana na wengine 100 wakajeruhiwa katika makabiliano na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS wakati wakijiandaa kwa shambulizi la mwisho katika ngome ya wanamgambo hao ya Sirte.

Ilikuwa mojawapo ya siku za umwagaji damu mkubwa tangu majeshi yanayoitii serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli kuanzisha operesheni ya mashambulizi mwezi Mei ili kuukomboa mji wa Sirte kutoka kwa IS.

Watu 29 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mji wa magharibi wa Garabulli kufuatia mlipuko ndani ya ghala ya silaha baada ya wapiganaji na wakaazi wenye silaha kukabiliana.

Kuanguka mji wa Sirte kunaweza kuwa pigo kubwa kwa IS ambayo imekumbwa na hasara kubwa Syria na Iraq ambako majeshi ya nchi hizo na majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani yanaendesha operesheni ya mashambulizi katika ngome zao.

No comments:

Post a Comment