Wednesday, 22 June 2016

Korea Kaskazini yafyatua upya makombora yake

Taarifa kutoka Korea ya Kusini zinasema, Korea ya Kaskazini imefyatua makombora mawili hii leo. Kama ilivyokuwa kwa kombora la mwanzo, na la pili pia lilifyatuliwa saa chache baadaye, katika mwambao wa mashariki wa nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Korea ya Kusini amesema hayo mjini Seoul. Jeshi la Korea ya Kusini linakadiria kombora la mwanzo kufyetuliwa lilikuwa la masafa ya wastani - chapa Musudan. Jeshi la Marekani pia limethibitisha ripoti hiyo.

Kabla ya hapo Japan ililiweka jeshi lake katika hali ya tahadhari kufuatia onyo Korea ya Kaskazini huenda ikaanza kufyatua makombora. Vyombo vya habari vya Japan vimeripoti pia kwamba jeshi la wanamaji limepewa amri ya kuliangusha kombora lolote litakalopita katika anga ya nchi hiyo.

Korea ya Kaskazini inatengeneza makombora ya masafa ya wastani na masafa marefu yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezidisha makali ya vikwazo dhidi ya Pyongayang mapema mwezi wa Machi mwaka huu.

No comments:

Post a Comment