Tuesday, 21 June 2016

Hatima ya Bemba kujulikana leo

Majaji katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague leo watatoa hukumu kwa mbabe wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Jean-Pierre Bemba, katika kesi ambayo waendesha mashitaka wanataka hukumu ya kifungo cha miaka isiyopungua 25.

Endapo majaji wataridhiana na upande wa waendesha mashitaka, hukumu hiyo itakuwa ya kifungo cha muda mrefu gerezani kuwahi kutolewa na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa katika kesi ambayo kwa mara ya kwanza imelenga ubakaji kama silaha ya vita.

Waendesha mashtaka hao wanamlaumu Makamu huyo wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kufumbia macho vitendo viovu vilivyofanywa na vikosi vyake katika ardhi ya Jamhuri ya Afrika Kati kuanzia Oktoba 2002 hadi Mei 2003.

Bemba alipatikana na hatia mwezi Machi, iliyohusisha mashitaka matano ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu, baada ya kuwapeleka wanajeshi 1,500 kutoka katika jeshi lake binafsi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati katika jitihada za kuzima mapinduzi dhidi ya mtawala wa wakati huo.

No comments:

Post a Comment