
Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine nchini Tanzania wanapanga kuwatuma panya waliopokea
mafunzo kwenda kutumiwa kugundua kifua kikuu nchi za nje.
Panya hao, ambao kiteknolojia hujulikana kama panya wa SUA-APOPO, wamebainika kuwa hugundua visa vya maambukizi ya kifua kikuu haraka na kwa ufasaha.
Panya hao hudaiwa kuwa na uwezo wa kupima sampuli 140 za makohozi kwa dakika 15 tu, wakati mtaalamu wa maabara aliyebobea huweza kupima wagonjwa 25 kwa siku.
Awali, walitumiwa Tanzania na Msumbiji pekee.
Lakini sasa chuo kikuu hicho kinapanga kuwapeleka Ethiopia na Bangladesh wakatumiwe huko.
Ethiopia ni moja ya nchi zilizotatizwa zaidi na aina ya vijidudu vya kifua kikuu visivyosikia dawa.
Bi Mariam Juma, mmoja wa wanasayansi katika chuo hicho, amenukuliwa na gazeti la Daily News la Tanzania akisema kwamba kutafunguliwa pia kituo jijini Dar es Salaam.
Akihutubia wanahabari katika maonesho ya biashara ya Dar es Salaam, Bi Juma alisema maafisa pia watawahimiza watu kujipima kujua hali yao.
No comments:
Post a Comment