Monday, 4 July 2016

Mfuko wa Rais wataka kujiendesha


Bodi ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) imeiomba Serikali kuupatia Sh4 bilioni kwa ajili ya kuufufua na kuuendeleza kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye mpango wake wa miaka mitano.

Kauli hiyo imetolewa leo na mwenyekiti mpya wa Bodi, Nattu Msuya akibainisha endapo watapewa fungu hilo, PTF itaweza kujitegemea badala ya kutegemea Serikali.

Tangu kuanzishwa kwa Bodi hiyo Oktoba 2015 hadi Juni 30, 2016  mfuko huo umeshakopesha vijana 114 na wanawake 399 Sh479 milioni.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa PTF, Haighat Kitala amesema tangu kuanzishwa kwake, mfuko huo  una akiba ya Sh1.8 bilioni kama mtaji huku ukiwa unadai Sh600 milioni zilizokopeshwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki ameahidi kushughulikia ombi hilo ili kuona jinsi gani Serikali inaweza kuisaidia PTF iweze kujiendesha.

No comments:

Post a Comment