Saturday, 25 June 2016

U.K huenda ikavunjika endapo Scotland watajiondoa baada ya Uingereza kujitoa EU


Waziri Kiongozi wa Scotland, Nicola Sturgeon, amesema kuna uwezakano mkubwa wa kuitishwa kwa kura nyengine ya maoni ya kujiondoa kwenye muungano na Uingereza, siku moja baada ya Waingereza kuamua kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Sturgeon amewaambia waandishi wa habari mjini Edinburgh, kwamba kuna hatari ya Scotland kuondolewa kwenye Umoja wa Ulaya, ambako inataka kubakia, jambo ambalo halikubaliki.

Asilimia 62 ya wapigakura wa Scotland, ambayo ni nchi ndani ya Muungano wa Uingereza, waliamua kusalia kwenye Umoja wa Ulaya kwenye kura ya maoni ya hapo jana.

Lakini kura ya jumla, imetoa ushindi kwa kundi la wanaotaka kujitoa kwa asilimia 52 dhidi ya 48.

Kwenye kura ya mwaka 2014, Scotland ilishindwa kujitangazia uhuru kutoka Uingereza baada ya asilimia 55 kuamua kusalia kwenye muungano huo wa miaka 300.

Kampeni kubwa ya waliotaka Scotland isalie kwenye Muungano wakati huo ilikuwa ni manufaa ya kiuchumi inayoyapata Scotland kwenye Umoja wa Ulaya kupitia Muungano wake na Uingereza.

No comments:

Post a Comment