Sunday, 26 June 2016

Rais Magufuli aja na mbinu mpya kisiasa


Rais John Magufuli, jana alitoa staili mpya ya kuwaalika wanasiasa kuanza kuzungumza kabla yake.

Hiyo ilitokea jana wilayani Kinondoni alikokwenda kwa ajili ya uzinduzi wa Mpango wa Jeshi la Polisi wa kuboresha usalama wa jamii.

Mh. Magufuli ambaye alifika uwanjani hapo saa 4:43 asubuhi, kabla ya kuanza kuzungumza aliwaalika wanasiasa mbalimbali kusema chochote kwa maelezo kuwa suala la ulinzi na usalama si la vyama.

Walioitwa ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni (Chadema), Boniface Jacob ambaye hakuwapo katika eneo hilo na Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa.

Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na Diwani wa Kata ya Kinondoni (Chadema), Mustafa Muro.

“Mstahiki Meya wa Kinondoni yuko wapi? Hayupo, sasa Jacob yeye ujambazi anautaka tu,” alihoji Rais Magufuli.

Hata hivyo, Meya Jacob baadaye alilieleza gazeti la Mwananchi  kuwa hakualikwa na badala yake alitakiwa kuteua madiwani watano kutoka Kamati ya Fedha kuhudhuria hafla hiyo na kusisitiza kwamba haungi mkono ujambazi na uhalifu.

Akisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha anatekeleza ahadi zake, Rais Magufuli amesema lengo lake ni kutowaangusha wananchi na amedhamiria kuijenga nchi kwa nguvu zote huku akirejea kauli yake ya kuwataka wananchi wamuombee.

“Nawaomba wananchi mniache nitekeleze ahadi zangu kwa Watanzania wote. Yapo aliyoahidi diwani wa Chadema aachwe ayatekeleze. Watu wa CCM wasimsumbue,” alisema.

No comments:

Post a Comment