Ndege za kivita za Urusi na zile za Syria zilifanya mashambulizi ya anga katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi katika mji wa Allepo nchini Syria hapo jana. Kundi la waangalizi limethibitisha.
Mwakilishi wa shirika la habari la AFP katika eneo la mashariki mwa mji huo linalodhibitiwa na waasi alisema mashambulizi hayo yalidumu usiku kucha hadi asubuhi.
Mji wa Allepo ambao ulikuwa ni kitovu cha biashara na uzalishaji kabla ya kuibuka kwa mgogoro nchini humo mnamo mwaka 2011 uligeuka kuwa uwanja wa mapambano tangu pale waasi nchini humo walipofanikiwa kudhibiti eneo la upande wa mashariki mwa mji huo mwaka mmoja baada ya kuibuka kwa mgogoro huo.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa siku mbili yaliyokuwa yamefikiwa na Urusi pamoja na Marekani mapema mwezi huu yamemalizika pasipo kuongezewa muda huku Urusi ikisema itaendeleza mashambulizi yake nchini humo kufuatia upande wa waasi kutotekeleza ahadi yake ya kutojihusisha na wafuasi wa kundi la itikadi kali la Al-Qaeda.
No comments:
Post a Comment