Saturday, 18 June 2016
Mkuu wa Mkoa Mwanza akabidhiwa gari la wagonjwa
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amepokea gari la Wagonjwa kutoka kwa Sargical Rafiki Mission kwaajili ya kuhudumia wananchi wa mkoa huo ambalo amelikabidhi kwa uongozi wa hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure na kuwataka kuitunza kwa maslahi mapana ya wananchi wa mkoa huo.
Akizungumza kabla ya kupokea gari hilo mkuu huyo wa mkoa amesema, msaada walioupokea kutoka kwa Rafiki Mission ni masaada wa kupigiwa mfano kwa kuwa watu wengi wanabarikiwa vitu vingi lakini suala la kutoa misaada wameshindwa.
Mongella amesema kama Mkoa ukipata marafiki wa aina ya Rafiki hawana budi kuwang’ang’ania wasiondoke kwenye himaya yao.
“Nafahamu hata sisi tunabarikiwa sana lakini hata siku moja hakuna mtu aliwahi kuleta hata mkasi, hivyo lazima tufahamu kutoa ni moyo na sio utajiri."
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema, karibu asilimia tisini ya matatizo ya afya yanayoikabili jamii ya kitanzania yamejikita katika suala la afya ya mama na mtoto ambayo kama taifa tukifanikiwa kuwekeza katika hili, basi matatizo mengine ya afya yataondoka yenyewe.
"Najua suala la mama na mtoto ni tatizo mtambuka kwa taifa, hivyo tukiwekeza zaidi katika afya ya mama na mtoto tutakuwa tumekabili changamoto kubwa ya masuala ya afya na itawawezesha wananchi kujikita katika shughuli za maendeleo”, alisema Mongella
Awali akitoa Salam za Rafiki Mission, Balozi Issaya Chialo, alisema wao kama Rafiki Mission, wanatambua matatizo yanayoikabili jamii ya kitanzania hususan masuala ya afya, na kwamba wao kama Rafiki Surgical Mission, hawana ubaguzi katika utoaji wa misaada kwa jamii nzima ya kitanzania.
“Mkuu wa mkoa sisi shughuli zetu zipo katika mkoa wa Mtwara tukijikita katika zaidi katika utafutaji wa mafuta na Gesi, lakini hiyo haituzuii sisi kupeleka misaada pembe zingine za nchi na ndio maana leo tupo katika mkoa wako wa Mwanza” alisema Balozi Chialo na kuongeza kuwa wanajisikia fahari katika hili.
Chialo ameutaka uongozi wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure kulitunza gari hilo la wagonjwa lenye thamani ya Mil. 40, ambalo litasaidia katika kuwakimbiza wagonjwa wenye mahitaji maalum sehemu mbali mbali za mkoa huo na mikoa ya jirani.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Subi amesema hivi sasa hospitali ya mkoa huo inakabiliwa na changamoto ya chumba cha kutolea huduma ya upasuaji kwa akina mama, ambapo mkuu wa mkoa amemtaka Mganga huyo wa mkoa kutenga kiasi cha Mil. 5 kutoka katika makusanyo ya ndani ya hospitali ya mkoa huo na Mkuu wa mkoa kupitia wadau wa maendeleo atahakikisaha kiasi kingine cha fedha kinacho salia kinapatikana kwa ajili ya ukarabati wa chumba hicho ambacho kinahitaji Mil.20 ili kiweze kufanya kazi ya upasuaji kwa akina mama.
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure, imekuwa msaada kwa wagonjwa wa mkoa huo na mikoa ya jirani kutokana na huduma zake kuwa nzuri na madaktari mabingwa wanaopatikana katika mkoa huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment