Saturday, 25 June 2016
Jaji Mkuu asishauriane na Rais
Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imepinga pendekezo la Rais kushauriana na Jaji Mkuu katika kuanzisha Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi, ikieleza kuwa hatua hiyo ni kuingilia mhimili wa Mahakama.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa licha ya kupongeza hatua ya Serikali kuanzisha divisheni hiyo alisema kamati yake haioni mantiki ya Rais kuingilia mamlaka ya Jaji Mkuu katika kuanzisha mahakama hiyo.
Katika marekebisho ya Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria, Sura 358 yaliyowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, kifungu kipya 4A kinamwezesha Jaji Mkuu kuanzisha mahakama hiyo lakini kwa kushauriana na Rais.
“Kamati imebaki na msimamo wake na kuendelea kuitaka Serikali kuwa uhuru wa Mahakama usiingiliwe na mihimili mingine. Ni vyema Jaji Mkuu akabaki na mamlaka yake ya kuunda divisheni za Mahakama pasipo kuingiliwa na Rais,” alisema Mchengerwa.
Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe, alisema kuna umuhimu wa kutenganisha mihimili ya Dola na kumpa Jaji Mkuu haki ya kujiamulia mwenyewe mambo yanayohusu Mahakama.
Bashe pia alieleza kuwa uamuzi wa Serikali kuwa kesi zitakazosikilizwa na Mahakama hiyo kuanzia Sh1 bilioni ni kikubwa.
Alisema ukitazama ufisadi pamoja na uwepo wa rushwa kubwa kuna rushwa za kati zinazoiathiri Serikali Kuu na wananchi wengi.
Naishauri Serikali kupunguza kiasi hiki cha fedha hadi kufikia Sh100 milioni,” alisema.
Alisema dhana kubwa ya kupambana na rushwa ambayo ndiyo iliyofanya kuanzishwa kwa divisheni hiyo itapotea na pia itaruhusu baadhi ya watu kucheza na kiasi kwa kuhakikisha wanakuwa na mashtaka yasiyofikia kiwango hicho cha Sh1 bilioni.
Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba, alipongeza hatua ya Serikali kuweka kiwango hicho cha fedha kwa sababu kingekuwa kiwango cha chini kingepunguza maana ya kuanzishwa kwa divisheni hiyo.
“Kwa kuweka Sh1 bilioni maana yake sasa tumeamua kupambana na rushwa kubwa,” alisema.
Pia, alisema suala la kuipa nguvu ya kisiasa divisheni hiyo kwa kuhakikisha inaanzia kwa Rais hadi ngazi ya chini si jambo baya.
“Hii ni kuonyesha kuwa hii vita tupo katika gari moja tunataka kupambana na rushwa kwa hiyo Rais kushirikishwa si jambo baya,” alisema.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema haoni mantiki katika madai ya baadhi ya wabunge kuwa Jaji Mkuu kushauriana na Rais ni kuingilia muhimili mwingine.
“Kuwasiliana na kiongozi mwenzake wa muhimili mwingine ambaye ndiye anayetafuta pesa kuna tatizo gani? Hakuwezi kuwa ni kuingilia muhimili mwingine,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Katiba, Rais ndiye mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amri Jeshi Mkuu hivyo anapaswa kufahamu.
Akijibu hoja hizo wakati wa kuchangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2016, Masaju alisema kuna kesi nyingi za ufisadi zinazozidi thamani ya Sh1 Bilioni na kutosha kusikilizwa na Divisheni ya Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi.
Masaju alisema mapendekezo ya muswada huo yameletwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Na hawa ndio wapo kwenye tasnia hii, wanajua hiki kitu ambacho miaka mingi tumekuwa tukisema. Haya makesi yanayofikia Sh1 bilioni na kuendelea yapo ya kutosha,” alisema.
Masaju alisema Mahakama hiyo pia inatoa fursa kusikiliza makosa mengine ambayo katika uhalisia wake hayawezi kukadiriwa kwa kiasi hicho cha fedha.
Alisema kuna kifungu kwenye muswada huo ambacho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika masuala yenye masilahi kwa umma hata yale ambayo hayajafikia kiwango hicho na yale yasiyo ya uhujumu uchumi kupelekwa kwenye mahakama hiyo.
Alisema mambo mengine yanaibuka na mawaziri ndiyo wenye nafasi ya kujua mahitaji ya wananchi kutokana na kukutana na wananchi kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye mikutano ya hadhara.
Masaju alisema kushauriana na waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria hakuwezi kumaanishwa kuwa ni kuingilia muhimili mwingine. Mjadala huo uliahirishwa hadi Jumatatu.
Labels:
Habari za Kisiasa
Location:
Dodoma, Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment