Thursday, 30 June 2016

Dr. Besigye kutinga Mahakamani bila Mawakili wake


Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani nchini Uganda, Dr. Kizza Besigye, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini, Jana alipandishwa tena kizimbani kwenye mahakama ya Uganda, ambapo alijiwakilisha mwenyewe bila ya mawakili wake.

Besigye ambaye toka kushikiliwa kwake ameshapandishwa kizimbani kwenye mahakama kadhaa za Uganda, kwenye maeneo tofauti tofauti ya nchi, hali ambayo mawakili wake wanasema wanashindwa kumuwakilisha vema.

Besigye alitarajiwa kupanda kizimbani bila kuwa na mawakili wake, katika kile alichosema ni hujuma zinazofanywa dhidi yake kuhakikisha anakosa wawakilishi muhimu kwenye kesi ambayo ameendelea kusisitiza kuwa imepikwa kisiasa kummaliza.

Mmoja wa mawakili wake, Yusuf Nsibambi, amesema wao kama wataalam wa sheria wanashindwa kumuwakilisha Besigye inavyopaswa kutokana na kutokuwepo kwa mahakama moja inayosikiliza kesi yake, na kwamba wanaona ni kama tayari ameshahukumiwa kuliko madai ya Serikali kuwa anashtakiwa.

Wafuasi wa Besigye, wanaharakti pamoja na wanasiasa wengine nchini Uganda, wamekosoa namna kesi hiyo inavyoendeshwa wakisema siasa imeingia hadi kwenye mfumo wa kimahakama, kwa kuwa kiongozi huyo hapati haki yake kisheria kama inavyotamkwa kwenye katiba ya nchi.

Besigye mwenyewe ameendelea kushikilia msimamo wa kujiwakilisha mwenyewe kwa kile anachosema ni kudai haki yake popote pale atakaposomewa mashtaka hata kama sio kwenye mahakama moja inayofahamika.

No comments:

Post a Comment