Thursday, 30 June 2016
Zanzibar kupata Nishati ya uhakika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imeweka malengo ifikapo mwaka 2020 itahakikisha vijiji vyote vya Unguja na Pemba vinapata huduma ya nishati ya uhakika ya umeme.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira, Juma Makungu Juma, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Ole, Said Omar Mjaka aliyetaka kufahamu lini huduma ya nishati ya umeme zitapatikana Zanzibar.
Juma alisema kwa sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kusambaza huduma ya nishati ya umeme kwa asilimia 86 kwa wananchi wake wa Unguja na Pemba.
Alisema mafanikio hayo yamekuja zaidi baada ya kisiwa cha Pemba kuunganishwa na Gridi ya Taifa kutoka Tanga kwa msaada mkubwa wa Serikali ya Norway.
“Mheshimiwa Spika napenda kulijulisha Baraza la Wawakilishi kwamba katika kipindi cha miaka minne ijayo visiwa vya Unguja na Pemba vitakuwa vimefaidika na huduma za usambazaji wa nishati ya umeme,” alisema Naibu Waziri.
Alisema kwamba matumizi ya nishati ya umeme faida zake ni kubwa ambapo katika baadhi ya vijiji vimefanikiwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Alisema serikali ipo katika hatua za mwisho za kusambaza huduma ya umeme katika baadhi ya visiwa wanavyoishi wananchi huko Pemba.
Labels:
Habari za Kisiasa
Location:
Zanzibar, Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment