Friday, 24 June 2016

Ushirikina wakimbiza walimu Dodoma


Walimu katika shule ya msingi Tinai wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, wanadaiwa kuondoka shuleni hapo kwa hofu ya vitendo vya kishirikina.

Inadaiwa katika tukio la karibuni, mwalimu mmoja alipata upofu akifundisha na mwingine alishambuliwa na bundi na kupambana naye.

Mwenyekiti wa kijiji cha Tinai, Josiah Chitau alitoa taarifa hiyo kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Francis Mwonga.

Alisema tukio la kwanza, mwalimu wa shule hiyo aliyemtaja kwa jina la Chibuga akiwa anafundisha darasani, ghafla alikumbwa na kutoona kabla ya kupelekwa ofisi ya walimu ambako alianza kuona tena.

Katika tukio la pili, Mwenyekiti wa Kijiji alimtaja mwalimu aliyejulikana kwa jina la Kwimba kwamba alipambana na bundi aliyeingia chumbani kwake na kuanza kumshambulia.

“Wananchi walifanikiwa kumkamata bundi wakamuua na kuamua kumchoma moto, lakini akiwa bado anaungua ghafla mbwa ambaye hajulikani alitokea wapi, akamchukua bundi na kutokomea kusikojulikana,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa kijiji alisema pia wanafunzi shuleni hapo walikuwa wakiona vitu visivyotambulika ambavyo vilihusishwa na ushirikina. Alisema mpaka sasa walimu wawili, Chibuga na Kwimba wamekimbia shuleni na wengine wanadai wako mbioni kuondoka.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Shadrack Chimale ambaye alidai amekaa shuleni hapo kwa miaka 20, alisema pia anataka kuondoka shuleni hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Francis Mwonga aliwataka wazee wa kimila kukutana, kujadili namna ya kutatua tatizo hilo. Pia aliwataka viongozi wa dini kila mmoja kwa nafasi yake, kukemea vitendo hivyo na kusema matukio hayo yanadumaza elimu. Alisema haikubaliki kuona walimu wanakimbia kutokana na sababu za ushirikina.

“Ushirikina ni doa, suala hilo lishughulikiwe, kuwaita lambalamba ni kinyume cha sheria, kinachotakiwa ni maendeleo, jicho la pili la serikali ni kushughulikia maendeleo ya wananchi wake,” alisema na kusisitiza umuhimu wa wananchi kumrudia Mungu.

No comments:

Post a Comment