Friday, 24 June 2016

Rais Paul Kagame kuizuru Tanzania


Rais Paul Kagame anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania Julai 1 kwa mwaliko wa mwenzake wa Tanzania, Rais John Pombe Magufuli.

Katika ziara hiyo Rais Paul Kagame atafungua mkutano wa kimataifa wa 40 wa wafanya biashara, Dar es Salaam International Trade Fair (DITF) na kufanya mazungumzo yenye lengo la kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, rais wa Rwanda atafanya ziara ya kikazi nchini Tanzania baada ya kualikwa na mwenziye wa Tanzania, Rais John Magufuli.

Wakati wa ziara hiyo, Bw Kagame na ujumbe wake wanatarajiwa kutia saini Mkataba wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili (MoU), ambo ulikamilishwa na kamati ya pamoja ya wataalam kutoka nchi zote mbili.

Nchi hizi mbili jirani, mwezi uliopita, zilikubaliana kuunda kamati ya pamoja ya utekelezaji (JIC) itakayofuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi muhimu, wakati wa kikao cha 14 cha Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC).

Kamati hii ilikubaliana kuimarisha mahusiano baina ya nchi katika sekta mbalimbali muhimu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano katika sekta ya usafiri wa anga, hasa kati ya mashirika ya ndege ya nchi hizi mbili, Rwandair na Air Tanzania.

Katika mkutano huo pia walikubaliana kuboresha miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara itakayounganisha nchi tatu ambazo ni Burundi, Uganda, na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) .

Mambo mengine ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ni pamoja na kuongeza kasi kwa ujenzi wa reli utakaogharimu trilioni kadhaa za Shilingi ya Tanzania.

Itafahamika kwamba Rais Paul Kagame atakua rais wa pili kutembelea Tanzania, toka Rais John Pombe Magufuli achukue hatamu ya uongozi wa nchi, baada ya Rais wa Vietnam, Truong Tan Sang.

No comments:

Post a Comment