Tuesday, 21 June 2016
Mwingine tena Kizimbani Dar kwa kumdhalilisha Rais John Magufuli
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Leonard Kyaruzi, leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka mawili ikiwemo kuchepusha na kusambaza taarifa za kumdhalilisha Rais Dk. John Magufuli kwa njia ya mtandao whatsApp.
Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Magreth Bankika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Simon Wankyo alidai kuwa June 2, mwaka huu katika jengo la Tanzanite Tower lililopo barabara ya Sam Nujoma, mshtakiwa alichapisha taarifa ya kumdhalilisha Rais Magufuli.
Wankyo alinukuu taarifa hiyo kuwa, "Huyu Pombe ni kwamba hana washauri? Hashauriki? Au ni zuzu? Bwege sana huyu jamaa, He Doesn’t consider the law in place before opening his mouth! Au na yeye anaumwa ugonjwa wa Mnyika?” .
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza, mshtakiwa alisambaza taarifa ya kumdhalilisha Rais Magufuli, kupitia mtandao wa Whattsapp kwamba, “Hivi huyu Pombe ni kwamba hana washauri? Hashauriki? Au ni zuzu? Bwege sana huyu jamaa, He Doesn’t consider the law in place before opening his mouth! Au na yeye anaumwa ugonjwa wa Mnyika?”.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo. Hakimu Bankika amesema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja anayetambulika, atakayesaini hati ya dhamana ya Sh. Milioni moja.
Mshtakiwa alitimiza masharti hayo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Hakimu amesema kesi hiyo itatajwa Julai 18, mwaka huu na mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment