Thursday, 6 October 2016

Kila sehemu ina namna yake, Je, unaufahamu vizuri Utamaduni wa Wamadagaka?


Nchini Madagascar, jamii ya Malagasy ina mila na desturi ya kushangaza ambapo maiti hufukuliwa na kufanyiwa sherehe.



Familia yote huhusika katika sherehe hiyo ijulikanayo kama Famadihana lakini sasa changamoto ni kwa familia nyingi zinashindwa kuchangisha fedha za kugharamia mila hii.

Washambuliaji Wavamia Kituo huko Mandare, Kenya.


Watu kadha wanahofiwa kufariki baada ya watu wenye silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Taarifa zinasema washambuliaji hao walivamia ploti moja usiku wa manane.


Gavana wa jimbo la Mandera Ali Roba ameandika kwenye Twitter kwamba watu 6 wameuawa na mmoja kujeruhiwa.
Amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye ploti hiyo wameokolewa na maafisa wa usalama.



Bado haijabainika nani walitekeleza mashambulio hao.
Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa al-Shabaab kutoka Somalia.


Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.


Kundi la al-Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulio nchini Kenya ikiwemo mauaji ya watu 67 katika maduka ya Westgate mjini Nairobi mwaka wa 2013.


Mwezi Juni mwaka huu, wanamgambo wa kundi hilo walishambulia gari ya polisi aina ya Land Cruiser kilomita chache kutoka mji wa Mandera, na kuua maafisa watano wa polisi.


Mwaka uliopita al-Shabab walitekeleza mashambulizi katika chuo kikuu cha Garissa na kusababisha vifo vya wanafunzi 148

Monday, 18 July 2016

Marekani sasa ni mwendo wa risasi tu


Rais Barrack Obama wa Marekani amewasihi wamerakani wajizuie dhidi ya hisia kali baada ya Mmarekani Mweusi kuwapiga risasi na kuwaua maafisa watatu wa polisi katika shambulizi la pili la kulipiza kisasi dhidi ya polisi wazungu wanaowaua wamarekani weusi.

Obama ameomba uvumilivu utawale mioyo ya wakaazi wa mji wa Baton Rouge Louisiana nchini Marekani ambao sasa wanahofu ya kuzuka mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Gavin Long ambaye ni mwanajeshi wa zamani aliwapiga risasi polisi kulipiza kisasi mauaji ya Alton Sterling.

Obama aliyasema hayo katika hotuba ya moja kwa moja kupitia kwa runinga kutoka ikulu ya WhiteHouse muda mchache tu baada ya mtu mmoja mweusi kuua maafisa watatu wa polisi hukohuko Baton Rouge alikouawa mtu mweusi
Alton Sterling pasi na hatia yeyote majuma mawili yaliyopita.

Alton Sterling aliyeuawa na polisi mzungu pasi na kosa lolote
Hasira imekuwa ikitokota miongoni mwa watu weusi baada ya mtindo wa kuuawa kwa wanaume weusi na polisi wazungu kuendelea kwa muda mrefu ilihali hakuna hatua inayochukuliwa dhidi yao.

Gavin Long ambaye ni mwanajeshi wa zamani alikuwa amerekodi ujumbe katika mji wa Dallas siku chache baada ya polisi watano kuuawa mjini humo katika shambulizi lililotekelezwa kulipiza kisasi cha mauaji ya Sterling.

Hasira imekuwa ikitokota miongoni mwa watu weusi baada ya mtindo wa kuuawa kwa wanaume weusi na polisi wazungu kuendelea kwa muda mrefu
Sasa imebainika kuwa Long alikuwa ameweka video kwenye mtandao akilalamika jinsi polisi wanavyowatendea waamerika weusi ambapo alitoa wito kwa wanaume weusi kujitolea kuokoa jamii yao.

Long mwenye umri wa miaka 29 aliwahi kuhudumu kama mwanajeshi wa Marekani .
Rais Obama ameshauri watu weusi dhidi ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Polisi akisema mauaji ya kulipiza kisasi sio suluhisho la tatizo sugu la ubaguzi wa rangi bali utachochea uhasama zaidi dhidi yao na polisoi wazungu.

Sunday, 17 July 2016

Tanzania na tishio la Ugaidi


Tanzania imefaulu kuepuka mashambulizi ya kigaidi kama yaliyoshuhudia katika mataifa jirani kanda ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo Shambulizi la hivi punde dhidi ya msikiti mmoja nchini Tanzania limeibua tishio la kuibuka kwa ugaidi nchini humo.

Aliyepokonywa ubunge Longido aipinga hukumu


Aliyekuwa Mbunge wa Longido (Chadema), Onesmo Ole Nangole amekata rufaa kupinga hukumu ya kuvuliwa ubunge.

Wiki chache zilizopita, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sivangilwa Mwangesi alitoa hukumu hiyo baada ya kujiridhisha na malalamiko ya Dk Stephen Keruswa

Wa CCM kwamba mazingira katika chumba cha majumuisho ya kura hayakuwa rafiki kuakisi matakwa ya wapiga kura.

Ole Nangole amesema hayo alipokutana na baadhi ya wakazi wa jimbo hilo nyumbani kwake mjini Longido na kuwaelezea msimamo wake wa kukata rufaa.

“Hukumu haikuwa ya haki hata kidogo, hakuna fujo yoyote tuliyofanya sisi tulikuwa tukidai haki ya kutangaziwa matokeo na hiyo ni haki yetu,” amesema.

Amewaambia kwamba ameshawasilisha maombi ya kukata rufaa ambayo tayari yamepokewa.

Hatimaye Mrema aukwaa, aula wa Rais Magufuli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempa shavu mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema kwa kumteua kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 16.

Mrema akiwa na Rais Magufuli wakati wa kampenzi za uchaguzi uliyopita

Mrema ambaye amewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani wakati awamu ya pili, amekuwa akimwomba Rais Magufuli ampe kazi aliyomwahidi alipojitokeza kwenye kampeni zake na kumpigia debe.

Mbali na Mrema anayechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Eusebia Munuo ambaye muda wake umemalizika, Dk Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi na watendaji wa taasisi nyingine mbalimbali na pia amewapandisha vyeo maafisa wa Jeshi la Polisi Tanzania.

Wengine walioteuliwa ni Profesa William R. Mahalu ana kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Wizi wa nyanya wamsababishia mauti


Watu wawili, wakazi wa Wilaya ya Musoma Vijijini na Tarime mkoani Mara, wameuawa kwa tuhuma za wizi na ujambazi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Erinest Kimola amewataja waliouawa kuwa ni Nyagoma Mase (34), wa Kijiji cha Mayani, Musoma Vijijini na Sererya  Moses (20) wa Kijiji cha Masanga Tarime.

Kimola amesema Moses aliuawa Alhamisi saa mbili asubuhi katika Kijiji cha Kukikukwe baada ya kukutwa na debe la nyanya zilizodaiwa kuwa ni wizi mali ya Ibaba Tunga.

Amesema Tunga alipomkuta mtuhumiwa huyo akiwa na debe la nyanya hizo zilizoibwa shambani kwake, alipiga yowe kuita watu.

Amesema watu  walikusanyika na  kumshambulia  kwa kutumia silaha za jadi kisha kuchoma moto mwili wake na kuteketeza nyumba yake ya  nyasi na kwamba, tayari watu watatu wamedakwa kutokana na mauaji hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa awataka viongozi wazembe wajiondoe


Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi amewaonya watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea watafute sehemu nyingine ya kwenda.

Akizungumza katika ufunguzi wa duka la kampuni ya Simu ya Tigo katika mji wa Kibaigwa wilayani Kongwa,  Ndejembe amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ haitawavumilia watendaji wa aina hiyo.

“Nawapa namba ya simu hii mnipigie kwa kero yoyote, nawaahidi nitayafanyia kazi maoni yenu lakini isiwe mambo ya umbeya kwa sababu sitayafanyia kazi hayo,” amesema.

Pia, amewataka wakazi hao kufanya kazi kwa bidii ili kukuza kipato na kuacha kulalamika, kwa sababu maendeleo yanapatikana kwa kufanya kazi siyo  vinginevyo.

Saturday, 16 July 2016

Siku 3 za maombolezo zatangazwa Ufaransa kufuatia mauaji ya kigaidi

Serikali ya Ufaransa imetangaza maombolezo ya kitaiafa kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu ya wiki ijayo, baada ya lori lililoingizwa kwa kasi Alhamisi Julai 14 usiku katika umati wa watu waliokua wakitazama urushwaji wa fataki katika sherehe ya maadhimisho ya Siku kuu ya kitaifa ya Julai 14.

Shambulio hilo lililotokea katika eneo la Promenade des Anglais mjini Nice liliwaua watu 84, wengine kadhaa kujeruhiwa, na watu wengine 18 wakiwa katika "hali mbaya" kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya ndani Bernard Cazeneuve. Rais Hollande amezungumzia "mashambulizi hayo kuwa ni ya kigaidi bila shaka”.

Mwendesha mashitaka wa mjini Paris, François Molins, katika taarifa yake Ijumaa hii Julai 15 saa 11 jioni, ametoa ripoti ya hivi karibuni kuhusu shambulizi la mjini Nice. “Watu 84 wamepoteza maisha, wakiwemo watoto na vijana 10, majeruhi 202, ikiwa ni pamoja na watu 52 walio katika hali mbaya na 25 katika chumba cha wagonjwa mahututi, “ amesema François Molins.

Baada ya shambulizi hilo la mjini Nice, Rais François Hollande amelihutubia taifa Ijumaa hii katika Ikulu kimkoa ya mji wa Nice kusini mwa Ufaransa. Rais Hollande aliyekuja kushikamana na kuungana na Serikali, ameeleza kwamba Ufaransa bado inakabiliwa na vitendo vya kigaidi. "Bado tunakabiliwa na tishio," amesisitiza François Hollande.

"Wakati huu ambapo ninazungumza, watu 80 wameuawa, watu 84 hasa, na watu zaidi ya hamsini bado wako katika hali mbayakabisa, ninamaanisha, kati ya maisha na kifo ...", amesema Rais Hollande

Nchini Marekani, viongozi mbalimbali serikalini wameelezea mshikamano wao na Paris katika tukio hilo. Barack Obama amelaani vikali, "kile kinachoonekana kuwa shambulio la kutisha nchini Ufaransa."

Mgombea urais katika chama cha Republican, Donald Trump, amefuta mara moja mkutano wake na waandishi wa habari uliokua umepangwa kufanyika Ijumaa hii.

Waziri Mkuu wa Canada alionyesha kwa upande wake toka Alhamisi hii jioni mshikamano wake na Ufaransa. "Canada inahuzunishwa na shambulizi (Alhamisi) hii jioni njini Nice," alisema Justin Trudeau kwenye akaunti yake Twitter.

Nchini Brazil Kaimu Rais, Michel Temer, amelaani kitendo hiki kilichoendeshwa dhidi ya raia wasiokuwa na hatia waliokua wakiadhimisha maadili ya juu kwa wote, uhuru wa watu, usawa kati ya wananchi na udugu.

"Ujerumani iko bega kwa bega na Ufaransa katika mapambano dhidi ya ugaidi," amesema Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Ijumaa hii Julai 15 asubuhi. "Kauli yangu inatosha tu kusema tunaungana na marafiki zetu wa Ufaransa," ameongeza Angela Merkel.

"Urusi inashikamana na raia wa Ufaransa katika siku hii ngumu," amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin. "Urusi uko tayari kwa ajili ya ushirikiano wa karibu na Ufaransa katika mapambano dhidi ya ugaidi."

Waziri Mkuu wa Uturuki Binal Yildirim ameandika kwa Kifaransa kwenye ukurasa wake wa Twitter: "Uturuki, daima inashirikiana na mataifa duniani katika mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi, na inaungana naUfaransa katika siku hii ngumu."

Marais mbalimbali kutoka nchi za Afrika vile vile wameonyesha hisia zao baada yatukio hilo la kuhuzunisha lililotokea nchini Ufaransa.

Ombeni Sefue azungumza tangu alivyotenguliwa

Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue amesema baada ya miaka mingi ya utumishi wa umma sasa ni wakati wake wa kupumzika na hafikirii kujitosa katika siasa.


Balozi Sefue ambaye alikuwa kivutio kwenye televisheni kutokana na kutoa taarifa za kutenguliwa uteuzi kwa watumishi waandamizi wa umma kabla ya kibao kumgeukia, amesisitiza kuwa siasa haipo katika damu na kwamba kazi anayopenda ni kuzisaidia taasisi za ujenzi kwa kuwa ni taaluma anayoipenda.


Mbali na kuonyesha kutokuwa na mpango huo, Balozi Sefue aliupongeza utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa maelezo kuwa una kasi nzuri na kwamba kurejea kwa uadilifu ni jambo linalomfurahisha zaidi akiwataka vijana kufanya kazi kwa bidii baada ya kuaminiwa na kupewa nafasi mbalimbali.


Balozi Sefue ambaye awali hakuonekana kuwa mmoja wa watu ambao wangeng’olewa kwa sababu yoyote ile, alilazimika kuondoka Ikulu ndani ya siku 123 tangu Rais Magufuli aapishwe kuwa Rais na siku 67 tangu balozi huyo atangazwe kuendelea na wadhifa wake. Uteuzi wake ulitenguliwa Machi 6 na nafasi yake kuchukuliwa na Balozi John Kijazi.


Baada ya kimya cha muda mrefu, Mei mwaka huu, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi wa Utawala Bora), Dk Laurean Ndumbaro alikaririwa akisema kuwa baadhi makatibu wakuu walioachwa katika uteuzi na Rais, wapo waliostaafu kwa mujibu wa sheria, akiwamo Balozi Sefue.

Ndessamburo ataka CHADEMA ijengwe


Aliyekuwa mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amesema inahitajika nguvu kukijenga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na Serikali kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara nchini.

Ndesamburo ambaye ni mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro amesema  wakati akifungua mkutano wa faragha wa  makatibu na wenyeviti wa chama hicho wa wilaya.

“Kujenga chama siyo mchezo, tunakoeleka siyo kuzuri tukaze buti na tutekeleze tunachokisimamia kwa vitendo kwa sababu wenzetu wanatumia mbinu nyingi kuhakikisha wanatukwamisha,” alisema.

Amefafanua kuwa kutokana na chama hicho kuzuiliwa kufanya mikutano ya hadhara, viongozi wa kata hadi Taifa wanatakiwa kuongeza nguvu ya ziada na kutumia mbinu mbadala kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao.

Mratibu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema wameamua ‘kutafuna mbuyu’ chini kwa chini kutokana kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara ili kuhakikisha chama hicho hakiyumbi.

Mapinduzi ya Kijeshi yafanyika Uturuki


Kundi moja la kijeshi nchini Uturuki linasema limechukua udhibiti wa nchi, huku madaraja jijini Istanbul yakifungwa na ndege za kijeshi zikionekana kupaa katika anga ya Ankara.

Mapema waziri mkuu Binalo Yildirim alitangaza kuwepo kwa “hatua zisizo halali” zilizochukuliwa na “kundi” la kijeshi, na kusisitiza kuwa hakuna mapinduzi ya kijeshi. Alisema serikali bado inadhibiti nchi.

Magari yamezuiwa kuvuka katika madaraja yanayovuka mto Bosphorus jijini Istanbul.

Kumekuwa na taarifa za milio ya risasi katika mji mkuu Ankara, na pia milio ya risasi karibu na ikulu ya rais.

Kumeripotiwa pia mlipuko karibu na makao makuu ya mkuu wa jeshi.
Kituo cha CNN Idhaa ya Uturuki kimeripoti kuwa Rais Recep Tayyip Erdogan yuko "salama” lakini hakikufafanua zaidi.

Erdogan amezungumza na CNN Turk kupitia Facetime
Baadaye, Bw Erdogan ameambia kituo cha habari cha CNN Turk, kwenye mahojiano ya webcam, kwamba kitendo cha leo kimechochewa na kuwepo kwa "mfumo sambamba".

Amesema jaribio la mapinduzi litakabiliwa kwa "hatua ifaayo" na kuwataka raia wa Uturuki wajitokeze barabarani.
Mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter na YouTube ilizimwa muda mfupi baada ya taarifa za mapinduzi ya serikali kutokea.

Ney wa Mitego ahojiwa na Polisi


Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama  Ney wa Mitego amehojiwa kituo cha Polisi Kati na kupewa dhamana kufuatia tuhuma zinazomkabili.

Kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema msanii huyo alihojiwa juzi kituoni hapo na yupo nje kwa dhamana, huku jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na  tuhuma zinazomkabili.

“Ni kweli juzi mchana  tulimhoji Ney wa Mitego na yupo nje kwa dhamana kuhusu kukamatwa kwake nitatoa taarifa  kwa nini tulimkamata,”amesema Kamanda Sirro.

Friday, 15 July 2016

Wasusia mazishi ya ndugu yao baada ya Mahakama kutupilia mbali shauri lao


Ndugu wamesusa kushiriki maziko ya marehemu Andrew Daffa  kutokana na Mahakama kumpa haki hiyo mjane wake badala ya baba mzazi aliyetaka yafanyike mkoani Tanga.

Kususa kwa ndugu hao kunatokana na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kutupilia mbali maombi yaliyofunguliwa na baba wa marehemu huyo akitaka mwili wa mtoto wake kuzikwa kijijini kwao mkoani humo.

Mwili huo umezika  katika makaburi ya Yombo Vituka, Dar es Salaam chini ya ulinzi wa polisi.

Awali, mwili wa Daffa ulizuiwa kuzikwa kutokana na maombi namba 240 ya mwaka 2016 yaliyofunguliwa na baba wa marehemu,  Charles Joseph aliyetaka apewe kibali cha kumzika mwanaye katika Kijiji cha Vigiri mkoani humo kwa madai kuwa alizaliwa huko.

Mvutano huo ulikuja kufuatia mjane wa Daffa, Glory Charles kutaka kupewa haki ya kuzika mwili wa mumewe katika makaburi yaliyopo Yombo Vituka kwa kile alichoieleza eneo hilo ndilo walilozika watoto wao watano.

Kutokana na mvutano huo, Jumanne wiki hii, Mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya mwili huo kuzikwa Tanga.

Daffa alifariki dunia Jumatano ya wiki iliyopita katika Hospitali ya Amana.

Hakimu Adolf Sachore amesema chanzo cha familia ni baba, mama na watoto, hivyo mahakama imetoa kibali mwili  huo uzikwe walipozikwa watoto wake.

Makumi wauawa katika Shambulizi la kigaidi Mjini Nice, Ufaransa


Zaidi ya watu 70 wameripotiwa kuuawa katika shambulio lililotokea katika mji wa Nice kaskazini mwa Ufaransa.

Lori lililokuwa likienda mwendo kasi lilijiingiza katika mkusanyiko wa watu waliokuwa wakiangalia maonesho ya fataki kuadhimisha siku ya kitaifa ya Bastille, ambayo huja na shamra shamra kila mwaka.

Mwendesha mashtaka katika mji wa Nice, Jean- Michel Pretre amesema lori hilo liliendelea kutembea kilo mita mbili kabla ya polisi kumpiga risasi dereva.

Bunduki na makombora yameripotiwa kukutwa ndani ya lori hilo.

Wakazi wa mji huo wa Nice wameshauriwa kutulia majumbani.

Rais Francois Hollande amerudi mjini Paris kwa ajili ya kufanya kikao cha dharura.

Hali ya tahadhari iliyowekwa toka kutokea kwa shambulio lililofanywa na Islamic State mjini Paris, bado iko palepale nchini Ufaransa.

Mkoa wa Mbeya wakataa tuzo ya usafi


Si jambo la kawaida kukataa tuzo hususan kwa Waafrika lakini Mkuu wa Mkoa  wa Mbeya Amos Makalla ameikataa tuzo hiyo  kwa madai kuwa jiji lake halijastaili kwani bado ni chafu.

 Makalla ameungana na wananchi wa jiji hilo kupinga kutajwa kushinda nafasi ya kwanza kwa usafi nchini, na kudai bado  limejaa takataka.

Makalla amesema hajatambua  vigezo vilivyotumika kwani jiji halina hata bustani za kupumzika wananchi, limejaa takataka karibu na bustani za maua hususan eneo la Kabwe na mitaa mbalimbali.

Awali  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alilitaja Jiji la Mbeya kwamba limeongoza kwa makundi ya majiji kwa usafi, wakati Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ikiongoza nchini na Kinondoni ikiongoza kwa kundi la manispaa za majiji.

Mkazi wa Uwanja wa Ndege, Daudi Mahenge amesema ipo haja kwa  Serikali kutoa taarifa sahihi kwani Mbeya haijawahi kuwa safi.

BAVICHA wakubali yaishe Mkutano Mkuu wa CCM


Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Mkoa wa Rukwa  limetangaza kuwa hawatakwenda  kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bavicha mkoani humo, Aida Khenan amesema wametii agizo la Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe la kuwazuia kwenda Dodoma.

“Tumeheshimu agizo la Mbowe ambalo limejaa busara na hekima kubwa  japokuwa  tulikuwa tayari kwenda Dodoma,” amesema Khenan ambaye pia  ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema).

Katibu wa Bavicha Mkoa wa Rukwa, Deogratis Kashatila  ameishauri Serikali  ya CCM isivizuie  vyama  vya  siasa kufanya mikutano kwa kuwa nchi ilisharidhia mfumo wa vyama vingi kwani ni kinyume na katiba.

Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi alinukuliwa akisema baraza hilo limeamua kuzuia mkutano huo wa CCM kutokana na tamko la Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yote ya kisiasa. “Hakuna mkutano wowote wa siasa unaotakiwa kufanyika, iweje CCM waandae mkutano huo, sisi vijana wa Chadema tutakuwapo Dodoma kuzuia,” amesema

Ombaomba wapato 60 wakamatwa jijini Dar

Katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ombaomba 60 wamekamatwa katika msako unaoendelea.

 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe amesema wamewakamata 60 na operesheni inaendelea.

“Ukamataji wa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam unaendelea, 60 wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka,”  amesema Dk Magembe.

Amesema miongoni mwa ombaomba hao, wapo watoto wenye umri wa chini ya miaka 18   ambao wamepelekwa katika vituo vya watoto yatima, kikiwamo Kituo cha Kurasini.

Dk Magembe amesema  bado ombaomba wamekuwa wakionekana jijini  Dar es Salaam kutokana na kuwapo kwa watu wanaotoka mikoani na kuingia katika makundi ya ombaomba kila siku.

Amesema  uongozi wa mkoa unashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoa elimu mikoani kuhusu operesheni ya kuwaondoa ombaomba.

Amesema ombaomba wengi wanakuja kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Awali  Makonda alitangaza operesheni kubwa ya kuondoa ombaomba katika Jiji la Dar es Salaam.

Aliwataka polisi kwa kushirikiana na ustawi wa jamii kuwaondoa ombaomba wote waliopo mitaani.

Pia, Makonda amepiga marufuku wananchi wanaowapa fedha ombaomba  kuacha mara moja ili wajitafutie riziki wenyewe kwa kufanya biashara au kurudi mikoani kujishughulisha na kilimo.

Mahakama yatupilia mbali pingamizi Tundu Lissu


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na washtakiwa wa kesi ya uchochezi, akiwamo mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu dhidi yake ikisema ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi mwisho.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, mwandishi, Idrissa Jabir Yunus na mchapishaji wa gazeti hilo, Ismail Mehboob.

Hakimu Thomas Simba amesema kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo tofauti na inavyodhaniwa na washtakiwa hao.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi hiyo  kwa kuandika na kuchapisha makala katika gazeti la Mawio la Januari 14-20, mwaka huu yenye kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar.”

Awali, Wakili wa washtakiwa hao,  Peter Kibatala aliweka pingamizi akidai Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo kwa  madai kuwa Kifungu cha Sheria ya Magazeti kilichotumiwa kuwashtaki  kinatumika Tanzania Bara tu na si Zanzibar.

Amedai Tanzania ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano inayojitegemea na kwamba mashtaka hayo yanazungumziwa kuwa yanasababisha chuki dhidi ya  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikikiliza.

 Hata hivyo, katika uamuzi wake jana, Hakimu Simba alifafanua kuwa  kifungu cha Sheria ya Magazeti kilichotumika kuwashtaki kinatumika hata Zanzibar.

Pia, Mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja nyingine ya pingamizi la upande wa utetezi la uhalali wa shtaka la tatu, ikisema liko mahakamani kiusahihi.

 Wakili Kibatala katika pingamizi lake kuhusiana na shtaka hilo alidai maelezo hayakidhi vigezo vya kisheria kulifanya liwe la uchochezi na hayako wazi ili washtakiwa wajitetee, hivyo aliiomba mahakama  kulifuta.

 Hakimu Simba alikubaliana na hoja za upande wa mashtaka kuwa shtaka hilo ni sahihi na linajitosheleza.

Thursday, 14 July 2016

Donald Trump asubiriwa kumtangaza msaidizi wake

Mgombea mtarajiwa wa chama cha Republikan Donald Trump anaendelea kupunguza watu anaotarajiwa kuchagua mgombea mwenza wa urais na anapanga kutoa tangazo lake Ijumaa.

Trump amesema katika mtandao wake wa Tweeter kwamba atatangaza saa 5 asubuhi Ijumaa katika jimbo la New York.

Kati ya wanaotarajiwa kupewa nafasi ni pamoja na Gavana wa Indiana Mike Pence ambaye alikuwa nae katika hafa ya uchangishaji fedha jumanne , spika wa zamani wa bunge la Marekani Newt Gingrich , na Gavana wa new Jersey Chris Christie .

Christie aliwahi kuwa mgombea wa chama cha republican na mpinzani wa Donald Trump katika uchaguzi wa awali ila aliamua kumuunga mkono mapema Trump baada ya kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Uhaba wa nishati ya umeme kuikumba Ghana


Ukosefu wa nguvu za umeme umetokea kwenye taifa la pili kwa ukubwa katika eneo la Afrika magharibi la Ghana.
Ukosefu wa nguvu za umeme umetokea kwenye taifa la pili kwa ukubwa katika eneo la Afrika magharibi la Ghana huku Rais John Dramani Mahama akilaumu wazalishaji wa mafuta katika Niger Delta nchini Nigeria.

Uchumi wa Ghana uliwahi kukua kwa haraka katika eneo hilo, lakini ukosefu wa umeme wa mara kwa mara, Serikali kutumia fedha zaidi pamoja na kuanguka kwa bei za bidhaa zinazotoka nchini humo zimepelekea Shirika la Fedha Duniani, IMF kutoa msaada wa dola bilioni moja kama njia ya kuokoa uchumi.

Rais Mahama amezungumzia tatizo lililoanza mapema mwaka huu baada ya kundi la wanamgambo kwa jina la Niger Delta Avengers, kuanza kuharibu mabomba yakusafirisha mafuta pamoja na vifaa muhimu katika eneo la Niger Delta ambapo Ghana inaagiza mafuta yake.

Wanajeshi wa Uganda waingia nchini Sudan Kusini

Hali ya usalama bado ni ya wasiwasi nchini Sudan Kusini licha ya hali ya utulivu kurejea, baada ya mapigano ya mwishoni mwa wiki iliyopita. Hakuna mapigano Alhamisi hii Julai 14 kwa siku ya tatu mfululizo.

Lakini nchi nyingi za kigeni zimeendelea kuwarejesha nyumbani raia wao. Na Alhamisi hii asubuhi, msafara wa majeshi ya Uganda umeingia katika ardhi ya Sudan Kusini, ukiwa na sababu rasmi, kuwarejesha nyumbani raia wa Uganda.

Askari zaidi ya mia moja na malori hamsini kutoka Uganda wameingia katika ardhi ya Sudan Kusini Alhamisi hii Julai 14. Hatua hiyo ilitangazwa siku moja kabla, na msafara ulichelewa kutokana na uamuzi wa Serikali ya Sudan Kusini kufunga mipaka yake.

"Vikosi vyetu vya vya jeshi viko njiani vikieleea katika mji wa Nisitu, kilomita 30 ana mji wa Juba. Hatuna nia ya kwenda mbali zaidi ya mji wa Nisitu, wala nia ya kwenda hadi katika mji wa Juba. Tayari kuna raia 2,000 wa Uganda ambo wanasubiri kurejeshwa nyumbani. Tunaamini kwamba operesheni hii itadumu siku 10, hadi 20, "amesema msemaji wa serikali ya Uganda.

Kuhusu muda wa operesheni, kumekuwa na hisia tofauti. Afisa wa Idara ya Ujasusi ya Uganda amelielezea shirika la habari la AFP kwamba vikosi vya jeshi la Uganda vnaweza kukaa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa mjini Juba, na kuongeza, "tumefanya hivyo katika siku za nyuma, kwa nini tusifanye hivyo kwa sasa? "

Marekani kwa upande wake, tayari imetangaza kwamba imewatuma askari 47 katika mji wa Juba, "kulinda raia na mali ya Marekani." Serikali ya Marekani imeongeza: "kwa sasa mjini Djibouti, askari wa ziada wako tayari kutumwa nchini Sudan Kusini kama itahitajika. "

Rwanda yapuuzia kumkamata Rais wa Sudan Kaskazini


Serikali ya Rwanda imepuzuia mbali ombi la mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai yenye makao yake makuu huko Hague Uholanzi ICC ya kumkamata rais wa Sudan Omar el-Bashir.

Rais Bashir atahudhuria kongamano la viongozi wa Afrika linaloandalia mjini Kigali wikiendi hii.

Rais Bashir atahudhuria kongamano la viongozi wa Afrika linaloandalia mjini Kigali wikiendi hii.

Waziri wa maswala ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo amesema kuwa ombi la ICC kupitia kwa barua rasmi walioiandika siku mbili zilizopita haina uzito wowote.

Mapema juma hili mahakama ya ICC iliyashtaki mataifa ya Djibouti na Uganda kwa baraza kuu la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kukosa kumkamata rasi Bashir alipozuru mataifa hayo.
Hii sio mara ya kwanza ziara ya rais Bashir imezua utata.

Mwaka uliopita mahakama ya Afrika Kusini ilimpata na hatia rais Jacob Zuma kwa kukiuka amri ya mahakama ya kumtia mbarano rais Omar el Bashir alipohudhuria mkutano wa umoja wa Afrika mjini Johannesburg nchini humo.

Waziri wa maswala ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo
Moja ya mada kuu katika kikao kijacho cha Kigali, itakuwa uhusiano baina ya bara la Afrika na mahakama hiyo ya ICC.

Viongozi wa Afrika wamekuwa wakishikilia kukutu dhana kuwa dhamira kuu ya mahakama hiyo ni kuwahukumu viongozi wa Afrika ,huku viongozi wa mataifa ya magharibi wakiruhusiwa kuponyoka mkono wa sheria licha ya kuwepo kwa madai dhidi yao.

ICC iliyashtaki mataifa ya Djibouti na Uganda kwa baraza kuu la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kukosa kumkamata rasi Bashir alipozuru mataifa hayo.

Mahakama hiyo kwa upande wake inasema kuwa imekuwa ikijaribu kutoa haki kwa maelfu ya waafrika ambao wamedhulumiwa.

ICC inamtaka bwana Bashir akamatwe kwa makosa ya mauji ya halaiki katika jimbo la Darfur Sudan.
Rais Bashir amekanusha madai yote dhidi yake.

Wednesday, 13 July 2016

Dr. Kizza Besigye aachiliwa kwa dhamana


Mahakama kuu nchini Uganda, imemuachia kwa dhamana kiongozi mkuu wa upinzani na aliyekuwa mgombea Urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Dr. Kizza Besigye.

Mwanasiasa huyo wa chama cha The Forum for Democratic Change, FDC, alikuwa anazuiliwa kwenye gereza la Luzira akituhumiwa kwa kosa la uhaini.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Wilson Masalu Musene, amesema kuwa dhamana anayopewa Besigye ni ishara ya haki ya kisheria ya mtuhumiwa, ya kwamba hana hatia hadi pale atakapopatikana na hatia au mtu kukiri kosa.

Jaji Masalu ameongeza kuwa, "kipekee Besigye kama watuhumiwa wengine, alikuwa anahudhuria vikao vya kesi yake kwa uaminifu".

Besigye, mgombea wa nafasi ya Urais kwa zaidi ya mara nne na kushika nafasi ya pili kwenye chaguzi zote, mwezi February mwaka huu baada tu ya kumalizika kwa uchaguzi wa rais, alijiapisha ambapo baadae alishtakiwa kwa kosa la uhaini.

Kwa mujibu wa sheria za Uganda, kifungu namba 23 cha Penal Code, kinasema kuwa, mtu akipatikana na hatia ya kosa la uhaini, hukumu yake ni adhabu ya kifo.

Makosa mengine yanayomkabili Besigye ni pamoja na kujitangaza mshindi kinyume cha sheria, kukaidi amri halali ya polisi na kuitisha maandamano kinyume cha sheria pamoja na kula kiapo kinyume na sheria za nchi.

Viongozi wa BAVICHA kizimbani


Viongozi wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, BAVICHA, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini, wakikabiliwa na mashtaka ya kukutwa na maandishi ya uchochezi.

Mahakama imewaonya washtakiwa hao, kutofanya kosa lolote la jinai wakiwa nje kwa dhamana, vinginevyo dhamana yao itafutwa.

Washitakiwa hao wametajwa kuwa ni Patrobas Katambi (33), mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Julius Mwita (30) Katibu wa Bavicha Taifa mkazi wa Dar es Salaam na George Tito (28) Mwenyekiti wa baraza hilo mkoani Mbeya.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa serikali, Beatrice Nsana na Lina Magoma huku upande wa washtakiwa wakitetewa na mawakili watatu wa kujitegemea, Fred Kalinga, John Gigongo na Isack Mwaipopo.

Akiwasomea shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi James Karanyemaha, Wakili wa Serikali Lina Magoma alisema washtakiwa wanadaiwa kukutwa na maandishi yenye lugha ya uchochezi kinyume na Kifungu cha 32(2) cha Sheria ya Magazeti Namba 229 iliyofanyiwa marejeo 2002.

Alidai Julai 9, mwaka huu katika baa ya Cape Town Manispaa ya Dodoma, washtakiwa walikutwa na fulana zenye maandishi ya “Mwalimu Nyerere Demokrasia Inanyongwa na Tuungane tuukatae Udikteta Uchwara.”

Washtakiwa walikana shtaka hilo huku upande wa mashtaka ukisema unaendelea na upelelezi na kuomba tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo. Alisema hauna pingamizi la washtakiwa hao kuachiwa kwa dhamana.

Hakimu Karayemaha alisema dhamana iko wazi kwa washtakiwa kwa kila moja kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika wenye barua kutoka kwa mtendaji kata na wawe na mali isiyohamishika, yenye thamani isiyopungua Sh milioni moja.

Pia aliwataka wadhamini kuhakikisha washtakiwa wanahudhuria mahakamani kila tarehe ya kesi na kama kuna sababu ya msingi mdhamini afike mahakamani kutoa taarifa. Alisema mshtakiwa ambaye atafanya kosa lolote la jinai akiwa nje kwa dhamana, dhamana yake itafutwa.

Washtakiwa walitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo imepangwa kutahjwa tena Julai 26, mwaka huu. Katika kesi nyingine, Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema Taifa, Joseph Kasambala (32) alipandishwa kizimbani kujibu shtaka la kutumia maandishi ya uchochezi.

Ilidaiwa na Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana kuwa Julai 9, mwaka huu katika Kituo cha Kikuu cha Polisi, mshtakiwa alikutwa akiwa na fulana yenye maandishi ya Mwalimu Nyerere Demokrasia imenyongwa. Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Julai 26, mwaka huu.

Watumishi hewa kizuizi cha ajira zaidi ya 70 elfu


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema serikali imelazimika kusitisha ajira mpya za watumishi 71,496 serikalini, mwaka huu hadi pale tatizo la watumishi hewa litakapopatiwa ufumbuzi.

Akifungua mafunzo kuhusu maadili ya viongozi wa umma kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji Ikulu Dar es Salaam jana, Kairuki alisema tangu oparesheni ya kutafuta watumishi hewa ianze hadi sasa watumishi 12,246 wameshaondolewa.

Kairuki alisema tatizo la watumishi hewa nchini bado ni kubwa kwani uzoefu unaonesha kuwa nchi nyingi zilizokumbwa na tatizo hilo, ni asilimia ndogo tu ya watendaji ndio iliyokuwa inawajibika.

Alisema kwa sasa serikali imelazimika kusimamisha masuala mengi ya utumishi wa umma ili ipate taarifa kamili ya aina ya watumishi waliopo, na kwamba ma-DED hao kuhakikisha wanasimamia vyema oparesheni hiyo kwani hadi sasa watumishi hewa waliobainika, takribani asilimia 90 wanatokea katika Serikali za Mitaa.

Aidha, Kairuki alisema pamoja na kugundulika kuwa tatizo la watumishi hewa ni kubwa nchini, pia serikali imebaini kuwepo kwa watumishi watoro wasiotimiza wajibu wao.

“Nawataka mkahakikishe mnawabana hawa maofisa utumishi, haiwezekani kuwepo na tatizo la watumishi hewa kubwa kiasi hiki huku pia kukiwa na tatizo la watumishi watoro, hawa maofisa kwani walikuwa na majukumu gani?” Alihoji Kairuki.

Alisema endapo serikali itabaini kuwa maofisa utumishi hao wamehusika katika matatizo hayo ya watumishi hewa na utoro, wataondolewa mara moja. “Serikali haina mchezo kila ofisa katika eneo lake, awe ofisa elimu, afya na kilimo wafanye kazi zao,” alisema.

Mtoto anusurika kuliwa na ndege tai Australia


Tai mmoja mkubwa nusura afanye kitendo cha kustaajabisha ,,, tai huyo alijaribu kumtwaa mvulana mmoja na kupaa naye nchini Australia.

Umati wa watu uliokuwa katika hifadhi ya Alice Springs Desert Park ulipigwa na butwaa tai huyo alipojaribu kumbeba mtoto wakati wa kurekodi kwa onyesho moja la wanyama pori.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa ''ilikuwa ni kama tai huyo aliona mnyama mdogo ambaye alitaka kumfanya mlo wake''

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa ''ilikuwa ni kama tai huyo aliona mnyama mdogo ambaye alitaka kumfanya mlo wake''.

Mvulana huyo anayekisiwa kuwa kati ya miaka 6-8 aliepuka kwa kupiga kamsa na mwishowe ndege huyo mkubwa akapaa na kutoweka.

Mvulana huyo alitibiwa baada ya makucha ya ndege huyo kumgwara usoni.

Hata hivyo wahudumu wa hifadhi hiyo waliingilia kati na kumfukuza tai huyo.

Bi Christine O'Connell kutoka Horsham katika jimbo la Victoria aliyenasa tukio hilo kwa kamera anasema tai huyo alimvamia mtoto huyo akijaribu kumuinua.

Hata hivyo wahudumu wa hifadhi hiyo waliingilia kati na kumfukuza tai huyo.

Wasimamizi wa hifadhi hiyo wamemuondoa tai huyo kwenye onyesho hilo.

Waandalizi wa onyesho hilo walifungasha virago vyao kwa haraka baada ya tukio hilo maarufu.

Wasimamizi wa hifadhi hiyo wamemuondoa tai huyo kwenye onyesho hilo.

Monday, 11 July 2016

Mwanamke apinga unyanyasaji unaotekelezwa na Polisi nchini Marekani


Maandamano nchini Marekani kupinga mauaji ya wanaume weusi na polisi wazungu yameendelea katika mji wa Baton Rouge, Louisiana.

Makumi ya waandamanaji walikamatwa huku polisi wakiendeleza sera yao ya kuwakamata kamata weusi wanaopinga mauaji hayo ya polisi.

Viongozi wa vuguvugu la Black Lives matter walikamatwa
Matukio ya makabiliano hayo yameibua hofu ya kuenea kwa uhasama na ubaguzi wa rangi. Hata hivyo picha moja imeibua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii kote duniani.

Polisi wameendeleza kauli ya kuwa na msimamo mkali dhidi ya weusi
Picha hiyo inaonesha maafisa wawili wa polisi waliojihami hadi kwenye kisigino wakijiandaa kumkabili kipusa mmoja mweusi ambaye hakuwa amejihami kwa namna yeyote ila kwa ujasiri wa kupinga mauaji hayo ya wanaume weusi jumanne iliyopita.

Picha hiyo ya mwanamke huyo imefananishwa na ile ya ''Tank Man'' ya China
Picha hiyo ilipigwa na mpiga picha wa shirika la habari la Reuters Jonathan Bachman, ambaye ni mkaazi wa mji wa New Orleans.

Waamerika wengi waliosambaza picha hiyo wameifananisha na ile picha ya mwanaume aliyekuwa akipigania haki za wenyeji nchini China wakati walipokabiliwa na wanajeshi wakiwa wamejihami na vifaru vya kijeshi.

Wapiganiaji haki za kibinadamu na haswa haki za wamarekani weusi wamekuwa wakijadili sadfa ya kuwa taifa linalodai kuwa kitovu cha demokrasia kinatumia mbinu za kidhalimu zilizotumika mataifa ya kikomunisti karne iliyopita.

Wanaume weusi wamejipata pabaya mikononi mwa polisi wazungu
Mpiganiaji haki za weusi Shaun King ambaye pia ni mwandishi wa jarida la New York Daily anasema kuwa ni jambo la kufedhehesha mno mno kuwa picha hiyo ya kihistoria inatokea Marekani mwaka huu wa 2016, weusi wakipigana dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Alton Sterling ambaye mauaji yake yaliibua maandamano Marekani
Kipusa huyo anadaiwa kukamatwa na polisi lakini hakuna anayemfahamu wala anayejua kilichomkuta mikononi mwa polisi.

Sudan Kusini hali si shwari, ndege za kivita zatumika katika mapigano


Uganda imetangaza kwamba itatuma wanajeshi wake katika mpaka wake na Sudan Kusini baada ya mapigano kuzuka upya nchini humo.

Msemaji wa jeshi la Uganda Paddy Ankunda amesema wanajeshi hao watatumwa kuzuia mapigano kuenea hadi maeneo ya Uganda.

Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa mataifa, linawaomba viongozi wakuu wa serikali ya Sudan Kusini, kuyadhibiti majeshi yao.

UN inasema kuwa mashambulio dhidi ya raia na makao makuu pamoja na kambi ya Jeshi ya Umoja wa mataifa, ni uhalifu wa kivita.

Walinda amani wawili wa umoja wa mataifa kutoka Uchina, wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Umoja wa mataifa unasema kwamba, mataifa jirani na Uchina yanafaa kujiandaa kutuma majeshi zaidi nchini humo, ikiwa hali ya usalama itaendelea kudorora .

Wanajeshi wakishika doria mabarabarani katika mji mkuu wa Juba
Hata hivyo baraza hilo litahitaji kuidhinisha vikosi zaidi.

Kwa sasa wanajeshi wa umoja wa mataifa walioko Juba ni elfu 13 pekee.
Mapigano yazuka tena Juba, Sudan Kusini.

Umoja wa mataifa unasema kuwa, walinda amani wanafaa kutumia kila mbinu kuwalinda raia.

Waandishi wa habari wameiambia BBC kuwa ndege za helikopta zimetumika kurusha risasi pande zote huku zikishambulia majengo ya maskani ya bwana Machar.

Wanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir na wale watiifu kwa Riek Machar wamekuwa wakipigana tangu Alhamisi.

Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika makao makuu ya kambi ya kijeshi ya umoja wa mataifa.

Vifaru vya kivita vinaonekana katika barabara za mji mkuu Juba, huku wakaazi wakijifungia ndani ya majumba yao. Mamia ya watu wameuwawa tangu ghasia hizo zianze upya siku tano zilizopita.

Mapigano yaliyoripotiwa kutokea katika uwanja wa ndege mjini Juba, yamesitishwa, huku mashirika mbalimbali ya usafiri wa ndege kuingia na kutoka mjini Juba, likiwemo shirika la ndege nchini Kenya -KQ yamesitisha usafiri.

Marekani yawaonya wakuu wa Sudan Kusini na kuwataka wakomeshe mapigano


Serikali ya Marekani, imetaka kusitishwa mara moja kwa vurugu nchini Sudan Kusini, baada ya kutokea mapigano mapya, jijini Juba, mapigano yanayotishia kuvunjika kwa mkataba wa amani kwenye taifa hilo jipya kabisa duniani.

Mapigano haya ni ya kwanza kati ya jeshi la Serikali na wanajeshi waasi mjini Juba, toka kurejea nyumbani kwa kiongozi wao, Riek Machar mwezi April mwaka huu, na kuchukua nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais, kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu nchini humo kwa miaka 3.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani, imeagiza kuondoka nchini humo kwa raia na wafanyakazi wake, na kulaani taarifa kuwa raia wa kawaida wemeshambuliwa, ambapo mpaka sasa watu 150 wamekufa kutoka kila upande.

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, akitia saini kwenye mkataba wa usitishaji wa mapigano nchini mwake, 26 August 2015
UN Photo/Isaac Billy
Utawala wa Washington, unawataka viongozi wote wawili, wanasiasa na makamanda wa vikosi, kuagiza wanajeshi wao kujiepusha na makabiliano ili kuzuia mapigano zaidi, na kuagiza warudi kwenye makambi yao, amesema msemaji wa wizara hiyo, John Kirby.

"Marekani imedhamiria kuhakikisha inachukua hatua stahiki ili kuwawajibisha wahusika wa machafuko haya mapya ambayo ni wazi yanakiuka sheria za kimataifa zinazolinda binaadamu, ikiwemo kushambuliwa kwa kambi ya tume ya umoja wa Afrika nchini humo, UNMISS.

Machafuko haya yamejiri siku moja tu baada ya taifa hilo kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 5 toka taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa Sudan, Jumamosi ya wiki iliyopita, Julai 9.

Machafuko haya mapya yalianza Ijumaa ya wiki iliyopita na kuendelea hadi mwishoni mwa juma, ambapo wananchi wameonekana wakikimbia makazi yao mjini Juba, huku umoja wa Mataifa ukisema kuwa roketi na silha nzito za kivita zimetumiwa, halikadhalika ndege za kivita na vifaru.

Onyo hili la Marekani, linatolewa wakati huu baraza la usalama la umoja wa Mataifa, likifanya kikao chake cha dharula, ambapo umezitaka pande zote mbili kuzuia wanajeshi wao kukabiliana.

Nchi 15 wanachama za baraza la Usalama, zimewataka Rais Salva Kiir na makamu wake wa kwanza wa Rais Riek Machar, kuheshimu mkataba wa amani na kuhakikisha wanatekeleza maazimio ya usitishaji wa kudumu wa mapigano.

Mapigano yazuka Sudan Kusini


Msemaji wa jeshi tiifu kwa makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar ameiambia BBC kuwa majeshi yao yanakabiliana na jeshi la serikali tiifu kwa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Kanali William Gatjiath amesema kuwa wanajeshi watiifu kwa bw Machar wamevamia mji mkuu wa Juba kutoka pande zote .

Kanali Gatjiath anasema wanajeshi hao wanalipiza kisasi kufuatia mashambulizi makali kutoka kwa jeshi la rais Kiir.

Serikali haijasema lolote tangu machafuko hayo yaanze muda mchache uliopita.

Awali Wanajeshi wanamuunga mkono makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar walisema kuwa kambi yao ilishambuliwa usiku wa kuamkia leo kwa risasi na bunduki nzito nzito.

Rais Salva Kiir na makamu wa rais Riek Machar wamewasihi wafuasi wao kulinda amani.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini unasema kuwa kulitokea ufyatulianaji wa risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba..
Maeneo yanayodhaniwa kuathirika sana ni yale ya Jebal.

Ujumbe huo unasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa rasasi ulishuhudiwa karibu na kambi ya umoja wa mataifa.

Siku za hivi majuzi ziaidi ya watu 100 wanaripotiwa kuuawa mjini Juba wakati wa mapigano kati ya wafuasi wa rais Salva Kiir na makamu wa rais Riek Machar
Wawili hao walikubaliana kumaliza vita vya wenywe kwa wenyewe na wametoa wito wa kuwepo utulivu.

Ripoti za awali kutoka nchini Sudan Kusini zilisema kuwa takriban watu 100 waliuawa wakati wa mapigano kati ya wanajeshi hasimu katika mji mkuu Juba.

Hata hivyo idadi kamili bado haijulikani lakini wengi wa wale waliouawa wanaripotiwa kuwa wanajeshi.
Mapigano hayo yaliyoanza siku ya Alhamisi yaliendelea hadi mapema Jumamosi.

Mwandishi wa habari mjini Juba anasema kuwa wanajeshi wameweka vizuizi vya barabarani mjini humo.

Anasema kuwa masoko yamefunguliwa lakini watu wengi wamebaki nyumbani.
Sudan Kusini inaadhimisha miaka mitano ya uhuru wake.

Baada ya kifo cha Osama bin Laden mwanaye aapa kulipiza kisasi


Mwana wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden, ameapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya baba yake.
Katika ujumbe wa sauti uliochapishwa katika mitandao Hamza bin Laden ameapa kulipiza kisasi kwa Marekani kwa kumuua babake 2011 huko Pakistan.

Ujumbe huo wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama,", Hamza ambaye inaaminika kuwa alikuwa na babake makomando wa Marekani walipowavamia na kumtwaa ameapa kuendeleza kazi aliyoianza babake.

Ujumbe huo ni wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama,"
''Tutaendelea kuwasaka na kuwapiga popote pale mtakapokuwa mumejificha ati nyuma ya pazia za usalama kwa maovu munayoyaendeleza, Palestina, Afghanistan, Syria, Iraq, Yemen, Somalia na kote kwenye ardhi ya waislamu mnayokalia '' shirika la habari la Reuters linamnukuu.
''Na kwa wale wanaodhania kuwa tutakuwa tukilipiza kisasi mauaji ya Osma ole wenu, kwa nini sisi tutakuwa tukilinda dini ya kiislamu'' alisema Hamza.

Osama aliuawa na makomando wa marekani katika maficho yake huko Pakistan mwaka wa 2011.

Hamza ambaye kwa sasa ana umri wa kati ya miaka ishirini hivi alikuwa na babake kabla ya mashambulizi ya kigaidi ya mwaka wa 9/2001 huko Afghanistan kabla ya kukimbilia Pakistan kufuatia mashambulizi makali ya Marekani na washirika wake.

Hamza kulingana na wachanganuzi anatambulishwa na kiongozi wa kidini wa kundi hilo Ayman al-Zawahiri katika ujumbe huo unaolenga kuwavutia vijana ambao kwa sasa wamejiunga kwa wingi na kundi la Islamic state.

Sunday, 10 July 2016

Viongozi wa BAVICHA watiwa mbaroni Dodoma


Viongozi sita wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) wamekamatwa na Polisi mjini Dodoma kwa madai ya kukusudia kuikashifu Serikali.

Katika siku za karibuni, viongozi wa Bavicha wamekuwa wakitoa matamko mbalimbali ya kuwahamasisha wafuasi wake kuja mjini hapa kwa kile walichoeleza kuwa ni kuisaidia polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika Julai 23 kwa madai kuwa jeshi hilo lilishapiga marufuku mikutano ya kisiasa.

Hata hivyo, jana polisi imetoa ufafanuzi juu ya kauli yake ikisema kwamba kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara ya siasa na siyo ya ndani kama huo wa CCM..

Awali polisi waliwakamata Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Mkuu, Julius Mwita, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, George Tito, Katibu Mwenezi wa Bavicha, Edward Simbeye na Katibu Bavicha Wilaya ya Temeke, Hilda Newton na baadaye Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema, Joseph Kasambala aliyekamatwa baada ya kwenda kituo cha polisi kwa lengo la kuwawekea dhamana wenzake.

Wàziri Simbachawene awatahadharisha viongozi wa Umma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amesema sheria haziwaruhusu viongozi wa umma kuwa na kampuni binafsi zinazofanya kazi ndani ya manispaa wanazoongoza.

Waziri Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Kibwake (CCM), amesema mkurugenzi atakayebainika kutoa zabuni kwa kampuni yake binafsi wakati ni kiongozi wa umma, atachukuliwa hatua za kisheria.

Ametoa kauli hiyo juzi wakati akipokea vifaa vya kisasa likiwamo trekta na mitambo maalumu kwa ajili ya Mradi wa Uboreshaji Miji Kimkakati (TSCP), kutoka kwa Mratibu wa mradi, Davis Shemangali.

“Sidhani kama wapo wenye tabia hii. Kama wapo waache mara moja kujihusisha na mchezo huu kwani tutawachukulia hatua kali,” alisema Waziri Simbachawene.

John Mnyika asema hana mpango kuhama CHADEMA


Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amekanusha taarifa zinazodai kuwa anataka kuachana na chama hicho.

 Mnyika amesema hayo jana alipopigiwa simu ili azungumzie taarifa hizo. Mbunge huyo wa Kibamba amesisitiza kwamba huo ni uzushi.

 “Hakuna kitu kama hicho na wala sina mpango wa kuhama,” alisema.

Habari za kujiuzulu kwa Mnyika zilianza kusambaa katika vyombo vya habari kwa mara ya kwanza mwaka 2013 baada ya aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kufukuzwa uanachama.

Uvumi ulienea kwenye mitando kwamba amejivua nyadhifa zake zote na kwamba ameshakabidhi barua yake kwa katibu mkuu wakati huo, Dk Willibrod Slaa.

Julius Mtatiro anena kuhusu viongozi wa Siasa za Tanzania


Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amesema siasa za Tanzania zinakokwenda zinahitaji viongozi wapya, damu tofauti na wanaoweza kutazama mambo kisasa zaidi na kwa mahitaji ya kizazi cha sasa.

Mtatiro amesema jana kuwa  hatarajii kugombea uenyekiti katika chama hicho wala haungi mkono kurejea kwa Profesa Ibrahim Lipumba.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Mtatiro amesema kwa kipindi kirefu kumekuwa na msukumo mkubwa kutoka kwa viongozi wa chama ngazi za wilaya, wajumbe wa mkutano mkuu, wabunge, madiwani, wanachama, wafuasi na wapenzi wa kada mbalimbali kumtaka ashiriki kinyang’anyiro hicho.

Jana Mwananchi lilikwenda nyumbani kwa Profesa Lipumba ili kujua msimamo wake ndani ya CUF na kuelezwa kuwa amepumzika anajisikia vibaya.

Al-Shabaab walitikisa Jeshi la Polisi Kenya


Jeshi Polisi nchini Kenya hapo jana Jumamosi lilisema kwamba zaidi ya wapiganaji 100 wa dola la Kiislamu walivamia kituo cha polisi Kaskazini-Mashariki mwa Kenya na kujeruhi afisa mmoja na kuondoka na silaha na risasi.

Shambulizi hilo katika kituo cha polisi cha Diff katika wilaya ya Wajir, karibu na mpaka wa Somalia, lilitokea majira ya saa nne usiku siku ya Ijumaa na linadaiwa kufanywa na wapiganaji wa Al Shabaab, kutoka Somalia.

Mkuu wa polisi Joseph Boinnet amethibitisha kutokea kwa shambulio hilo na kusema kuwa maafisa waliweka upinzani mkali na kuwafukuzia mbali licha ya wapiganaji hao kuwa zaidi ya 100 wakiwa katika malori matatu na wakiwa na silaha nzito.

Kituo cha polisi cha Diff kilikumbwa na shambulio kama hili mwezi Aprili mwaka huu wakati maafisa watatu walipojeruhiwa na gari la polisi kuibiwa ambapo viongozi walisema wapiganaji karibu 100 wa Al Shabaab walishiriki pia katika uvamizi huo.

Saturday, 9 July 2016

Korea Kaskazini yarusha kombora la masafa marefu


Korea Kaskazini kwa mara nyingine imetekeleza jaribio la kombora lake la  masafa marefu kuelekea baharini.

Hili ndilo jaribio la hivi karibuni kutekelezwa na jeshi nchini humo kinyume na wito wa Umoja wa Mataifa pamoja na mataifa jirani kama Korea Kusini na Japan kuitaka kuacha majaribio hayo kwa sababu za kiusalama.

Jaribio hili limefanyika licha ya kuwepo kwa azimio la Umoja wa Mataifa kuzuia nchi hiyo ambayo inaendeleza mpango wa kutengeneza silaha za Nyuklia kwa lengo la kushambulia mataifa ya Magharibi.


Hili ni jaribio  la nne kuwahi kutekelezwa na Pyongyang tangu mwezi Januari mwaka huu wakiwa na lengo la kuwa na silaha za masafa marefu kuishambulia Marekani.

Nchi za Marekani na Korea Kusini zimekubaliana kuweka mpango wa pamoja kutega mitambo maalum kuzuia mashambulizi kama haya katika siku zijazo.

Jeshi la Polisi Nchini latoa sababu za kuzuia mikutano ya Siasa kufanyika hadharani


Jeshi la polisi nchini limeendelea kusisitiza msimamo wake wa kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa mpaka hapo hali ya usalama itakapotengemaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kamishina wa polisi operesheni na mafunzo makao makuu ya jeshi la polisi nchini Nsato Mssanzya amesema jeshi la polisi halitakubaliana na kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa ambazo  zinaweza kuchochea uvunjifu wa amani kwa jamii.

Kamishna Mssanzya amesema jeshi la polisi litaendelea kuimarisha hali ya usalama kwa wananchi wake ikiwemo kulinda usalama wa raia na mali zao huku likiwataka baadhi ya wanasiasa kufuata sheria na taratibu ambazo zimewekwa.

Mssanzya amesema jeshi la polisi limepiga marufuku maandamano pamoja na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa huku likifafanua kuwa jeshi hilo halitaingilia mikutano ya ndani inayofanywa na vyama hivyo.

Wanajeshi zaidi wauawa Sudan Kusini


Taarifa kutoka Sudan Kusini zinasema mamia ya watu, wengi wao wakiwa ni wanajeshi wameuawa katika mapambano baina ya vikosi vyenye uhasama katika mji mkuu wa Juba.
Mwandishi mmoja wa habari aliyeko mjini Juba amesema mapigano yameendelea mpaka mapema saa za asubuh ya Jumamosi.

Wanajeshi wametanda kwenye mitaa huku watu wachache wakionekana kutoka nje.
Daktari mmoja amesema mili mingi imepelekwa hospitali huku chumba cha kuhifadhia maiti kikiwa kimejaa.

Mapigano baina ya wanajeshi watiifu wa Rais Salva Kiiri dhidi ya Makamu wa rais Riek Machar yalianza tangu siku ya Alhamis.

Sudan Kusini inatimiza miaka mitano ya Uhuru na kuanzishwa kwake lakini hakuna sherehe zitakazofanywa.

Mabalozi wa Urusi wafukuzwa Marekani


Imebainika kuwa Marekani iliwafukuza maafisa wawili wa Urusi mwezi uliopita kufuatia kushambuliwa kwa mwandiplomasia wa Marekani mjini Moscow.

Afisa wa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni aliseme kuwa shambulizi hilo ambalo lilifanywa na mlinzi raia wa Urusi nje ya ubalozi wa Marekani, halikusababishwa na uchokozi.

Urusi inasema kwa mwanadiplomasia huyo alikuwa amemgonga mlinzi huyo usoni.

Marekani inailaumu Urusi kwa kuwadhulumu wanadiplomasia wake na familia zao.

Baba akesha akilinda wanawe walemavu wa ngozi


Ni mwendo wa saa nne toka jiji la Kampala nchini Uganda hadi kuyafikia makazi ya bwana Mwanje na wake zake wawili Lynda na Florence. Ni katika makazi haya bwana Mwanje ndipo anaishi na watoto wake nane wanaokadiriwa kuwa na miaka mitano hadi kumi na tatu huku watano kati yao wakiwa na ulemavu wa ngozi.

Na watoto wote watano wenye ulemavu wa ngozi amezaa na mkewe mkubwa Florence, wataalam wanaeleza kuwa ulemavu wa ngozi unatokana na upungufu wa madini ya melanin yanayohusika kuweka rangi ya ngozi, macho na nywele.

” Mara ya kwanza kupata mtoto mwenye matatizo ya ulemavu wa ngozi niliogopa sana, sikujua nini nitafanya, mwishowe niliamua kumpenda, nilimpenda zaidi” alisema bwana Mwanje.

Katika familia nyingi kumpata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ni tatizo, wengi wao huwaficha ndani kwa kuogopwa kuchekwa na majirani, hii inatokana na imani potofu inayoenezwa dhidi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi.

Kuna baadhi ya wanaume ambao huwatelekeza wake zao baada ya kuzaliwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi” kuna mambo mengi yasiyo ya kweli katika jamii yangu kuhusiana na wanangu watano kuwa walemavu wa ngozi, wanasema nilimcheka mtu mwenye ulemavu wa ngozi nilipokuwa kijana na akanipa laana na ndiyo sababu ya wanangu kuwa na ulemavu wa ngozi” alisema Florence mke mkubwa wa bwana Mwanje.

Kumekuwa na imani potofu kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi katika nchi zote za Afrika Mashariki, wapo wanaoamini miili ya watu wenye ulemavu ina nguvu ya kutajirisha watu maskini na kuwa matajiri wakubwa. Pia wapo wanaoamini wao ni mizimu ya kweli na siyo binadamu.

Katika nchi ya Tanzania na Malawi kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kutekwa na baadaye kuuwawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na baadhi wakikatwa viungo vyao wa mapanga wangali wazima, kifupi watu wenye ulemavu wanaishi kwa hofu kubwa kulingana na imani hizo kandamizi na potofu.

Nchini Uganda hali tofauti na nchini Tanzania na Malawi lakini ubaguzi wa wazi wa watu wenye ulemavu nchini Uganda ni jambo la kawaida. Katika shule nyingi wanafunzi wanagoma kukaa na watu wenye ulemavu wa ngozi kwenye dawati moja.

” Nilitaka wanangu wapate elimu bora, nikaamua kuwapeleka shule bora lakini tatizo shule iko mbali na makazi yangu, hivyo nilihofia wanangu wanaweza kutekwa. Kwasasa wanasoma shule ya kawaida iliyo jirani na makazi yangu” alisema bwana Mwanje.

“ Jambo lililowahi kunitia hofu zaidi, siku moja mwanagu Robert na wenzake walikuwa wakicheza jirani na shamba langu la mpunga. Mpaka jua linazama walikuwa bado porini wakicheza ghafla walimwona mtu kajificha na akaanza kuwafukuza hali iliyosababisha kila mmoja akimbilie uelekeo wake.

Robert alikimbilia uelekeo wake na wenzake uelekeo mmoja, kutokana na kelele za watoto yule mtu naye alikimbia na mpaka leo hatutajua alikuwa nani na lengo lake lilikuwa nini.” Alisema bwana Mwanje huku akionesha hali ya huzuni na wasiwasi.

“Tangu tukio hilo litoke natumia muda mwingi kukaa jirani na watoto wangu kuhakikisha usalama wao. ”
“ kuna muda napatwa na machungu watoto wangu wanaponiuliza kwanini wako tofauti na sisi, nawajibu kuwa hakuna kitu kibaya, wote tupo sawa ndani ya miili yetu.”

Waziri Mkuu wa India kufanya ziara nchini


Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi anawasili leo nchini kwa ajili ya ziara ya kitaifa ya siku mbili kwa lengo la kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema Modi atatumia fursa hiyo kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya nchi hizi mbili pamoja na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi.

Alisema Modi atakutana na Rais John Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo. Pia kuweka saini kwenye mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya sekta za viwanda, maji, elimu, sayansi na teknolojia na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.

Dk Mahiga alisema Modi pia atazungumza na jumuiya ya wafanyabiashara wakubwa wa India ambao baadhi yao wameshaonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa viwanda vya kutengeneza chuma, saruji, dawa ya binadamu na maji ya matunda.

“Natoa mwito kwa wafanyabiashara mbalimbali hapa nchini watumie fursa hii kushiriki ili waweze kukutana na wenzao, Kongamano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi,” alisema.

Jerry Muro anusurika ajalini


Muda mchache baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kumfungia mwaka mmoja Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro, bahati mbaya kapata balaa jingine.

Kwa mujibu wa salehjembe. blogspot, Muro amekumbana na ajali ya gari akiwa njiani kutoka Machame kijijini kwenda Machame mjini ambako yuko mapumzikoni.

Gari alilokuwa akiendesha liliteleza na kwenda kugonga kwenye karavati na tairi kupasuka.

“Hakika nimenusurika, unajua huku Machame ni milima. Halafu sasa kuna utelezi kutokana na mvua ingawa si kubwa, sasa wakati nateremka, gari likateleza na kwenda kugonga lile karavati,” alisema Muro.

“Lakini namshukuru Mungu, nimepona. Nilipata shida kupiga jeki kwenye tope mwisho nimefanikiwa na baada ya hapo nitaanza safari ya kwenda Dar es Salaam.”

Muro amefungiwa bila ya kupata nafasi ya kujitetea kwa kuwa wakati barua ya mwito kwenda TFF kwa ajili ya kusikilizwa inapelekwa, yeye alikuwa Machame mapumzikoni kwa ajili ya sikukuu.

Korea Kaskazini yawatishia amani Korea Kusini na Marekani


Marekani na Korea Kusini zimekubaliana kuweka mfumo wenye utata wa ulinzi dhidi ya makombora, kama njia ya kukakabiliana na vitisho vinayoendelea kutoka kwa Korea kaskazini.

Mfumo huo wa ulinzi unaowekwa katika maeneo yenye milima mirefu kudhibiti mashambulizi ya makombora utawekwa kujibu vitisho tisho kutoka Pyongyang, ilieleza taarifa. Haijabainika wazi ni wapi mtambo huo utawekwa na hatimae ni nani ataudhibiti.

Namna mfumo wa kukabiliana na Makombora (THAAD) unavyofanya kazi
Uchina, ambayo imekuwa ikipinga mara kwa mara mpango huo, imepinga mfumo huo tena kupitia wajumbe wa korea Kusini na Marekani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uchina amesema kuwa mfumo wa THAAD utadhuru amani na utulivu katika kanda hiyo, licha ya uwezo wake wa kugundua na kulipua makombora ya Korea Kaskazini.

"Uchina inaelezea kutoridhishwa kwake na kupinga vikali hili'', ilisema katika taarifa kupitia mtandao wake.

UN yawatia hatiani Wanajeshi wa Burundi kwa ubakaji


Umoja wa Mataifa unasema, wanajeshi wake wa kulinda amani waliowanyanyansa kimapenzi wasichana wadogo katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakolinda amani ni kutoka Burundi.

Imebainika kuwa wanajeshi hao ndio waliwanyanyasa wascihana wawili, mmoja mwenye umri wa miaka 12 na mwingine mwenye umri wa miaka 18 mwezi Mei mwaka huu.

Msemaji wa UN Stephane Dujarric amesema uchunguzi binafasi unafanyika na huenda wanajeshi hao wakajarudishwa nyumbani.


Upande wa jeshi la Burundi hawajazungumza lolote kuhusu vitendo hivyo viovu wanavyoshutumiwa baadhi ya askari wa Burundi waliojiunga katika kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Askari wa kulinda amnai wa Umoja wa Mataifa wamekua wakinyooshewa kidole kwa visa kama hivyo katika nchi mbalimbali wanakolinda amnai.

Hivi karibuni Baadhi ya askari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walishtumiwa kujihusisha na vitendo hivyo viovu, na baadaye kuchukuliwa uamuzi wa kuwarejesha nyumbani.

Ndoa za utotoni Tanzania kukoma


Mahakama kuu nchini Tanzania leo imeidhinisha umri halisi wa kuolewa kwa mtoto wa kike kuwa miaka 18. Wasichana wenye umri wa miaka 14 huolewa kwa ridhaa ya wazazi wao.

Mahakama kuu imetoa muda wa mwaka mmoja kuhakikisha kuwa Serikali inasahihisha sheria ya mwaka 1971 kifungu cha 13 kinachoruhusu Mtoto wa kike kuozwa akiwa na umri miaka 14
Wasichana wanaoolewa katika umri huu mara nyingi wanakabiliwa na unyanyasaji wa majumbani sambamba na kutengwa na jamii huku wakipewa nafasi ndogo kwa ajili ya elimu na ajira.

Huu ni ushindi mkubwa kwa wanaharakati wa Tanzania katika kupigania haki za watoto na sasa itakuwa rahisi kuwaokoa wasichana wanaoathirika na utamaduni wa kuozeshwa wakiwa wadogo.

Uamuzi huu umekuja wakati Bunge kupitisha sheria ya kifungo cha miaka 30 ama faini ya dola 2500 kwa mwanaume atayebainika kumuoa ama kumpa mimba mwanafunzi.Hata hivyo sheria hii inawatenga maelfu ya wasichana ambao si wanafunzi.